Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, awali ya yote nianze kwa kukushukuru kwa kunichagua nikawa Mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo ambapo mwanzoni nilipoona jina langu lipo kule nilikuwa nina wasiwasi, lakini nilipofika kule kwenye Sheria Ndogo nikagundua kwamba kule ndiko ambako sheria zinazoongoza nchi kwenye grassroot/ kwenye Halmashauri zipo pale na mambo mengi yanayogusa wananchi yapo kule kwenye Sheria Ndogo, kwa unyenyekevu mkubwa sana nakushukuru sana kwa kunichagua nikawa Mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Spika, naomba mchango wangu niulekeze kwenye Kanuni za Sheria za Filamu na Michezo ya Kuigiza, naanziaa hapo. Taasisi ambazo zimekasimishwa madaraka ya kutunga sheria ndogo ndogo tunatarajia zifanye kazi hii kwa weledi mkubwa, lakini zifanye kazi hii katika namna ambayo hizi sheria ndogo zinazotungwa haziji kuharibu mambo na badala yake zinakuja kujenga.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kanuni hii ya Sheria za Filamu na Michezo ya Kuigiza imeweka masharti kwa taasisi ya Serikali ikiwemo Bunge, kuomba kibali cha kutaka kutengeneza filamu pale ambapo taasisi hiyo inahitaji kutengeneza filamu. Taasisi kama TANAPA, Taasisi za Elimu zinahitaji kutengeneza filamu kwa ajili ya shughuli mbalimbali kwa mfano Taasisi za Elimu zinahitaji kutengeneza filamu kwa ajili ya kufundishia; taasisi kama TANAPA wanahitaji kutengeneza filamu kwa ajili ya kuvutia watalii ili tuweze kuongeza vivutio vyetu NA tuweze kuvitangaza kupitia filamu.

Mheshimiwa Spika, lakini kanuni hii inataka taasisi za Serikali kuomba vibali kabla ya kutengeneza filamu, mbaya zaidi kanuni iliyotengenezwa inakinzana na sheria mama yenyewe ambayo sheria mama iliondoa hitaji hilo la kuomba vibali kwa taasisi za Serikali zinapotaka kutengeneza filamu. Niombe kanuni hii iweze kuondolewa/sharti hili liweze kuondolewa kwenye hii Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza.

Mheshimiwa Spika, kanuni ya 16 ya sheria hii imeorodhesha vitu ambavyo ni maudhui yanayokatazwa na sheria hii, matarajio yetu sisi nikiwemo na mimi mwenyewe ni kwamba muigizaji anapotaka kuigiza kwa mfano muigizaji anataka kuelezea madhara ya dawa za kulevya ni matarajio yangu kwamba tunamuona mtu yule anaishi maisha yake halisi kwenye jamii, baadaye tutamuona anaanza kutumia dawa za kulevya na baada ya hapo tutaona madhara ya dawa za kulevya; lakini sheria hii maudhui yaliyooneshwa inakataza yule mhusika wa filamu kuigiza kile kipengele cha kutumia dawa za kulevya.

Mheshimiwa Spika, sasa kama inakataza kile kipengele muhimu katika uigizaji maana yake ni kwamba inauwa kabisa tasnia ya uigizaji na filamu nchini. Sio hapo tu imeenda hadi kwenye mavazi, hadi kwenye umalaya na kadhalika sisi tunatarajia mtu akiwa malaya tumuone anavyokuwa malaya, baadaye tumuone anavyopata magonjwa ikiwepo hayo ya zinaa, tuone madhara yake ili watu watakaokuwa wanatazama ile filamu yale maudhui waone lile jambo ni baya na baada ya hapo waweze kuliacha kwenye jamii, lakini kwenye kanuni ya 16 imekataza mambo yote hayo naomba kwa kweli hii kanuni na yenyewe ifanyiwe marekebisho.

