Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii kuchangia hoja hii ambayo naiunga mkono kwa sababu inakwenda kujibu hoja zote ambazo zimetolewa katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, imetolewa hoja ya uboreshaji wa miundombinu ya kusafiri kwa njia ya maji ambayo; kama mlivyoshuhudia wengi tayari tumekwisha rekebisha katika Ziwa Victoria na juzi tarehe 15 Juni, 2021 Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan alizindua pale Mwanza meli ya MV Victoria na MV Butiama pamoja na Chelezo, na huo ulikuwa ndio mwanzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hoja iliyotolewa ya miundombinu ya maji tulishuhudia tarehe 15 mwezi wa sita Mheshimiwa Rais Wetu Samia Suluhu Hassani alishuhudia utiaji saini wa mikataba mitano ambayo ilikuwa inalenga katika kuboresha usafiri wa maji. Alishuhudia mkataba wa Meli kubwa katika Bahari ya Hindi ambayo ni tani 2,800 ambayo imelenga usafiri kati ya hapa na Comoro. Alishuhudia meli kubwa katika Ziwa Tanganyika ambayo vile vile ina meli yenye uzito wa tani 2,800, alishuhudia utiaji wa saini wa meli kubwa ya abilia 600 katika Ziwa Tanganyika pamoja na uzito wa shehena tani 400. Vile vile alishuhudia utiaji wa saini wa meli mpya ya tani 3,000 katika Ziwa Victoria pamoja na ukarabati wa MV Umoja. Kwa hiyo bajeti hii ambao inakwenda kujibu maswali hayo naiunga mkono kwa sababu hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda kwenye Bandari, upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara unaendelea na bajeti hii inakwenda kukamilisha; kwa hiyo unakwenda kutatua matatizo hayo. Katika Bandari ya Dar es Salaam lile gati la RoRo limekamika na magati namba moja hadi saba yamekamilika na sasa hivi tunamalizia pale ile yard ya kuelekea makasha. Hivyo bajeti hii itaimarisha kuimarisha lango hilo vizuri sana. vile vile lango la kuingilia katika Bandari ya Dar es Salaam linakwenda kupanuliwa, na sasa hivi pale tutaingiza meli kubwa kabisa ambazo zinaweza kubeba hadi makasha 7,000 hadi 8,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bajeti hii tutaagiza mitambo mikubwa ya kupakulia na kupakilia mizigo maalufu kama SSG Shore to Sea Gantry ambazo zimeagizwa kwa kutumia na bajeti hii. Katika Bandari ya Tanga vile vile lango la kuingilia pale limechimbwa, ambalo litakamilishwa kwa kuongeza gati mbili kubwa za mita 250, 250 ili tuweze kupokea meli kubwa za mita 300. Vile vile Mtwara tunafanya vivo hivyo tunaongeza magati mawili ambayo tayari yanakamilika na sasa hivi tunaagiza vifaa vya kupakilia mizigo, hivyo bajeti hii inakwenda kutatua hayo matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa reli vile vile tulimshuhudia Rais wetu mpendwa tarehe 14 mwezi wa sita akiweka jiwe la msingi katika Reli ya Standard Gauge kutoka Mwanza hadi Isaka. Kwa hiyo inadhihirisha kwamba bajeti hii ambayo itakwenda kukamilisha kipande hicho inatekeleza mwendelezo wa kazi hizo ambazo tumeziendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika uchangiaji vile vile iliongelewa hoja ya TARURA, kwamba tuaingalie; na ni kweli katika marejeo ambayo tumeyafanya ya uwiano wa mgawanyo wa fedha za mfuko wa barabara ambao tumebaini kwamba ulifanyika mwezi Disemba, 2020 tumebaini kwamba tatizo kubwa siyo mgao wa fedha bali ni kiasi kidogo cha fedha za mfuko. Tayari mmeona katika bajeti hii hatua zimeanza kuchukuliwa katika kuongeza bajeti hii, ni muhimu tuiunge mkono kwani inakwenda kutatua hayo matatizo yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, imeongelewa miundombinu ya Jangwani pale katika mchango wa bajeti hii. tayari TANROADS