Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, kwa kunipatia fursa hii na mimi nitumie fursa hii kumpongeza sana Mwenyekiti wa Kamati na Makamu wake na timu yao nzima kwa kazi kubwa nzuri wanayoifanya kwa kweli sheria ndogo hizi ndiyo uhai wa utekelezaji wa sheria katika maeneo yetu Tanzania nzima. Na Katiba imetoa ruhusa sisi Wabunge kukasimisha madaraka hayo katika maeneo hayo ambayo yanahusika kwa ajili ya kutunga hizo sheria ndogo, lakini pia tumepewa jukumu la kudhibiti sheria hizi sasa na hili sio jambo la tofauti, ni jambo la utaratibu wa kawaida katika Mabunge yote ya Jumuiya za Madola. Kwa hiyo tupo sawa sawa na tunakwenda vizuri na Sheria ya Tafsiri za Sheria kifungu 38 kimeeleza wazi kama ambavyo amesema Makamu Mwenyekiti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na mimi nikubaliane na wewe kwamba kutungwa kwa hizi sheria ndogo kunategemeana pia na utungaji wa sheria wa sisi hapa Bungeni kupitia Kamati yetu ya Katiba na Sheria. Kwa hiyo ningefurahi kama tungeweza kuwa na ushirikiano wa karibu sasa baina ya Kamati ya Katiba na Sheria na wenzetu wa Sheria Ndogo ili tukaweza kuona kwamba zile sheria ambazo zinatoa mianya kwenye kutengenezwa sheria ambazo zinakosa masharti na vigezo basi angalau tupunguze hilo suala.
Mheshimiwa Spika, changamoto ni nyingi sana ameeleza katika Kamati ya Sheria Ndogo ikiwemo na kukinzana kwa Sheria Ndogo na Sheria mama kama ambavyo nimeeleza, lakini sheria hizi kukosa uhalisia na utekelezaji wake kuwa mgumu katika maeneo yetu, lakini pia tumeambiwa hapa mawasiliano hafifu kutoka kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu pamoja na mamlaka husika au baadhi ya mamlaka husika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nafikiri Mwanasheria Mkuu akijipanga vizuri na timu yake basi marekebisho mengi hayatofika kwenye Kamati ya Sheria Ndogo, kwa hiyo hilo nafikiri mwenyewe yupo na amelipokea. Lakini suala la kutoshirikishwa wadau ni suala ambalo ni changamoto kwa sababu hata sisi hapa katika utunzi wa sheria tunaona kwenye Kamati ya Katiba na Sheria tunawaalika wadau wengi, tukipata maoni ya wadau wengi ndio sheria inakwenda kuwa afadhali nzuri kwa sababu wanatoa maoni ndio wale wanaoenda kuzitumia hizo sheria zetu huko kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini suala lingine la tozo kwenye tasnia ya filamu, lakini kwenye hiyo jando imetajwa basi hayo mambo ni ya kuzingatia ya kuangalia siyo lazima mpaka yafike kwenye Kamati yetu ya Sheria Ndogo, nafikiri wenyewe huko wanaweza kurekebisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kuna suala muhimu sana ambalo nitalizungumza hapa leo ni kuhusu suala la michezo ya kuigiza hii; kama tuna kumbukumbu nzuri Bunge la Kumi na Moja tulipitisha sheria katika kurekebisha kuipa Bodi ya Filamu mamlaka ya kudhibiti mporomoko wa maadili tunavyofanya maigizo yetu hapa kwenye filamu zetu Tanzania, sisemi kwamba napingana na kamati moja kwa moja, lakini ninachotaka kusema ni kwamba ikiwa ulevi, ikiwa ukahaba, ikiwa mavazi mabovu yatalenga kuielimisha jamii basi mchezo huo hauna tatizo, lakini ikiwa ulevi, ukahaba pamoja na mambo mengine yanayofanywa kwenye filamu yanaelekeza kuiharibu zaidi jamii hilo sasa ni tatizo na ndiyo maana Bodi ya Filamu ikapewa mamlaka ya kudhibiti filamu zote ambazo zinaoneshwa kwenye nchi yetu, hili ni jambo la msingi sana. Kwa sababu kila pahala kama ambavyo wenzangu wamesema kwamba tukisema wavae hijabu wote michezo itakufa au haitoonekana vizuri, siyo lazima kuvaa hijabu au kuvaa kama mimi ndiyo unazidi kupendeza, hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ila sema tunavyokwenda kwenye mabasi tunafuatana na familia zetu na watoto wetu, michezo inayoonyeshwa kwa kweli hasa kwa sisi wanawake yaani siyo kama ndiyo amevaa, haijavaliwa nguo yaani mwili wote upo wazi nguo ipo juu ya paja ni hatari kwa kweli. Kwa hiyo tunawafundisha Watoto wetu mambo ambayo siyo ya maana na siyo maadili ya nchi yetu. Kwa hiyo, hilo mimi napenda nigongee sana hapo na ninaomba kamati inielewe hivyo kwamba hii Bodi ya Filamu imepewa Mamlaka kwa mujibu wa sheria tuliyotengeneza wenyewe katika Bunge la Kumi na Moja kwa hiyo tuendelee, tuwaachie wafanye kazi yao, lakini watoe elimu kwa namna ambayo itaielimisha jamii na siyo kuipotosha jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini mwisho kabisa pamoja na kuomba ushirikiano mzuri baina ya kamati yangu na Kamati ya Sheria Ndogo kifungu cha 38(2) cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria kinatoa ruhusa Bunge kupitisha azimio la kukataa Sheria Ndogo ambayo inakiuka masharti ya sheria mama. Kwa hiyo, naomba sana kamati yetu ya sheria ndogo ilizingatie hilo, tunapoona kwamba sheria ndogo inakinzana na sheria mama na inaleta mtafaruku huu katika utekelezaji basi kama kuna uwezekano izuiliwe kupitia Azimio la Bunge kwa mujibu wa sheria ya kifungu 38(1). (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ahsante sana kwa kunipa fursa. (Makofi)