Mheshimiwa Spika, lakini kanuni hii ya sheria za filamu na michezo ya kuigiza imeweka maombi ya vibali bila ya kutumia njia za kisasa za mtandao; fikiria muigizaji yuko Jimbo la Ngara aje kuomba kibali cha kutaka kutengeneza filamu yake hapa Dodoma ama Dar es Salaam; fikiria mtu ambaye yuko Sumbawanga kwa kweli jambo hili na lenyewe halipendezi kwa sababu katika karne hii ya kutumia mtandao tunatarajia kwamba maombi haya yarahisishwe na yafanyike kwa njia kielektroniki.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli tunaomba eneo hilo na lenyewe liweze kuboreshwa lakini niende kwenye kanuni ya Bodi ya Kitaaluma ya Walimu yaani Tanzania Teachers Professional Board. Kama alivyosema Mwenyekiti wetu wa Kamati wakati anawasilisha, ni kweli kwamba wakati tunachambua sheria hizi walikuja wadau mbalimbali wakiwa wanalalamika kwamba hawakushirikishwa wakati wa kutengeneza kanuni hizi.

Mheshimiwa Spika, ili sheria iende kwa walaji na waweze kuikubali ni muhimu sana sheria hiyo iweze kuwashirikisha hivyo sheria hii ni kama vile inakosa uhalali kwa sababu walaji walilalamika kwamba hawajashirikishwa. Lakini ukifuatilia kwa mfano kanuni ya 8(6)cha Kanuni ya Bodi ya Kitaalama ya Walimu, imemtaja Mwenyekiti miongoni mwa watu wanaotakiwa kuweka sahihi kwenye kile cheti kinachomruhusu mwalimu aweze kufanya kazi ya ualimu.

Mheshimiwa Spika, huyu Mwenyekiti hajasemwa ni Mwenyekiti wa Kijiji, Kata, wa kitu gani kwa hiyo ukiangalia kwa ujumla sheria hii ina mapungufu makubwa ambayo yanahitaji kuboreshwa. Kanuni ya 8(2) ya sheria hii imetaja cheti kinachoitwa Ordinary Certificate of Secondary Education wakati cheti kama hiki ndani ya nchi hii hakipo cheti kilichopo ni Certificate of Secondary Education, sasa tunajiuliza hawa watu tuliowakasimisha madaraka ya kutunga sheria hawaangalii vitu vilivyopo?

Mheshimiwa Spika, hivyo hii kanuni ya walimu hii imelalamikiwa sana tunaomba ifanyiwe marekebisho, vitu vilivyokatazwa tunaona vinarudi.

Mheshimiwa Spika, naomba dakika mbili kuna mtu hakuwepo…

SPIKA: Haya malizia.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, kuna kurejea kwa tozo za kero hapo nyuma Serikali iliyokuwepo ilikuwa imeshaanza kufuta tozo zote ambazo ni za kero, hebu fikiria Watanzania wanapokuwa wametoka kwenye kazi ngumu, wananchi wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanatakiwa waende wakapumzike, wengine wanakwenda kwenye kumbi za starehe wengine wanakwenda kwenye kumbi za sinema.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna hii kanuni za ada na tozo mbalimbali za Halmashauri zimeanza kuweka tozo kubwa kwenye maeneo haya ya starehe. Sisi tunapokuwa majumbani kwetu tunaangalia tv zilizoko majumbani kwetu lakini tukumbuke kuna watanzania wengi hawana tv eneo lao la kwenda kujidai mida ya jioni ni kwenye hizi kumbi za starehe pamoja na sinema. Ninaomba hili jambo liangaliwe ili tuache Watanzania wafurahie maisha hasa wanapokuwa wametoka kwenye kazi ngumu.

Mheshimiwa Spika, kuna tozo hizi zimesemwa bajaji shilingi 1,500 basi la abiria ambao lina siti 20 shilingi 1,500 hii ni Jiji la Mbeya wanataka kutoza vitu vya namna hii, wakati mwingine bajaji anaongea na mteja shilingi 1,000/buku tu anampeleka mteja kutoka eneo moja kwenda eneo lingine. Hivyo vitu hivi visipoangaliwa vitaanza tena kurudisha zile kero ambazo kwa kweli tulishatoka huko na sasa hivi wananchi wanaishi maisha mazuri, hivyo hizi sheria ndogo ndogo zote ambazo zinaleta kero tusiweze kuzipitisha.

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa unyenyekevu mkubwa kwanza kwa kuniongezea dakika Mwenyezi Mungu akubariki ninaunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)