inafanya pale usanifu wa kina ili tuweze kupata utatuzi wa changamoto hiyo na ambayo katika ukamilifu wake tutaweza kupata utatuzi, kwamba tufanye nini pale ili mafuriko ya pale Jangwani na ile miundombinu ya Mwendokasi iweze kulindwa na tuweze kuendelea na kutoa huduma pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile katika michango iligusiwa sheria yetu ya barabara ya Namba 13 ya mwaka 2007 ambayo ilikuwa inaongelea kuzuia malori yanayozidi tani 10 kuelekea katika vijiji vyetu ambavyo ililenga kwamba tuiachie. Sheria hiyo imezingatia uwezo wa barabara zetu za kule na kuzilinda hivyo lengo lake ni kulinda miundombinu ya zile barabara hasa madaraja yake. Hivyo, sheria hiyo tutaendelea kuizingatia ili kulinda miundombinu hiyo. Lakini tuendelee kuongeza ulipaji kodi ili tuweze kupata fedha zaidi za kutosha kuweza kuimarisha miundombinu hiyo ili iweze kuwa bora zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile ilitolewa rai hapa kwamba kuna ahadi nyingi katika miundombinu ya barabara ya viongozi wa Taifa. Hapa tunarudia kusema tena kwamba hizi ahadi za kitaifa tunazipangia mkakati wa kuzitekeleza. Imetolewa hoja kwamba tuziwekee database na hilo ambalo tumelifanya. Kwamba ahadi zote za kitaifa zilizotolewa katika ujenzi wa barabara, vivuko nakadhalika tutazizingatia kulingana na vipaumbele vyake katika bajeti zitakazokuwa zinaendelea hapa Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile ilitolewa rai ya kupunguza msongamano wa magari katika babara inayokwenda Tunduma hasa pale Mjini Mbeya katika barabara ya Igawa hadi Tunduma. Hilo nalo tunaenda nalo, na kwa sasa hivi tunamalizia ule upembuzi yakinifu wa ile by-pass ili itakavyokamilika katika bajeti hii tuanze na utekelezaji wa ujenzi wa barabara ile ambayo inaondoa changamoto hiyo ambayo tunayo pale. Hivyo ni bajeti hii hii ndiyo itakayotatua changamoto hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna michango ya bajeti hii ambayo ilihusiana na viwanja vya ndege. Kwa mfano ilitolewa rai kuhusu kiwanja cha ndege cha Sumbawanga na vinginevyo. Tayari vile viwanja ambavyo vilikuwa vijengwe kwa ufadhili wa European Investment Bank, maongezi yameshakamiliaka na sasa hivi tunasubiri wakati wowote waweze kutoa fedha ili vile viwanja vinne viweze kujengwa katika bajeti hii. Kwa hiyo tuna kila haja ya kuiunga mkono bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kisera, bado nia ya Serikali kuunganisha mikoa yote kwa viwanja vya ndege ipo pale pale hivyo tutaendelea kuviboresha viwanja vyote vya mikoa na kuvijenga ili viweze kuendelea; na kwa sasa hivi viwanja vyote tunaviboresha katika kiwango cha kuviwekea taa ili viweze kufanya safari za usiku na tuweze kuongeza safari katika miundombinu ya viwanja hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo barabara nyingi ambazo Waheshimiwa Wabunge wameziongelea hapa na zote hizo ambazo tumezipanga katika bajeti hii tunaomba kupewe hiyo fursa ili tuweze kuzitekeleza katika bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda katika miundombinu ya reli, nikirudia pale, tuna reli ambazo tumepanga kuzifanyia upembuzi yakinifu ambazo ni Reli ya Tabora hadi Kigoma ambayo vile vile inakwenda kufanyiwa katika bajeti hii. Reli ya Kaliua - Mpanda hadi Karema nazo tutakamilisha kuzifanyia upembuzi yakinifu. Hivyo tukimaliza huo upembuzi yakinifu kazi ambayo itafuata katika reli hizo ni ujenzi, na kazi zote hizo zimepangwa zitekelezwe katika bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Apika, huo ndio mchango wangu, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)