Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buchosa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu kwa Taifa langu katika bajeti hii ya mwaka 2021/2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijazungumza mengi, naomba nitoe shukrani nyingi sana kwa Serikali ya Awamu ya Sita; kwa Mheshimiwa Rais kwa mambo ambayo mimi peke yangu, sijui kwa wenzangu; amenitendea kwenye jimbo langu. Katika historia, tangu mwezi Januari mpaka Aprili, nimeshapokea karibu shilingi bilioni tatu za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo, mimi na Wabunge wenzangu tulipata nafasi ya kukutana na Mheshimiwa Rais kabla hajaja Mwanza kwenye kikao kidogo, nikawa nimeomba kupewa kituo cha afya kwenye Kisiwa cha Maisome. Ni jana Waziri wa TAMISEMI, dada yangu Mheshimiwa Ummy, alinipigia simu ya kwamba kituo hicho kitajengwa. Kwa hiyo, natumia nafasi hii kuishukuru sana Serikali hii kwa usikivu na namna ambavyo inafanya kazi kuwatumikia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango nitakaoutoa leo nilikuwa nimetarajia kuutoa wakati wa Wizara ya Afya, lakini bahati mbaya nafasi haikupatikana. Hata hivyo, kwa sababu tuna Wizara ya Fedha na Waziri wa Fedha yuko hapa na ndio mpangaji wa ceiling za kisekta na Wizara zote, ni vizuri nikazungumza suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna uhusiano mkubwa sana (correlation) kati ya afya za watu na maendeleo ya Taifa. Kuna uhusiano mkubwa sana. Wanasema there is a correlation between the wellbeing of the people and socio-economic development. Nchi yoyote ambayo watu wake hawana afya, haiwezi kuwa nchi yenye maendeleo. Nchi yoyote ambayo vijana wake ni wagonjwa, haiwezi kuwa nchi yenye maendeleo. Kwa hiyo, kuna umuhimu wa kuwa na Taifa lenye afya. Watu wenye afya wataleta maendeleo ya nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama huo ni ukweli, nataka nikurejeshe wewe na Wabunge wenzangu kwenye Azimio la Abuja. Mwaka 2001 mwezi Aprili, nchi zote za Afrika ikiwemo Tanzania chini ya OAU, walikutana Abuja na zikakubaliana na wakaazimia ya kwamba fifteen percent ya annual budget itaelekezwa kwenye huduma za afya. Hayo yalikuwa ni makubaliano. Hayati Mzee Mkapa alikuwa pale na wote walikubaliana na nchi zote zikakubaliana kwamba kila tunapopanga bajeti yetu, asilimia 15 lazima iende kwenye afya kwa sababu tunataka kujenga Taifa la watu wenye afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, miaka 20 baadaye; nina habari ya kusikitisha kuhusu azimio hilo ya kwamba hatujaweza bado kutimiza suala hilo, nafahamu ya kwamba tuna matatizo ya bajeti, uchumi kwenda taratibu, lakini ipo sababu ya Wizara ya Fedha kutazama na kupanga jinsi ya kuiwezesha Wizara ya Afya iweze kutimiza majukumu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka 20 baadaye, nitakupa mfano wa mwaka 2017 na 2018 tulikuwa asilimia 7 tu, ya bajeti yetu kwa Wizara ya Afya na hiyo ilikuwa chini ya azimio la Abuja ambalo lilitaka asilimia 15. Mwaka 2018/2019 tulishuka na kwenda asilimia 6.7 inaendelea kushuka bajeti ambayo inatakiwa kuhudumia afya ya watu wetu. Mwaka 2021/2022 bajeti tunayoijadili hapa leo tumeshuka mpaka asilimia 2.7 maana yake nini, maana yake ni kwamba tuna bajeti ya trilioni 1 kwa afya, lakini tuna trilioni 36 annual budget hiyo peke yake inaashilia ya kwamba tumeshuka mpaka 2.72 percent hiyo ndiyo allocation yetu kwa afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina wasiwasi kama tunaweza kuwa na Taifa lenye afya kwa bajeti ambayo tumeipanga kwa mwaka huu. Nafahamu kabisa ya kwamba tuna matatizo kama nchi, nafahamu ya kwamba mnahitaji kufunga mkanda kama Taifa. Lakini afya za watu wetu ni kitu cha muhimu sana na kikubwa kabisa ambacho nataka nikizingumzie hata hiyo kidogo ambayo tunaipata, tunai-allocate yote huwa haiendi kwenye wizara. Tunawezaje kuwa na Taifa lenye afya linaloweza kujenga ustawi wa watu wake wakachangia utumishi wake, hatuwezi mpaka tuweze kuhakikisha ya kwamba hata kama hatuendi 15 percent, lakini lazima tuweze kupandisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna kodi hapa, kodi mpya tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri, tumekuja na kodi mpya, kodi ya simu, kodi ya majengo, kwenye mafuta tumeweka shilingi 100 na fedha hizi zimeelekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu, kwenye elimu, kwenye maji na vilevile kwenye afya, ndiyo maana nazungumza hapa leo ya kwamba ipo sababu kubwa sana ya Mheshimiwa Waziri atakavyopata fedha hizi azielekeze kwenye afya za watu wetu ili bajeti iweze kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikupe mfano, mfano huu ni wabajeti ya Wizara ya Afya mwaka 2019, nitakueleza jinsi ilivyogawanywa, asilimia 41.9 kwa mujibu wa health forum chini ya UNICEF ilielekea Wizara ya Afya na nyingine asilimia 40.7 ilielekea kwenye TAMISEMI ambayo ndiyo watekelezaji wa Sera huo ndiyo ulikuwa mgawanyo, nyingine ikaenda NHIF asilimia 10, nyingine 0.4 ikaenda TACAIDS sasa tuachane na hizo zilizoenda TAMISEMI tuachane na hizo zilioenda NHIF na TACAIDS.
