Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge

Hon. Dr. Adelardus Lubango Kilangi

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kidogo katika taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla kama ambavyo imekuwa ikitokea kila mwaka tunazipokea changamoto mbalimbali ambazo zimeainishwa na Kamati na kwa kweli tunawashukuru na kuwapongeza sana. Kama ambavyo wengi wa Waheshimiwa Wabunge wamezungumza hapa ndani, wanafanya kazi kubwa sana ya kufanya uchambuzi na hasa kwenda kwenye maudhui. Kwa sababu, sisi wakati mwingine tunaangalia tu yale masuala ya kiufundi ya kisheria, lakini masuala ya maudhui kwa kweli, Waheshimiwa Wabunge na Kamati wanaweza wakatusaidia sana katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kila wakati tunapokea mapendekezo hayo na maono hayo tunayachukua na tunayafanyia kazi kila mwaka. Lakini pengine wengi watakubaliana nasi kwamba kadri tunavyokwenda hizi changamoto zinazidi kupungua, ndio kusema kwamba, tunazifanyia kazi changamoto ambazo zinakuwa zimekwishaelezwa kila wakati uchambuzi unapofanyika.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa ufupi tu zimeelezwa bado zile zile changamoto za sheria ndogo kupingana na sheria mama, kuna masuala ya kuweka tozo katika Kanuni au katika sheria ndogo, kuna masuala ya kutoshirikishwa wadau wakati wa utengenezaji wa sheria ndogo na pengine katika mazingira baadhi ya sheria hizi zinaonekana zinabeba labda maslahi binafsi.

Mheshimiwa Spika, sisi kama walivyosema Wabunge wengine tunaendelea kusisitiza kwamba misingi ya utengenezaji wa sheria ndogo ipo wazi na imeelezwa vizuri sana na tumeendelea kuieleza. Tunaomba kwamba misingi hiyo iendelee kufuatwa wakati wa utengenezaji wa hizi sheria ndogo na wakati wowote misingi hii isiachwe.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna jambo nilipenda niliseme hapa, sheria nyingi zinazolalamikiwa ni sheria ndogo zilizotungwa na Halmashauri zetu. Sasa katika Halmashauri zetu Waheshimiwa Madiwani ndio wanahusika, lakini pia Waheshimiwa Wabunge pia ni Wajumbe katika Mabaraza hayo. Nilikuwa napenda kutoa wito kwamba ningewaomba sana Waheshimiwa Wabunge, wachukue muda wa kutosha waangalie hizo sheria zinazopendekezwa katika Halmashauri hizo na kuona kama baadhi ya changamoto hizi ambazo zinalalamikiwa zipo na basi zifanyiwe kazi katika ngazi hiyo. Tukifanya hivyo na Wabunge wote wakitimiza wajibu wao tutakuwa tumepunguza sana changamoto nyingi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu changamoto za kiuandishi tumekuwa tunaendelea kuzungumza kwamba tuna zoezi na ambalo ni endelevu la kuwapatia uwezo wanasheria wetu waliopo maeneo mbalimbali kwenye Halmashauri, kwenye Taasisi, kwenye Wizara, uwezo wa kuweza kufanya hiyo kazi ya uandishi wa sheria katika weledi unaotakiwa. Hata hivyo, kama ambavyo tumekiri na imeelezwa na watu wengi taaluma ya uandishi wa sheria sio jambo rahisi. Kwa hiyo, pengine hutegemei sana kwamba, kwa semina ya wiki moja utaweza kuwafanya watu wawe na umahiri kama alionao Mwandishi Mkuu wa Sheria.

Mheshimiwa Spika, lakini vinginevyo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ipo tayari wakati wote na tunatoa msaada wakati wowote tunapotakiwa kuweza kuboresha hizi sheria ndogo.

Mheshimiwa Spika, kwa mchango huo, naomba kuwasilisha na nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)