Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge

Hon. Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, KAZI, BUNGE, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, na mimi kwanza nianze kwa kukushukuru sana kwa kuipa nafasi Serikali, ukianza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini na mimi pia kwa niaba ya Serikali kuweza kupata fursa ya kutoa mchango kidogo, kuhusu hoja hii ambayo umeiweka leo mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Kwanza kabisa nadhani tutakubaliana Waheshimiwa Wabunge wote tuchukue nafasi nyingine ya pekee kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kutimiza siku 100 za utendaji wa kazi akiwa ameonesha historia ya kufanya vizuri ndani ya siku 100 za utendaji wake wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ninaposimama hapa majukumu mengine niliyopewa kwenye Hati Idhini ambayo inanipa kazi hii ya kuwa Chief Whip ndani ya Bunge ni kuwa kama mchezaji kiungo kati ya Serikali na Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba tu niseme kwamba mafanikio haya ambayo tunayapata ndani ya Serikali, hatuwezi kusema pia hayajachagizwa na wewe mwenyewe Spika na Bunge lako Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, lakini tuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kuendelea kuishauri Serikali katika masuala mbalimbali na hatimaye kuifanya Serikali iweze kutekeleza wajibu wake sawasawa na kwa kweli tuweze kusimamia masuala mbalimbali ya uendeshaji wa Serikali wa siku kwa siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja iliyopo hapa mbele yetu imeletwa na Kamati ya Bunge lako Tukufu, Kamati ya Sheria Ndogo inayoongozwa na Dkt. Rweikiza akisaidiwa na Ndugu yangu Dkt. Ridhiwani Kikwete. Inshallah na wewe siku chache zijazo nadhani mambo yatakuwa sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli niwapongeze sana viongozi hawa wawili wa Kamati ya Sheria Ndogo, pamoja na wajumbe kwa kazi kubwa wanayoifanya. Umesema hapa na umewasikia Wajumbe waliposimama hapa mbele, kila mmoja mjumbe aliyechangia alikuwa anasema wakati anateuliwa kwenye Kamati hii alikuwa haelewi hii Kamati maudhui yake na utendaji wake wa kazi, lakini alipoingia ndani ya Kamati ndio aliona umuhimu wa Kamati hii ndani ya Bunge, lakini umuhimu wa Kamati hii katika kusimamia haki za Kikatiba za wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi naomba niungane na Kamati na kazi nzuri inayofanywa na Kamati na niseme kwa kweli kama tunahesabu Kamati ambazo ni muhimu kwa utendaji kazi wa kila siku wa Serikali, lakini mapokeo yake kwa wananchi Kamati hii inayoshughulikia sheria ndogo pia ni Kamati muhimu na inafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiaw Spika, ninasema hivyo kwa nini, kwa sababu, kifungu cha 38(1) cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria, ikienda sambamba na kifungu cha 43(2) cha Kanuni za Bunge kinatuagiza sisi Serikali kuweka mezani nakala ya Magazeti ya Sheria Ndogo zote zilizotungwa kwa mujibu wa Katiba. Ili Bunge lenye majukumu ya kutunga sheria litutizame sisi Serikali na watendaji wote ndani ya Serikali, kama tunayatumia madaraka hayo vizuri na Bunge liweze kuturekebisha pale ambapo hatutendi haki kwa niaba ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kazi hii tumekuwa tukiifanya na Waheshimiwa Wabunge mmeniona nikiweka hayo magazeti hapa mezani. Bunge lako la Kumi na Moja liliweza kufanya kazi ya kupitia sheria hizi ndogo takribani 2,601 na sheria 547 zilifanyiwa kazi na kukutwa na dosari na ikatupasa Serikali turudi tukajipange upya na kufanya mabadiliko kwenye sheria hizo kwa ustawi wa Watanzania. (Makofi)

Kwa hiyo, nataka kuyasema haya tuone Bunge hili lilivyo na nafasi nzuri na nakumbuka Kamati ile iliyopita, ilifanya kazi nzuri wakina Mheshimiwa Mdee na Mheshimiwa Chenge akiwa Mwenyekiti, ilikuwa kweli ukienda kwenye Kamati ya Sheria Ndogo unaona unakwenda kukutana na miamba na sasa hivi, unapowakuta kina Ridhiwani na kina Dkt. Rweikiza, unajua kabisa ile Kamati inaenda kufanya kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi ninapokwenda kule huwa ninajiandaa kweli kweli kwa sababu hakuna mchezo unatakiwa ukatoe maelezo fasaha. Bunge lako hili kwa siku hizi 100 limeweza kupitia Sheria Ndogo 915, kwenye hii Kamati ya Sheria Ndogo na imegundua dosari 119 kwenye sheria 23. (Makofi)

Ninaomba nitoe ahadi mbele yako; kwanza, tutaendelea kuyaheshimu mamlaka ya Kikatiba ya Bunge katika udhibiti wa sheria hizi ndogo zifanane na matakwa ya sheria mama ambazo zimekuwa zikitungwa na Bunge lako Tukufu. Kwa niaba ya Waheshimiwa Mawaziri wenzangu na Serikali nzima kwa ujumla tutaendelea kuheshimu jukumu hili la kikatiba mlilopewa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, Wizara yangu inasimamia masuala ya sera, tutajitahidi kuhakikisha Sheria ndogo, sheria mama zinaendana na sera zilizotungwa ili ziweze kwenda sambamba na ziweze kutekelezeka vizuri.

Mheshimiwa Spika, lakini tuna maazimio hapa kama manne ambayo yameletwa na Kamati hii ya Sheria Ndogo, yanatutaka Serikali tukayafanyie kazi. Ninaomba nikuhakikishie Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ina jukumu la kuratibu shughuli za Serikali Bungeni, tutahakikisha kila Wizara na kila Taasisi, ambayo imepewa maelekezo ya kufanya maboresho na marekebisho ya sheria hizi, tutakwenda kuyafanyia kazi na tutarudi kutoa taarifa ndani ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la mwisho Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema ndani ya Serikali tumeamua kujipanga, yapo mambo ambayo tutayafanya iIkiwa ni pamoja na kufanya training ya kutosha kwa wanasheria wetu kwenye level mbalimbali, lakini kufanya uunganishaji kwa sababu ni lazima sheria hizi zizungumze katika Taasisi moja, Wizara moja, Wizara nyingine, Halmashauri, sheria hizi ziweze kuzungumza. Tumeona hapa tafsiri ya sheria moja kwenye taasisi nyingine na taasisi nyingine zitatofautiana, lakini lengo ni moja.

Kwa hiyo, mapungufu ya namna hii kwa kweli kwa mikono miwili tunayachukua na tunaahidi kwamba tutakwenda kuyafanyia kazi lengo letu mwisho wa siku tuweze kufanya vizuri. Ufanyaji vizuri wa sheria ndio utendaji wa haki kwa watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaunga mkono kabisa hoja ya Kamati na kama Serikali, tunachukua wajibu wetu wa kwenda kuyatekeleza yale yote ambayo yamewekwa kwenye maazimio haya ya Kamati.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, na ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. (Makofi)