Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii, nami ningependa kuchangia kidogo katika eneo hili la sheria ndogo. Kwa uwelewa wangu sheria ndogo zinapaswa zifuate utunzi wa sheria na kuhakikisha kwamba hazikinzani na yale ambayo yameelekezwa kwenye Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, na kati ya vitu ambavyo Katiba yetu inatambua ni pamoja na suala nzima la freedom of association na huu ndiyo msingi wa sekta ya Asasi za Kiraia kwa maana ya CSOs, NGOs na kadhalika ambao wanakuja pamoja kwa lengo la kuchangia maendeleo katika jamii.

Mheshimiwa Spika, sasa katika upande huu wa sheria ndogo ziko sheria ndogo ambazo zinatungwa na Halmashauri, lakini pia zipo kanuni ambazo zinatungwa na Mawaziri wenye dhamana ya maeneo husika. Hapa ningependa kurejea kwenye Sheria ya NGOs. Katika sheria hii ilitoa mwanya wa Waziri mwenye dhamana kuandaa kanuni kutunga kanuni na kati ya kanuni ambazo zimetungwa chini ya sheria hii ya NGOs ipo kanuni ambayo inataka NGOs kwa maana ya sekta Nzima ya Asasi za Kiraia pale ambapo zinapata ufadhili wa mradi wowote hata kwa kiwango cha milioni 20 uwasilishe lile andiko lake, uwasilishe pia na mkataba na nini ambacho unataka kwenda kufanya, uwasilishe kwenye ofisi mbili tofauti yaani unatakiwa uwasilishe kwenye Ofisi ya Msajili wa NGOs lakini pia Hazina na baada ya kuwasilisha hivyo vitu vyote huyu NGOs hawezi kutekeleza ule mradi mpaka apate kibali kutoka kwa msajili wa NGOs na Hazina, jambo ambalo kwa kawaida linaongeza mlolongo mrefu. (Makofi)

Kwa hiyo unakuta labda NGOs imegundua kuna changamoto fulani kwenye jamii, imetafuta ufadhili imepata ufadhili labda milioni 20/30 lakini hawezi kutekeleza mpaka apewe kibali na unakuta ufadhili ule kapewa labda mradi unatakiwa utekelezwe ndani ya miezi sita mpaka mwaka, mlolongo mzima huu wa mpaka kupata kibali unachukua miezi sita, kwa hiyo mpaka unakuja kupata kibali ile fedha inabidi umrudishie mfadhili au inakuwa ni muda mfupi sana umebaki kiasi kwamba huwezi kutekeleza ule mradi jinsi ambavyo umetakikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa jambo hili linafifisha ile financial freedom ya hii sekta ya Asasi za Kiraia, lakini mbaya zaidi unapelekea pia kuwapa changamoto wadau wa maendeleo kwa maana ya wafadhili wanakuwa na hofu kuona je, mradi utatekelezeka ndani ya muda ambao umepangwa?

Mheshimiwa Spika, mimi napenda kukiri kanuni hii iliwekwa kwa nia njema kabisa ya kuhakikisha kwamba tunaimarisha uwazi na uwajibikaji kwenye Sekta ya Asasi za Kiraia, lakini hapo hapo tutambue ya kwamba hizi NGOs zote zinakuwa zimesajiliwa kwa hiyo Serikali kupitia Msajili wa NGOs imepitia katiba zake, imepitia malengo ikawapa usajili, kila mwisho wa mwaka wanatakiwa wawasilishe ripoti yao ya mwaka ya kazi/audited accounts.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi napenda kupendekeza hii kanuni Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana aiangalie upya ili pia basi hizi NGOs, sekta ya AZAKI kwa maana ya NGOs, CSOs, wanatakiwa watakapokuwa wanawakilisha taarifa zao za mwaka (audited accounts) pia wawasilishe mikataba ya zile fedha walizopata na namna walivyozitumia. Kwa sababu kinyume na hapo tunaenda kinyume na lengo zima ambalo kwanza limewekwa kwenye Katiba, lakini hata lengo la ile sheria mama ya NGOs ambayo inataka kuhakikisha ya kwamba Sekta hii ya AZAKI inachangia katika maendeleo ya jamii na sekta hii inafanya kazi kubwa sana kwa kushirikiana na Serikali na hata juhudi zake zimetambuliwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa hiyo kwa kumalizia napenda kuiomba sana Serikali kupita wizara husika izipitie upya kanuni hizi, lakiniā€¦

MHE: SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ninaomba nimpe taarifa anayezungumza kwa sababu mimi pamoja na wengine najua wamo hapa tumefanya kwenye NGOs kwa muda mrefu. Ni lazima upeleke taarifa kwenye Wizara husika na audited account huwa wanafanya hivyo kwa watu wa NGOs sijajua labda anazungumzia eneo lipi?

SPIKA: Nakuongezea dakika Mheshimiwa fafanua.

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, ahsante nashukuru kama alinisikiliza vizuri kwenye mchango wangu nilisema kwamba kila mwaka NGOs zinawasilisha taarifa zao za mwaka za hesabu, lakini pia zinawasilisha audited accounts, lakini kwenye kanuni imesema kwamba NGOs itakapopata mradi wa kuanzia shilingi milioni 20 isitekeleze mradi huo mpaka ipate kibali kutoka kwa Msajili wa NGOs na Hazina. (Makofi)

Kwa hiyo, mimi ninachoongelea hapa kwa sababu tunaongelea sheria ndogo na mojawapo ya sheria ndogo zipo za upande wa halmashauri, lakini pia zipo zile ambazo zinatungwa na Mawaziri wenye dhamana kupitia kanuni, kwa hiyo, hicho ndiyo nilichokuwa nakiongelea na ningependa na yeye ajielimishe zaidi katika eneo hili ili kwa pamoja tuweze kuishauri Serikali vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kurejea tena naiomba sana Wizara yenye dhamana ya masuala ya maendeleo ya jamii ipitie upya kanuni hizi ili iweze kuimarisha financial freedom ya sekta hii ya AZAKI maana hivi sasa inakinzana na inafifisha juhudi za sekta za AZAKI kuchangia katika maendeleo ya jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia napenda kumshukuru sana Waziri mwenye dhamana ya masuala ya maendeleo ya jamii kwa sababu mchango wangu kwenye bajeti ya Wizara hii niliiomba sana itusaidie ili ufanyike uchaguzi wa Baraza la NGOs la Taifa (NACONGO) ambalo liko ngazi ya Wilaya, Mikoa mpaka Taifa na hivi sasa uchaguzi huo unaendelea, kwa hiyo, napenda kumshukuru sana kwa kutusaidia katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, majuzi kwenye kikao chake na Baraza la Maaskofi wa Kikatoliki Tanzania alikumbushia kwamba yeye ni mwanaharakati na ni mwana-AZAKI pale ambako walipokuwa wanamtambulisha Askofu Kilaini. Kwa hiyo, na kwa kutumia hiyo hiyo napenda kuendelea kumwakikishia kwamba sekta ya Asasi za Kiraia tunamtambua kama mwana-AZAKI mwezetu na tunaahidi kuendelea kumpa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza azma yake ya maendeleo ya jamii kwa Taifa letu na hakika tutafika pale ambapo anataka tufike kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana kwa fursa hii na nakubaliana na maoni ya kamati husika, ahsante. (Makofi)