Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwanga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kupata nafasi hii ya mwisho ya kufunga jamvi la uchangiaji. Awali ya yote niishukuru na kuipongeza sana Serikali kwa jinsi ambavyo imeendelea kuziongezea nguvu Mamlaka za Serikali za Mitaa na bajeti hii inashuhudia hayo, kwa hiyo, kwa hilo nipende kuwapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na kuongezea nguvu Serikali za Mitaa ni pamoja na suala hili la by-laws ambazo tunazizungumzia leo, kwa hiyo niwapongeze sana Kamati husika, wasilisho lao limekuwa zuri na ambalo nadhani pia limerahisisha uchangiaji wetu kwa siku hii ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni wazi kabisa kwamba taarifa ya Kamati imeonyesha umuhimu mkubwa sana wa kuziongezea uwezo mamlaka zinazohusika na utungaji wa hizi wa hizi by- laws na kwa sababu Mwanasheria Mkuu wa Serikali yupo hapa na amesikia na hili niseme kwa nidhamu kwa sababu kwa taratibu zetu huyu ndiye wakili namba moja au msomi namba katika nchi, kwa hiyo, sisi wote tukimkuta huwa tunampisha kiti kwanza, naamini kwa vile yupo hapa na amesikia basi hiyo kazi itafanyika. Sheria ndogo ni muhimu siyo kwa uchumi wa nchi tu, lakini hata katika kulinda utulivu wa nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatizo la sheria ndogo lipo kwenye kukinzana na sheria mama, lakini pia kupatikana kwa ule murua na sheria zingine zinazohusika, ile harmonization. Nitoe mfano, kwenye Jimbo langu la Mwanga sisi tunategemea sana mapato kwenye chanzo kimoja kinachoitwa madini ya ujenzi hasa mchanga. Ilitungwa ile Sheria Ndogo ya Ada na Ushuru ya Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga ya mwaka 2019 ambayo ilizipa halmashauri mamlaka ya kukusanya mauzo pamoja na ushuru kwenye hivi vyanzo vya madini haya ya ujenzi na hilo linaendelea kufanyika. Sasa hilo limefanyika bila kuangalia upande mwingine wa sheria ya madini ambapo Kamishna wa Madini anayo mamlaka ya kutoa hizi primary mining licenses kwa watu binafsi hata kwa mamlaka hata kwa vijiji.
Kwa hiyo, utakuta kweli Halmashauri ina mamlaka hayo chini ya by-law, lakini wapo watu ambao wanazo primary mining licenses kwenye maeneo yao. Kwa hiyo, hapo sasa kunakuwa na mgongano kwamba mimi nina leseni mbona wewe unakuja kukusanya hapa. Kwa hiyo, hilo linahitaji sana kutazamwa tusitazame tu zile sheria mama, lakini pia tutazame pia hizi sheria zingine ambazo zinahusika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, limesemwa vizuri hapa suala la rumbesa, kwa tatizo la rumbesa linatoka wapi! Tatizo la rumbesa linatokana na Sheria ya Vipimo (Weights and Measures), rafiki yangu, Mheshimiwa Shangazi atakubali kule kwake wanalima viazi sana, by-laws inasema rumbesa hapana, lakini ile Sheria ya Vipimo yenyewe inazungumzia juu ya uzito kwamba kilo 100 bila kujali imejaa mpaka wapi as long as ni kilo 100 imetimiza sheria. Sasa swali linakuja kwamba hivi gunia ni kipimo au ni kifungashio? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hawa wengine sasa huko kwenye barriers sasa/kwenye vizuizi vya barabarani, ndio wanachukua sasa faida hapo wakifika hapo wanaweza kukubabaisha. Kwa sababu upande mmoja anaweza akasimama na by-laws, upande mwingine akasimama na Sheria ya Vipimo. Sasa wewe hapo katikati ndio unakuwa uko katikati ya nyundo na msumari unaendelea kuumia.
Mheshimiwa Spika, nikirudi nyuma kidogo ni kwamba hizi by-laws zinapotoa mamlaka fulani, lazima pia ziende kubana hizi Halmashauri kwenye suala la matumizi; kwa mfano kabla ya mwaka 2019 kwenye Jimbo langu vijiji vilikuwa vinakusanya mapato na ushuru wa mchanga kwenye vijiji kule, sasa ikachukuliwa na Halmashauri, lakini bado suala la kuzibana halmashauri kuhakikisha kwamba, ile asilimia 40 inarudi kwenye shughuli za maendeleo za maeneo husika yanayoonekana, sio tu tusikie sikie tu kwamba hapa sijui kuna gharama fulani ilitumika, no. vitu ambavyo vinaonekana na vitu tangible hilo bado halijafanyika vizuri. (Makofi)
Sasa hilo linaleta ile resistance kwamba watu wanaona kama vile wamenyang’anywa mapato yao, lakini kwa sababu hawaoni kile kinachorudi wazi. Kwa hiyo, nadhani nguvu inayotumika kwenye kukusanya, pia itumike katika kuhakikisha kwamba ule wajibu wa kurudisha yale mapato nyuma kwa wale wananchi unatekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi kama mchangiaji wa mwisho siwezi kuwa na mengi sana ya kusema, labda tu nimalizie kwa kusema kwamba yapo mambo mengine ya kisera ambayo yanatakiwa yatangulie kwanza kabla ya by-law. Kwa mfano, tuna tatizo la kutenga maeneo ya malisho, ya mifugo na maeneo ya wakulima. Leo hii ukitunga by-law kabla ya sera ya matumizi bora ya ardhi ile by-law lazima italeta mgogoro tu. Kwa hiyo, zitangulie kwanza hizi sera husika ziweze kupitia katika michakato na zikubalike halafu, ndio twende kwenye by-law hapo zitatekelezwa vizuri. Suala la kutimiza sheria bila shuruti tutaliona kwa vizuri zaidi, kuliko sasa hivi ambapo inaonekana wakati mwingine kama ni vita kati ya wananchi na mamlaka zetu husika. Vinginevyo kwa kweli mimi niendelee kushukuru kwamba hasa katika bajeti hii mamlaka hizi za Halmashauri zimepewa nguvu ya kutosha. Kwa hiyo, sisi kama sehemu ya Mabaraza ya Madiwani tukitimiza wajibu wetu, nina hakika tutakwenda vizuri na wananchi wataona faida ya ushuru na tozo mbalimbali ambazo wanalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)