Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii. Kwanza namshukuru sana Mungu kwa kunijalia nafasi ya kuwepo hapa. Pamoja na hayo yote, naomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa bajeti hii ya kwanza na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na msaidizi wake Mheshimiwa Masauni kwa bajeti yenu ya kwanza hii. Nina ushauri na kwa sababu muda ni mfupi, naomba niende haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tunakuja huku mara nyingi kuwawakilisha wenzetu hasa Madiwani; kwenye maeneo mengi ya mafao yao/posho zao; sasa kwa sababu Madiwani wengi mara nyingi wamekuwa waki-suffer kutokana na namna ambayo wanalipwa, kwanza nawapongeza kwa sababu Serikali imekubali zile hoja za Wabunge ambazo zilikuwa zinaletwa humu, nawe Mheshimiwa Naibu Spika alileta hoja hapa ili walau Madiwani walipwe kwenye accounts zao kama Serikali ilivyosema.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri mwingine ambao sasa kwa kuwa Madiwani hao wana wigo mkubwa na ziko kata nyingine kwa mfano kule Mbulu Vijijini ni kubwa na ni pana, hawana uwezo wa kuizunguka kwa mara moja. Sasa naomba Serikali iangalie kwenye bajeti hii waweze nao kupewa mikopo kama tunayopewa Wabunge ili mikopo hii basi ikawasaidie. Aidha, wapewe usafiri na iandikwe kabisa na ziwe katika principal ambazo wao wenyewe wanaweza kulipa kutokana na fedha ambazo watapewa na kuongezewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kiinua mgongo cha Mheshimiwa Diwani ni kidogo sana, lakini posho ile ikiongezwa ni wazi kwamba unaweza kuangalia katika mafao haya anaweza kukopeshwa nini? Aidha, kama ni gari dogo au pikipiki. Kwani hawa ni wawakilishi wetu wa kutosha katika maeneo ya kata zetu, kwa hiyo, naomba hili lizingatiwe sana. Kwa sababu hii basi, wataweza kusimamia miradi, maana miradi mingi katika maeneo yetu wanapaswa kusimamia kwa ukaribu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Kamati ambayo inaweza kusimamia miradi ni Kamati ya Fedha kwa mujibu wa sheria na inapata nafasi ya kuzunguka mara nyingi katika maeneo ya Halmashauri. Kwa hiyo, unapompa na kumwezesha Diwani akaweza kuzunguka maeneo haya ni wazi kabisa miradi itasimamiwa kwa karibu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwa kuwa sasa Halmashauri imeshaondolewa mzigo wa ulipaji wa hii posho na mishahara ya Madiwani, napendekeza, tuna Wenyeviti wa Vijiji ambao bado hawajakumbukwa, naomba Mheshimiwa Waziri aangalie na Serikali ione, Wenyeviti wa vijiji asilimia 20 inayotajwa kwenye kanuni zetu haziwafikii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kwa sababu mshahara ule wa Madiwani umeshaondolewa kwenye Halmashauri kwa kupitia mapato ya ndani, kwa nini fedha hizi zisiende basi tukawapatie Wenyeviti wa Vijiji hata allowance kidogo tu? Hata kama siyo mshahara, basi posho ya mwezi kidogo tu ili Mwenyekiti wa kijiji aone kwamba aah; awe na utaratibu, maana ukiangalia katika mtindo wa sasa hivi, Mtendaji wa Kijiji analipwa fedha. Kwa hiyo, inaonekana Mtendaji wa Kijiji ni bosi wa Mwenyekiti kumbe kwa kawaida kabisa Mwenyekiti wa Kijiji ni bosi na ana Serikali yake ya Kijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Serikali zote ambazo zimeachwa kidogo, ni Serikali ya Kijiji. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Serikali kwa Wizara ya Fedha ione ni namna gani, kama siyo bajeti hii, basi bajeti ijayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Wenyeviti wa Vitongoji ni wa msingi sana kwa sababu wao ndio wanaotoa habari, wanaotoa taarifa na ndio wanaoandaa mikutano, ndio wanaotekeleza sera zote na ndio wakusanya michango. Kwa hiyo, hata hao wanapokusanya michango waonekane basi. Serikali ipange utaratibu wa namna fulani, hata wao fedha chache ziwe zinawafikia. Hata wao isiwe kama bakshishi, iende kwenye account. Maana siku hizi kila mtu ana account, waelekezwe hao wapate na fedha kidogo hata kama fedha zenyewe ni chache, lakini ajue kwamba anapata kiwango fulani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini wakishapata utaongeza morality katika Serikali kutoka kwenye ngazi ya Taifa hasa hadi kwenye vitongoji maana hao wote ni Serikali. Ukifanya hivi, Serikali hii itakuwa imejiwekea legacy; na Mheshimiwa Mwigulu utakuwa umejiwekea legacy kwamba, kwa kweli katika wakati wako umeweza kufanya hii ya kuwalipa Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Vitongoji na Madiwani sasa