Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtwara Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti. Kwanza nianze kwa kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini niwashukuru wasaidizi wake kwa ujumla nimshukuru Waziri wa Fedha na Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie dakika tano hizi kwa mambo kidogo ya msingi, tunapotaka kuzungumza uchumi wa nchi yetu lazima tujikite kwenye viwanda, lakini tunapotaka kuzungumza uchumi wa nchi yetu lazima tujikite kwenye kilimo, lazima tuwe na watu ambao wana nguvu za kutosha na watu wenye uelewa. Nini maana yake?
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu walizungumza kuhusiana hapa na vijana ambao wapo mtaani wamachinga. Genge hili la wafanyabiashara wadogo wadogo limekuwa ni kubwa mno, lakini bado sijaona kama Serikali ikiwa inajikita kuelekeza wapi iwapeleke hawa watu. Lakini nataka nitoe mfano mmoja, vijana hawa wanapanga biashara barabarani, lakini vijana hawa tayari wanafamilia zao majumbani kwao. Imetokea siku kijana huyu ambaye yupo barabarani ameumwa, kwa hali ya kawaida hawezi kumchukua mkewe aende pale barabarani akapange zile nyanya au akapange zile nguo zake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa jambo lingine kwenye wamachinga hao hao kwa hali na mazingira ambayo yapo, hatuwatengenezi hawa vijana kwenda kujitegemea. Kwa sababu, kwanza hawana insurance hawakopesheki kwenye mabenki vijana hawa. Sasa, rai yangu tunayo maeneo sisi ya kutosha, maeneo haya Serikali sasa ifike mahali itambue kwamba, inaweza ikawajengea maeneo ya kisasa. Kwanza, faida yake baada ya kuwajengea maeneo ya kisasa tutaweza kupata kodi, vilevile kwenye fursa sasa ya kuwajenga vijana wetu kutoka kwenye umachinga kwenye wafanyabiashara wakubwa. Nina imani kubwa sana hata Mheshimiwa Shigongo ametokea kwenye umachinga, lakini leo amekuwa mfanyabiashara mkubwa kwa sababu yeye aliwezeshwa. Ninaiomba Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie masuala ya bandari na uchumi. Masuala ya bandari na uchumi tunazo bandari katika nchi yetu, lakini napenda sana niizungumzie bandari ya Dar es Salaam, niizungumzie bandari ya Mtwara. Ukiangalia bandari ya Dar es Salaam kwa shughuli zinazofanyika kila siku, bandari ile inaonekana kwamba iko tight. Lakini kwa nini tusifike pahali tukapanua wigo tunayo bandari ya Mtwara tunayo bandari ya Tanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tukienda pale Dar es Salaam tunakuta zaidi ya meli 20 au 30 ziko hangar zinasubiri kupakua pale mzigo, lakini bado tunawapelekea kupata hasara kubwa jinsi meli inavyokaa kule hangar inasubiri iingie pale. Kuna service charge ambazo zinaingia kutokana na gharama za watu ambao wamekodi meli zile. Rai yangu, tutumie bandari sasa ambazo tayari zina uwezo wa kubeba hizo meli kubwa ili tupate fursa zingine za kimaendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka nizungumze Mheshimiwa Naibu Waziri leo hii tunaishukuru sana Serikali yetu, kwa kweli mimi kwangu pale Mtwara haya mafuriko yaliyotokea hali ilikuwa ni mbaya sana. Nilivyoambiwa ninapewa milioni 500, kwanza nilisali na nikasema eeeh Mama nakushukuru sana na Serikali yako. Haijawahi kutokea katika nchi yetu kwamba, Serikali imeamua kutoa package moja kwenye mzunguko mmoja kwa Majimbo yote. Kwamba leo mnapata milioni 500 kila Jimbo, kwa ajili ya matengenezo ya barabara zetu. Hongera sana Mama Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunazungumzia zao letu la korosho la Mtwara, tulikuwa tuna Mfuko wa Export Levy. Mfuko ule ambao Serikali iliuchukua lakini mpaka leo hii kila tunapozungumza Wabunge wa Mtwara kuzungumzia juu ya fedha zetu za export levy bado hatujapata muafaka na hatujaambiwa nini kinaendelea. Rai yangu kwako Mfuko huu ndio ulikuwa unazalisha korosho kwa asilimia kubwa. Kwa sababu, ulikuwa una uwezo wa kuwenda kununua pembejeo, kwenda kuwasaidia wakulima na wakulima walikuwa hawana shida ya pembejeo kwa sababu tayari walikuwa wana mtaji wao, niiombe Serikali, nina imani Serikali yetu ni sikivu sana na inaweza kutusaidia, mfuko huu tunaomba urejeshwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine niishukuru Serikali, niishukuru Serikali kwa mpango ambao umeletwa wa NLG tunakwenda kujenga viwanda Lindi. Viwanda hivi ambavyo vinakwenda kujengwa Lindi, mimi niiombe tena Serikali gesi inatoka Mtwara na kama gesi inatoka Mtwara, basi kwenye Wizara ya Uwekezaji muda sasa umefika wa kuiangalia Mtwara kama Mtwara, iwe nayo ni zone ya kimaendeleo. Kwa sababu haiwezekani kwamba gesi iko Mtwara, lakini Mtwara hatuwajibiki kwenye masuala mazima ya gesi. Nilikuwa naomba, nimuombe Waziri wa Uwekezaji kwamba, hili ni jukumu lake na ana mamlaka makubwa sana ya kuweza kutusaidia wawekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)