Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Allan Joseph Kiula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kukupa shukrani kwa kunipatia nafasi ya kutoa mchango wangu katika Wizara hii muhimu jioni ya leo. Nachukua nafasi hii kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na timu yake kwa reforms ambazo zinaendelea katika Sekta ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumza Mbunge aliyepita hapa kwamba ukienda Muhimbili unaona mabadiliko na ziko sehemu nyingi ambapo ukienda unaona mabadiliko; nami nafananisha utendaji kazi wa Rais wetu na Mawaziri hawa kama ile theory ya Japan, “Gemba Kaizen Theory,” ambayo inasema lazima uende kwenye gemba. Lazima uende mahali shughuli zinapofanyika ili uweze kutoa majibu sahihi kwa changamoto sahihi ambazo zinakuwepo…
Ni sababu ya urefu jamani, samahani! Nitakuwa napiga magoti. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema kwamba, utendaji kazi wa Waziri na Mawaziri umechukua ile theory ya Japan, inaitwa Gemba Kaizen Theory ambayo inasema uende kwenye eneo la tukio ili uweze kutatua matatizo. Unaona changamoto, unatatua matatizo hayo. Pia nawapongeza Madaktari na Wauguzi ambao wameendelea kufanya kazi bila kuchoka kwa weledi mkubwa kuokoa maisha ya Watanzania tukitambua kwamba population yetu sasa hivi ni zaidi ya milioni 48, hivyo tunahitaji kupata huduma hiyo muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie suala la haki ya kupata tiba. Suala la haki ya kupata tiba ni sawa sawa na haki ya kuishi, kwa sababu ukipata tiba ina maana unaendelea na maisha. Sasa nikiwahamisha Bunge hili nilipeleke katika Jimbo langu la Mkalama, tunao wakazi 188,000. Wakazi hao hawana Hospitali ya Wilaya, tunatumia Hospitali ya Mission. Vituo vya Afya vilivyopo ni vitatu, Zahanati zilizopo ni 24. Facilities hizo ndizo zinatoa huduma kwa idadi hiyo ya wakaazi. Wakaazi hao wako kwenye remote area, yaani maeneo ya pembezoni. Tunaposema maeneo ya pembezoni, maana yake unaondoka kwenye njia kuu za lami unaingia porini, ukiingia porini ndiyo unawakuta hawa wananchi wa Mkalama ambapo wako ndani katika vijiji vinavyofikia 70.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza vifo vya akinamama, watoto na wazee takwimu tunazozisoma humu kwenye vitabu hivi tunavyoandikiwa zinajumuisha vile vifo vinavyorekodiwa kutoka kwenye Hospitali, Zahanati na Vituo vya Afya. Napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba vipo vifo vingi ambavyo havitolewi taarifa kwa sababu watu wanafariki majumbani. Akinamama wanafariki njiani wakienda kujifungua. Ukiangalia sisi huduma tunategemea Hospitali ya Hydom kupata matibabu. Ukitoka hapo unaenda Nkhungi, lakini unaenda Singida; na Jimbo lilivyo kubwa huduma hiyo haipatikani kwa urahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba kabisa Wizara iangalie Wilaya hizi mpya na iangalie maeneo ya pembezoni yapate uangalizi wa karibu. Pia kwa kutambua wingi wa watu na Kata; tuna Kata 17; naomba kupitia Wizara hii Zahanati zifuatazo zipandishwe ziwe Vituo vya Afya. Ihuguno, Msiu, Nduguti na Ilunda. Tukipandisha hivyo, tutakuwa na Vituo vya Afya saba. Pia tunalo gari la wagonjwa moja ambapo gari hilo ni chakavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wasiotambua ni kwamba sisi tumegawanyika kutoka Iramba Magharibi, ndiyo tukapata Iramba Mashariki. Kwa hiyo, tuligawiwa gari moja. Hatuna gari la wagonjwa. Tunalo gari chakavu ambalo halina uwezo tena wa kufanya kazi. Kwa hiyo, namwomba kabisa Waziri anayehusika na Wizara hii na Naibu wake waangalie uwezekano wa kutupatia gari la wagonjwa na gari hilo liwe jipya kwa sababu ya mazingira ya kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia suala la watumishi; tunao Madaktari wawili, watu 188,000 ukigawanya kwa Daktari wawili