Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ANNA L. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi na naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetulinda, ametuleta tena mara nyingine hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja kwenye hoja, naomba nimpongeze Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanazozifanya. Wizara yao ni kubwa sana lakini wanajitahidi sana, wana majukumu mazito, naomba mpambane Mungu atawasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Katavi sasa hivi una miaka kama minne inaelekea mitano, hatuna Hospitali ya Mkoa. Tumeambiwa tumetengewa pesa tujengewe Hospitali ya Mkoa wa Katavi lakini mpaka leo hatuoni jitihada ya aina yoyote. Sasa hivi Mkoa wa Katavi una watu wengi, ukishasema mkoa ina maana umepanua wigo mkubwa kwa hiyo, shughuli mbalimbali zinafanywa ndani ya Mkoa wa Katavi lakini hatuna Hospitali ya Mkoa, tumebaki na Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ambayo ndiyo imebeba majukumu yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ni ndogo na wafanyakazi ni wachache, nashukuru na wao wenyewe wamejionea. Wameainisha hapa kwenye hotuba ndani ya Mkoa wetu wa Katavi ukiangalia Wilaya ya Mpanda Vijijini, Mpanda Mjini na Wilaya mpya ya Mlele kuna sehemu wamesema asilimia 100 hakuna wahudumu. Sasa sijui wananchi wa Mkoa wetu wa Katavi wanaoumwa wanafanyaje. Naomba Mheshimiwa Waziri uliangalie kwa makini sana suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi wamekukaribisha uende kwenye Mikoa yao, naomba Mheshimiwa Waziri uje Katavi ujionee mwenyewe hali halisi ya Mkoa wetu na jinsi wananchi wanavyopata shida ya matibabu. Hospitali ile ya Wilaya, manesi pamoja na madaktari saa nyingine wanachoka, wakichoka sasa lugha zinakuwa tofauti. Wagonjwa wakienda pale kauli zinakuwa tofauti, zinakuwa mbaya kwa sababu si wao, wamechoka. Naomba Mheshimiwa Waziri muangalie kutupatia Hospitali ya Mkoa wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mlele ina hospitali ambayo imejengwa na Serikali. Naomba niipongeze Serikali imejenga hospitali nzuri sana Inyonga lakini mpaka leo ni kituo cha afya. Mmeweka vifaa vingi na vizuri lakini kasoro yake ni ndogo sana, ni choo tu hakuna ndiyo imefanya hamtaki kuipandisha iwe Hospitali ya Wilaya ina maana Wilaya ya Mlele hakuna Hospitali ya Wilaya. Mheshimiwa Waziri tunaomba tupandishie hii hospitali na tuletee wafanyakazi. Vile vifaa mlivyoleta vimekaa sasa vimeanza kuharibika kwa sababu hakuna wataalam wa kuvitumia. Sasa inakuwa tunachezea hela za Serikali kututangulizia vitu wakati wahudumu na wataalam hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hospitali ambayo iko Inyonga imejengwa vizuri sana lakini tatizo lake ni choo tu. Mmejenga majengo makubwa, mazuri, lakini sijui ilikuwaje huyo mkandarasi aliyewekwa hakuweka choo mpaka leo hii tunashangaa ilikuwaje. Kila mtu anashangaa kwa sababu tunaomba muipandishe hadhi inashindikana, ukiuliza tatizo unaambiwa hamna choo. Sasa sijui katika utaalam ilikuwaje, mmejenga majengo mazuri, mmeleta vifaa vikubwa na vizuri halafu choo hakipo halafu hamtaki kutoa kibali ili iwe Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu mkubwa naomba mtusaidie kwani wananchi kule wanapata shida, jiografia yetu ya Mkoa wa Katavi jamani ni ngumu, naomba chonde chonde mtusaidie. Ukienda kule Mheshimwa Waziri utasikitika wananchi wanavyohangaika huduma hamna. Naomba Mheshimiwa Waziri ile hospitali hata kama haina vyoo tupandishieni iwe na hadhi ya Hospitali ya Wilaya ili wananchi wa Wilaya ya Mlele wapate huduma safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja upande wa Chuo chetu cha Msaginya. Tuna chuo pale kinaitwa Msaginya, Chuo cha Maendeleo lakini hakifanyi kazi yoyote. Chuo kile ni kizuri, mnakitolea pesa kila mwaka, lakini kwa nini hamna mipango mizuri mkapeleka watu wakajifunza pale? Kuna vijana wengi ambao wamekaa bure hawana kitu chochote cha kufanya wangeenda huko. Vyuo mmevijenga vizuri, wataalam mmewaweka kwa nini vijana wasiende pale wakajifunza useremala na akina mama wakaenda pale wakajifunza ujasiriamali? Vile vyuo majengo yanaharibika na mnapoteza hela nyingi.
Naomba hivi Vyuo vya Maendelo ya Jamii viwekewe mikakati mikali ili vijana wengi wajifunze ujasiriamali kupitia Vyuo hivi vya Maendeleo ya Jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja upande wa Benki ya Wanawake. Kwanza, naomba nimpongeze Mkurugenzi wa Benki ya Wanawake, Mama Chacha, amefanya kazi nzuri lakini bado hajatufikia sisi akina mama kwenye Mikoa, Wilaya na Vijiji vyetu, ameishia Dar es Salaam na asilimia kubwa ya akina mama wako vijijini. Najua watu wengi wamesema hii benki haiwezekani lakini wanawake wote wana haki ya kupata benki hii kila mkoa kwa sababu hela iliyochukuliwa kuianzisha ni Serikali. Kwa hiyo, kila mkoa tunahitaji Benki ya Wanawake ili wanawake wa Tanzania hii wajivunie benki yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sasa kuzungumzia Bima ya Afya, hii mimi naisemea kila siku. Bima ya Afya dawa hakuna! Tunaomba sasa Bohari Kuu waende moja kwa moja viwandani kuchukua dawa. Kama dawa ziko huko Ujerumani, India waende moja kwa moja wakachukue dawa huko ili waje kuwahudumia Watanzania. Hizi dawa wanazochukua kwa wafanyabiashara hazikidhi mahitaji.
Tunaomba sasa Serikali iwape fungu kubwa Bohari Kuu ya Dawa ili sasa wananchi wote waweze kupata huduma safi na salama wajivunie Serikali yao kupitia Bima ya Afya. Sisi tuko tayari kufanya hamasa, wananchi wote waingie kwenye Mfuko wa Bima ya Afya lakini tunaomba mtuwekee dawa ili wananchi wapate huduma safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana.