Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Rhoda Edward Kunchela

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabla ya kuanza kuchangia napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai ambao amenipatia. Napenda niunge mkono hotuba ya Kambi ya Upinzani kwa asilimia mia moja. Kwa nini naunga mkono asilimia mia moja, kwa sababu hotuba ya Upinzani imeeleza uhalisia wa maisha ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma katika document zilizopita kila siku Wizara hii inapunguziwa bajeti. Abuja Declaration ambayo mlisaini mwaka 2001 lengo lake hasa ili kuwa ni ku-improve afya ya Watanzania. Ukisoma kwenye vitabu vyenu kuanzia TAMISEMI mpaka hii hotuba yenu ambayo mmei-present leo inaonyesha dhahiri kabisa kwamba hamjajipanga kwa sababu pesa mlizotenga ni ndogo.
Pia ukiangalia kwenye hii bajeti ya TAMISEMI inasema kwamba mlitenga shilingi bilioni 277 lakini kuna shilingi bilioni 518, jumla inakuwa ni shilingi bilioni 796. Sasa ukipiga kwa asilimia 100 ya shilingi trilioni 22 ambazo zimetengwa unapata ni asilimia 4.5. Shirika la Afya Duniani linasema kwamba mnatakiwa mfikishe asilimia 15. Sasa hii inaonyesha ni kiasi gani mme-fail kutekeleza hii Abuja Declaration, ingekuwa haina maana msingesaini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nataka nichangie kidogo kuhusiana na Wilaya ya Mpanda, Mkoa wa Katavi. Siwezi kuunga mkono hoja kwa sababu ni aibu kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuendelea kupunguza bajeti, lakini wananchi wetu wanaendelea kufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hospitali hii Mheshimiwa Waziri hakuna vitendea kazi lakini aibu nyingine inayoikumba Serikali ya Chama cha Mpinduzi ni kwamba hospitali nzima hakuna BP machine wala thermometer na oxygen machine ipo moja na inatumika kwa wodi sita, sasa hii ni aibu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie kuhusiana na masuala ya wazee. Wazee ni watu ambao wanateseka kwenye nchi hii lakini ukisoma kwenye hii hotuba ya Waziri haijaonyesha specifically mmetenga kiasi gani kwa ajili ya kutunza hawa wazee, mme-generalize tu yaani inaonekana kama hampo serious na hawa wazee. Naendelea kuwashangaa wazee kwa nini wanaendelea kukipa kura Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kwa sababu Halmashauri zetu zimeshindwa kukusanya mapato haya basi sasa zingeachiwa Manispaa kukusanya mapato. Inaonekana kabisa kwamba Wizara ya Afya mmeshindwa kuchukua jukumu lenu la kuwahudumia wazee ingawa mnasema kwamba Sera ya Wazee ni kuwahudumia bure kitu ambacho mnawadanganya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye Sera ya Afya. Ukisoma hotuba ya Waziri katika kata 3,990 kwa Tanzania nzima kata 484 ndizo ambazo zina vituo vya afya. Huu ni utani mnaoufanya kwa Watanzania wetu kwa sababu haiwezekani kuna difference ya kata 3,506 hazina vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye sera hii ya afya inasema vijiji kuwa na zahanati katika vijiji. Tuna vijiji zaidi ya 12,245, ukisoma kitabu cha Waziri wanasema tuna zahanati kwenye vijiji 4,502 tuna difference ya vijiji 8,043 hatuna zahanati na moja ikiwa ni Wilaya ya Mpanda pamoja na vijiji na kata zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia suala la afya ni kwamba tukidumisha afya za wananchi wataweza kufanya kazi, watajenga uchumi wao lakini siyo kuendelea kutupa porojo hizi ambazo mnatupa kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie suala la ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi imekuwa ni wimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisoma kitabu cha bajeti hapa mmesema kwamba mmetenga shilingi bilioni 1.8 lakini ni second time, mara ya kwanza Serikali ilitenga pesa wajanja wakapiga ile pesa wakaila.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni Serikali gani ambayo haipo serious zinatengwa pesa kwa ajili ya wananchi kujengewa hospitali yao lakini watu wachache wanachukua pesa wanakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sijui kama hizi pesa zipo theoretically au mnaingia sasa kwenye utekelezaji kwa ajili ya kuwajengea Hospitali ya Mkoa wananchi wa Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe masikitiko yangu na hii inawezekana tukaendelea kupiga kelele kumbe Serikali ya Chama cha Mapinduzi sasa imelemewa na mzigo. Ni Serikali gani ambayo kila kitu ninyi mna-set kwamba ni priorities kwenu? Afya, elimu, katiba, viwanda yaani kila kitu, lakini hatuoni utekelezaji. Mna documents nyingi sana mmeandika, ni theoretically! Sasa ingewezekana basi ingekuwa vizuri mka-set kitu kimoja baada ya kingine, kwamba tunaweka afya na mipango yetu ni moja, mbili, tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ajitahidi basi akatembelee hata Zimbabwe; kuna hospitali inaitwa Palalanyatu, ni hospitali iko Harare pale, ni kama Muhimbili. Huwezi kukuta hata takataka, huwezi kukuta inzi, lakini leo wanapoka magazeti, media, wanasema Muhimbili ina vitanda, huduma zimeboreshwa. Ni uongo na unafiki mtupu! Wakatembelee waangalie Zimbabwe wanafanya nini? Wakaangalie wenzao wanafanya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijamaliza, labda niseme, kutokana na upungufu wa vitendea kazi kwenye hospitali zetu hasa Mkoa wa Katavi, maana imefikia kipindi sasa hata wauguzi wetu ni wachache katika zahanati zetu katika hospitali. Nitoe masikitiko yangu kwamba wiki moja iliyopita nilipigiwa simu na ma-nurse kwamba vifaa baadhi ya hospitali vipo lakini wauguzi wetu hawana ule ujuzi wa kuweza kutumia vile vifaa. Sasa unashangaa vifaa vipo lakini mama mjamzito anapelekwa wodini ma-nurse wanashindwa kutumia vifaa vile. Wanakwambia tumtangulize mama wodini wakati tunamsubiri Daktari ili kuja kumtibu huyo mgonjwa. Sasa ni vitu ambavyo vinatia hasira. Kama mko serious... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)