Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge

Hon. Ramadhan Suleiman Ramadhan

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chake Chake

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge

MHE. RAMADHANI SULEIMAN RAMADHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kunipa nafasi hii ya kuchangia kwenye hoja iliyoletwa mezani ya ripoti ya Sheria Ndogo kuhusiana na uchambuzi na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Mheshimiwa Spika, na mimi kutoka mwanzo wa mchango wangu naomba nieleze kwamba ni mmoja kati ya member ambao wanahudumu katika hii Kamati ya Kudumu ya Bunge Sheria Ndogo, kwa hiyo namimi naomba nichukue fursa hii kukupongeza kwa imani yako kwangu kwa kuniamini na kunichagua na kuhudumia kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Spika, mimi mchango wangu nataka niulekeze kwenye uhalisia ulipo ambao unawekwa katika sheria ndogo mbalimbali zinazoletwa kwetu. Kwa mujibu wa Ibara ya 64(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, mamlaka ya kutunga sheria yamewekwa kwa Bunge, lakini Katiba hiyo hiyo kwenye kifungu 97(5) ikatoa pia mamlaka kwa Bunge kukasimu madaraka yake kutunga sheria kwa vyombo vingine.

Mheshimiwa Spika, kutokana na wingi wa shughuli za Bunge, Bunge likapewa mamlaka kwamba linaweza kukasimu madaraka yake ya kutunga sheria kwa mamlaka nyingine au vyombo vingine ili viweze kulisaidia kwenye kutunga sheria zinazogusa maisha ya watu kila siku huko. Kwa sababu tunajua mchakato wa Kibunge wa kutunga sheria unakuwa ni mkubwa baadhi ya wakati na mahitaji ya sheria kwenye jamii zetu yakiwa makubwa nayo kwa hiyo mamlaka ya Bunge zikapelekwa ziruhusu mamlaka zingine zitunge sheria ili sheria hizo zisaidie kwenye maisha ya watu.

Mheshimiwa Spika, sheria zilizoletwa mbele ya Kamati na tukazichambua, tumebaini kama Kamati kuna sheria 11 zilikosa uhalisia kutokana na vifungu vilivyomo kwenye sheria pamoja na maisha ya Watanzania, kwenye kiingereza tunaita reasonability, vifungu vya sheria havina reasonability ya maisha ya Watanzania na inavyoonekana kuna baadhi ya maeneo ikitokea mtu anafaida ya jambo au interest kwenye kitu fulani kimbilio lake anakimbilia kwenye mamlaka za kutunga sheria ndogo kwenda kuweka sanctions ya hayo anayotaka, anaona kwamba huko ni rahisi zaidi kuliko kuja Bungeni. Kwa hiyo wanatumia mwanya wa mamlaka za kutunga sheria ndogo kwenda kuweka vitu wanavyotikana wao. Kwa mfano, kuna sheria ndogo ililetwa mbele yetu na tukaijadili Sheria Ndogo ya Ada na Ushuru Halmashauri ya Njombe, sheria imeweka tozo na ada ya ushuru ya shilingi 1,000 kwa pikipiki inayoingia stand pamoja na shilingi 1000 kwa gari zinazoingia stand.

Mheshimiwa Spika, huku ni kuvunja moyo au ku- discourage watu wanaojishughulisha na shughuli za pikipiki hao bodaboda; yeye unamwekea shilingi 1,000 mwenye daladala inayopakia watu 40 unamwekea shilingi 1,000 ni kumuonea. Kwa hiyo hayo ndiyo mambo sisi tuliyaona kama Kamati natukayajadili na tukaishauri Serikali na mamlaka zilizotunga hizo sheria kwenda kurekebisha.

Mheshimiwa Spika, kuna Sheria Ndogo ya Ada ya Ushuru wa Halmashauri ya Kiteto imesemwa hapa kwenye taarifa na msoma taarifa, imeweka ada shilingi 20,000 kwa shughuli za jando na unyago, siyo sahihi hata kidogo. Tumezifanya shughuli za jando na unyago kuwa kama chanzo cha mapato, wakati zilivyowekwa uhalisia wake ni kuwa sehemu ya kufundisha vijana wetu nani shughuli za kijamii zinazokwenda kuwapa madarasa vijana wetu jinsi ya kuja kuishi kwenye jamii pana zaidi.

Kwa hiyo unavyoiweka kwamba lazima shughuli hiyo itoe shilingi 20,000 ni kuwaonea wananchi wasiokuwa na kipato wa kwenye jamii nyingi hasa za vijijini, kwa hiyo hayo ni miongoni mwa vitu ambavyo tumeviona wakati tunajadili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna Kanuni ya Filamu na Michezo ya Kuigiza; mchangiaji wa kwanza Advocate Mheshimiwa Swalle alisema hapa, Sheria Ndogo ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Mjini wao wameweka kumiliki na kuendesha shughuli za kuonesha filamu kwenye mabanda ya filamu yale mabanda yetu yale tunaita mabanda umiza kibali kinaanzia shilingi 300,000 mpaka shilingi 1,000,000; huku ni kuwaonea wajariliamali wadogo waliojiwekeza kwenye hayo mabanda umiza, watu wenyewe ni maskini mtu ana mtaji wake mdogo, kaweka banda lake kwa ajili ya kuonyesha mpira na filamu wewe unamtaka akatoe shilingi 300,000 mpaka shilingi 1,000,000 hiyo shilingi 300,000 mpaka shilingi 1,000,000 anaitoa wapi.

SPIKA: Mheshimiwa Ramadhani Suleiman Ramadhani nakushukuru kwa mchango wako.

MHE. RAMADHANI SULEIMAN RAMADHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)