Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Bahati Keneth Ndingo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbarali

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kupata fursa nami niungane na Waheshimiwa Wabunge kuendelea kuipongeza Serikali ya Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa bajeti yake hii ya kwanza, nzuri kabisa ambayo imepokelewa kwa bashasha kubwa huko mtaani. Lakini pia niendelee kuipongeza Wizara ya Fedha kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kutuletea bajeti ambayo inakuwa ni chachu ya maendeleo kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwa kuongeza vyanzo vya mapato ya ndani. Tunaona bajeti hii inayokwenda kuisha tarehe 30 Juni, tulikuwa na vyanzo vya mapato ya ndani kwa asilimia 69, sasa kwenye bajeti hii tunatarajia kuwa na vyanzo vya mapato asilimia 72. Kwa hiyo ina maana tunakwenda kupunguza utegemezi wa bajeti na mikopo ya nje na wahisani kwa asilimia tatu. Siyo kazi ndogo niwapongeze sana kwa ubunifu wa kuibua vyanzo vipya vya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtakubalina na mimi na Waheshimiwa Wabunge ni kwamba kwa takribani miaka mitano iliyopita kuanzia 2014 mpaka 20219 Halmashauri zetu bado zimekuwa na changamoto ya kuweza kupata mapato ya kutosha. Kwa hiyo tumekuwa tukiipa Serikali Kuu mzigo mkubwa kwenye Halmashauri zetu. Tumeona kwamba kwa takriban kuanzia mwaka 2014 mpaka 2019 zaidi ya asilimia 85 ya Halmashauri zilishindwa kujigharamia matumizi yake ya kawaida. Hivyo zilipelekea kwamba Serikali Kuu iendelee kuzisaidia hizi Halmashauri. Kwa hiyo, utaona kwamba bado Serikali Kuu ina mzigo mkubwa ambao ni lazima kama Taifa tuje na mbinu mbadala za kuendelea kutafuta vyanzo vya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kuishauri Serikali, niliona katika Mpango wa Pili wa Serikali mliongelea Hati Fungani za Manispaa (Municipal Bonds) lakini pia niliona katika bajeti ya mwaka 2018/2019 Mheshimiwa Waziri wa Fedha kipindi hicho ni Makamu Rais sasa, alisisitiza kuendeleza Mpango ule wa kuanzishwa kwa Hati Fungani za Manispaa, ilielezwa Bunge lako Tukufu kwamba mmekwenda kufanyia training karibia Manispaa ya Mwanza, Arusha na nyinginezo na Tanga. Sasa, naona hili jambo pia limekuwa kama linasinzia. Hii nchi ni kubwa lazima tubuni halmashauri hizi zijiendeshe kibiashara. Tukisema halmashauri zote nchini ziweze kujiendesha kwa kutegemea Serikali Kuu tutakuwa tunajidanganya. Kwa hiyo niiombe sana Serikali iweke mkazo kwenye kuhakikisha wanamalizia uanzishwaji wa hizi Hati Fungani za Manispaa au Municipal Bonds.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana, kwenye bajeti tukatoe kipaumbele kwenye miradi ambayo itakwenda kuchochea uchumi kwa haraka. Leo hii tuna mradi mkubwa unakwenda kuanza wa Liganga na Mchuchuma lakini kama Serikali imeandaa mazingira ambayo yatakuwa wezeshi kwa mradi huu kutopatikana kwa vikwazo. Barabara zipo, miundombinu rafiki kwa ajili ya mradi huu ipo? Ni vitu ambavyo kama Serikali lazima tuhakikishe tunatoa vipaumbele kwenda kutekeleza bajeti yetu kwenye vyanzo ambavyo vitakwenda kuchochea uchumi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ukienda kule kwenye barabara za huko vijijini utaona jinsi kuna uwekezaji mkubwa kwa mfano, kuna uwekezaji mkubwa ulifanywa na Serikali ya Awamu ya Tatu kule kwetu Madibila, Mbarali. Waliwekeza zaidi ya bilioni 28 lakini leo hii hata barabara kufika kwenye yale mashamba hakuna. Ni jinsi gani Serikali inapoteza mapato kule kwa kukosekana tu barabara ile barabara ipo tangu Serikali ya Awamu ya Tatu imeahidiwa kwa wananchi kilomita 151 kutoka Rujewa, Madibila mpaka Mafinga kule kuna wakulima wa mbao, kuna uwekezaji mkubwa Serikali imetengeneza skimu za umwagiliaji kubwa lakini hakuna barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe sana Serikali, leo hii lango kubwa la biashara kwenye nchi za Southern Africa, Kusini mwa Afrika, (SADC) leo hii lango kubwa la biashara ni kule, barabara ile haifai kutoka pale Igawa mpaka Tunduma ni shida. Kwa hiyo, ni lazima kama Serikali tutoe vipaumbele kwenye maeneo ambayo yataweza kuchochea uchumi wa Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze TAMISEMI kwa kuwashirikisha Waheshimiwa Wabunge katika miradi mbalimbali inayoendelea. Niombe sana na Wizara nyingine zifanye hivyo kama Wizara ya Ujenzi wakae na Waheshimiwa Wabunge, Wabunge hawa wanajua barabara ambazo zitakwenda kuchochea uchumi kwenye Majimbo yao. Kwa hiyo niwaombe sana na Wizara nyingine muwape kipaumbele Waheshimiwa Wabunge wa Majimbo yao ili waweze kujadiliana nanyi na kuwapa kipaumbele ambacho kitasaidia kujua ni nini kipaumbele cha vitu ambavyo vitachochea uchumi katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninashukuru sana kwa kupata fursa, naunga mkono hoja. (Makofi)