wanaenda kufaidika. Kwa hiyo, naomba hivi vyeo viwili visisahaulike, maana ni vyeo vya msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye miundombinu na hasa ya barabara. Duniani kote, uchumi hauwezi kwenda vizuri kama miundombinu iko vibaya na hasa miundombinu ya barabara. Naomba Serikali ione, mmeelekeza fedha kwenye barabara nimeona, lakini siyo kubwa sana, ni kidogo. Kwa hiyo, naomba elekeza maeneo haya kwa sababu wakulima wanapotoa mazao, wanapopeleka viwandani na uzalishaji unakuwa mkubwa, Serikali ni rahisi na kupata kodi na kukusanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, iko barabara ambayo kwa kweli nisipoisema naona kama sijafikisha ujumbe, ni barabara yetu moja ya Karatu – Hydom – Sibiti. Nashukuru kwanza Waziri amejibu swali langu leo na kwa kweli amesema inatangazwa kilometa 25. Kwa ajili hiyo nilishawahi siku moja kuomba hapa nipige sarakasi, hilo na-withdraw, leo sipigi hiyo, kwa sababu nimeona kwanza Serikali imekubali na inataka kujenga barabara hiyo. Ni vizuri kushukuru hata kwa kidogo, ni 25 zimetangazwa, nimeziona na imesemwa imetangazwa na ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, mmetangaza kilometa 25. Sasa kilometa 25 ni kipande kidogo sana. Kwa bahati nzuri hiyo barabara iko kwenye bajeti inaonyesha kilometa 50.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe basi, kwa sababu inaonyesha kilometa 50 na hii ni ahadi ya Rais, ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano na sasa ni ahadi ya Rais wa Awamu hii ya Sita, mama Samia Suluhu Hassan, alikuja akaisema barabara hii akiwa Dongobesh akiwa pia Haydom. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa itakuwa si vyema sana na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kwa sababu ni Waziri wa Fedha wewe barabara hii, lazima niseme tu ukweli kwa namna fulani ni mdau. Sasa niombe najua bajeti ni kidogo yaani rasilimali ni kidogo, lakini naomba mwakani uiwekee fedha ili walau basi isiwe katika ile hali imesemwa kwamba 25 kwa sababu barabara hii inapita Majimbo tisa; Jimbo la Karatu, Mbulu Mjini, Jimbo la kwangu la Mbulu Vijijini, Jimbo la Mkalama na inakuja mpaka Iramba na inakwenda mpaka Sibiti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo basi barabara hii itakapofunguliwa itakuwa imekidhi maeneo mengi sana kwa kuwapatia watu hawa huduma. Na unajua Mheshimiwa Dkt. Mwigulu barabara hii inaleta watu wa kwako wa jimboni kwako kuja katika eneo la Haydom Hospitali. Ni hospitali kubwa sana ya Kanda ambayo iko pale, naomba Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ajue, anapoanza kujenga hiyo barabara aangalie kwa sababu pale hizi kilometa 25 sijui utaanzia wapi? Na sio suala langu linakuwa la Mkandarasi, lakini angalia eneo hili la Haydom kwa sababu eneo hili ni oevu na pale kuna maeneo ambako hayafiki na hayafikiki. Basi uone ni namna gani ya kuanza kilometa 25, sikupangii uanze wapi lakini angalia eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ukiangalia, katika mpango huu wa bajeti, ninaifurahia sana. Lakini nitashukuru kuona kwamba, bajeti ya mwaka huu nimeona pia ipo kilometa zingine 25. Sasa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu wewe ni mtani wangu, unajua kabisa na yupo Mheshimiwa Msaidizi wako anayeitwa Comrade Masauni na nyinyi ni vijana wenzangu. Tumekuwa wote Jumuiya ya Vijana hebu wekeni kilometa hii 25 ijayo, ili zifike 50 na hii barabara ikamilike. Weka hiyo legacy basi bwana usitake nikaanza kuruka sarakasi huku na unajua hataniruhusu. Sasa kama haniruhusu rafiki yangu si uweke tu fedha mambo yaende vizuri. Kwa nini tuanze kuvunja Kanuni za Kibunge wakati wewe ni Mbwanee na Mbwanee ni Saitaa na Saitaa mambo yote mazuri. Brother weka hii fedha ili baadaye kule mzee tuzeeke tukiwa tuna barabara. Sasa hivi ni vijana brother na barabara hii inapita jimboni kwako, inakwenda mpaka Mkalama, inakutana kule kwa nini usiweke hii fedha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jamaa ameishia hapo kilometa 25, bajeti hii ya kwako hii. Bajeti ya Mama Samia Suluhu Hassan ya 2022 kwenda 2023 na wewe Mheshimiwa Engineer Masauni hapo wekeni barabara hii na Mheshimiwa Naibu Spika uko hapa na najua mtaweka barabara hii na Mungu atawabariki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishie hapa kwa sababu kengele imelia. Lakini nikushukuru sana wewe kwa kunipa nafasi hii na Mungu akubariki sana ahsante. (Makofi)