Mheshimiwa Naibu Spika, twende moja kwa moja kwenye iliyokwenda Wizara ya Afya, nionyeshe namna ambavyo fedha hiyo iliweza kutumika na nionyeshe ni kiasi gani kama Taifa hatupo serious kwenye suala la kuzuia magonjwa yasitokee.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokifanya ni kama tunatamka hivi ugueni mkishaugua mje tutawatibu, kama Taifa nimeona hatuna capacity ya kuwatibu watu wote wanaougua ipo sababu ya kuyazuia magonjwa kabla hayajatokea. Leo hii wote tunafahamu ya kwamba kansa inatafuna Taifa letu, lakini wangapi wanafahamu ya kwamba kansa inayotusumbua inasababishwa na Aflatoxin sumu kuvu ambayo ipo kwenye mazao. Niishukuru sana Wizara ya Kilimo wanajenga ghala kwenye jimbo langu kwa ajili ya kuhifadhi mazao ili watu wasiweze kuhifadhi mazao vibaya hatimaye kukawa na sumu kuvu ikawasababishia kansa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo ni suala la elimu tu, ni elimu peke yake ikitolewa hapa nchini watu wataweza kuepuka kansa inayosumbua Taifa. Wizara ya Afya asilimia 41.6 inayokwenda kule 33.5 inalipa mishahara, asilimia 31.8 inakwenda kwenye capacity building mambo ya kuelimisha watu, kuelemisha watumishi wetu wa wizara ya afya ili waweze kufanya kazi vizuri, sina tatizo lolote na capacity building hata kidogo ni sawa, lakini asilimia 31.8 capacity building, asilimia 7.1 inakwenda kwenye tiba, sasa sikiliza hapa, asilimia ngapi inakwenda kwenye preventive medicine, asilimia inayokwenda kwenye preventive medicine ni asilimia 3.7, tunawezaje kuzuia watu wetu wasiugue kwa asilimia 3.7? Hiyo ndiyo hoja yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nazungumza hapa leo natoa mchango wangu kumkukumbusha Mheshimiwa Waziri na nimeikubali bajeti yake na haya kama hayatafanyiwa kazi hivi sasa, yafanyiwe kazi huko mbele tuongeze bajeti yetu kwenye preventive medicine asilimia 3.7 haitoshi kuzuia watu wetu wasiugue.
Mheshimiwa Naibu Spika, napozungumza hapa leo, tarehe hii ya leo infant mortality rate kwenye Taifa letu, watoto wanaokufa chini ya miaka mitano wanakufa watoto 60 katika kila watoto 1000, katika kila watoto 1000 watoto 60 wanakufa. Navyozungumza leo kwa mambo ambayo yangeweza kuzuiliwa kwa elimu peke yake, leo ninapozungumza hapa, leo siku ya leo, jioni ya leo mortality rate ya kinamama wanaojifungua ni wakina mama 558 katika kila vizazi 100,000, tunawapoteza wakina mama wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wiki mbili zilizopita mama kapoteza maisha akiwa ndani ya Mtumbwi anaenda hospitali mtoto katanguliza mkono, tutawazuiaje wakina mama wasiendelee kufa mpaka tutenge elimu, pesa ya kutosha, wakina mama wetu wasiendelee kuugua, inawezekana. Navyozungumza leo hapa hepatitis B, Homa ya Ini ni asilimia 6 watu wengi wana Homa ya Ini tunaweza kuwazuia kwa kuwachanja watu wetu kuna shida gani kama NHIF wakikubali Chanjo ya Homa ya Ini iingie kwenye Bima ya Afya?
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuendelea kupoteza maisha ya watu wetu ni lazima sasa Mheshimiwa Waziri akumbuke suala la muhimu sana kwenye Taifa hili preventive medicine tuzuie watu wetu wasiugue kwa kuongeza bajeti angalau kutii azimio ambalo tulilisaini wenyewe, Azimo la Abuja, Abuja declaration. Nchi yetu inapita kwenye wakati mgumu na ninafahamu nani wajibu wetu kama watanzania kujua tunawezaje kufunga mkanda ninachokiomba, Mheshimiwa Waziri nakusihi rafiki yangu wakumbuke Wizara ya Afya uokoe maisha ya watu ambao hawatakiwi kuugua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)