unapata 94,000; ukigawanya unakuta kwamba kila Daktari anahudumia watu 257 kwa siku katika siku za mwaka ukigawanya. Madaktari hawa watafanyaje kazi kwa utaratibu huo? Nasi kule tunaposema Madaktari, maana yake hata ma- clinical officer ni Madaktari. Maana yake hapo wenzetu wanapozungumza Madaktari wanazungumzia Madaktari Bingwa, lakini tunaoishi nao kule ni akina nani? Tuna upungufu wa Madaktari 21, Wauguzi 113 na Maabara 23. Tunaomba ufanyike mpango mahsusi tuweze japo kupunguziwa pengo hilo la wafanyakazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali yetu ya Nkhungi ambayo ni ya Mission na yenyewe iweze kupelekewa Madaktari Bingwa waweze kuendelea kutoa huduma wakati ambapo tunasubiri mabadiliko zaidi ambayo tunatarajia tutayapata ndani ya miaka mitano hii. Pia ukiangalia sasa hivi kuna magonjwa yasiyoambukiza (non communicable disease), sasa kule vijijini watu wanapokuja huku mijini kupata huduma wanakuwa wameshachelewa. Cancer, fibroid, sukari, BP, Cardiovascular Disease, magonjwa ya figo, hayo yote ni matatizo makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kabisa, uwe unafanyika utaratibu maalum kuwa na mobile health services au Kit Program za Madaktari; wanapelekwa, wanatembelea wilaya hizo na kuwapima watu na kuwasaidia, hasa akinamama ambao ndiyo waathirika wakubwa. Program hizo zikiwa zinafanyika katika kipindi cha miezi mitatu mitatu, zinaweza kutusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala ambalo limezungumzwa na kila Mbunge hapa linaloitwa CHF. CHF ni tatizo kubwa! Tunasema ni tatizo kubwa kwa sababu tunawahamasisha wananchi wanachanga, wakimaliza kuchanga hawapati matibabu na mwaka ukiisha wanatakiwa wachange tena. Sasa hivi tunatakiwa tuwaambie wananchi wachange na dawa hawakunywa; hiyo ni changamoto kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara iweze kuangalia jambo hili na kuweka utaratibu mzuri kuhakikisha wananchi wakitoa hizo fedha wapate dawa. Dawa ziwepo wapate na vipimo vinavyohusika, tumeambiwa kwamba dawa zikiwa hazipatikani MSD, kutakuwa na mzabuni kila mkoa. Jambo hilo Mkoa wa Singida halijafanyika na lenyewe liangaliwe ili dawa ziweze kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maslahi ya wafanyakazi wa Wizara hii yaangaliwe kwa karibu kwa kuzingatia mazingira magumu. Sisi ambao tuko pembezoni, Madaktari wetu wanafanya kazi masaa 24 kwa siku saba, wanapata kitu gani cha ziada? Siyo hivyo tu, mgawanyo wa Madaktari hao; Madaktari wanaishia mijini. Wakifika Singida, wanageuka, wanarudi walikotoka au wanakwenda kwenye hospitali binafsi. Jambo hilo linatakiwa liangaliwe na Madaktari wafike kule kwa kuweka incentives mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la matibabu bure kwa wazee na lenyewe liangaliwe. Mheshimiwa Waziri ametoa circular, ipo, lakini haijasimamiwa kikamilifu. Bado malalamiko yako kila upande, wazee wetu wanapata tabu, wananyanyaswa. Wilaya ya Mkalama ni wilaya changa, mapato yake ni kidogo sana. Tunapofikia mahali tunasema wilaya ijenge hospitali, hiyo ni changamoto. Tunaomba Wizara itutafutie mfadhili au ichukue hatua za makusudi kuhakikisha kwamba tunapata Hospitali ya Wilaya ili iweze kutoa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, alizungumza Mbunge mmoja suala la mafunzo, naomba Sekta ya Afya, Wizara iangalie namna kwenye Vyuo, wanafunzi hao waweze kupata mikopo, waweze kusoma, kwa ngazi ya cheti, ngazi ya Diploma na kwenda mpaka juu. Kwa sababu wakisoma na tukiweka mkakati wa miaka mitano, mpaka itakapokwisha, pengo hili litakuwa limemalizika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri na naomba mambo ambayo tumeyatoa yazingatiwe na hasa sisi ambao tunatoka katika maeneo ya porini. Mimi naita kule ni porini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.