Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Kama ambavyo mtangulizi wangu amesema Mheshimiwa Eng. Ezra, nami pia ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara. Tumetumia muda hasa kupitia huu Mkataba na mapendekezo yaliyoletwa mbele yetu na Serikali na pia tulipata nafasi ya kuwaona wadau mbalimbali wakiwemo TCCIA na CTI tumesikia pia maoni yao na baadaye tulikutana na maoni ya mwavuli wa watu fulani walioungana, inaitwa Trade Investment Coalition (TIC) juu ya Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba na Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara Afrika ndiyo ambao tunajadili hapa sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mchango wao waliouleta kwenye Kamati ungeingia kwenye Hansard kama pia sehemu ya mchango wangu ili kuweza kuboresha zaidi na watu waweze kujifunza baadaye.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Waheshimiwa Wabunge waridhie huu mkataba lakini lazima tuuridhie kwa tahadhari. Kwa sababu Tanzania tumekuwa na tendency kidogo wakati fulani ya kujilizaliza au kulalamika kwenye mambo ambayo sisi wenyewe labda hatuna nia nzuri ya kuyafanyia utafiti ili tuweze kuona tunakwenda wapi? Naomba radhi sana Waheshimiwa Wabunge waliochangia hapa kwenye hili swali linalohusiana na suala la mahindi na ndugu yangu pale ametumia mfano huo huo, na mimi naomba nitumie mfano huu ili kuweza kujenga hoja yangu vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema NFRA wanatakiwa wakanunue mahindi, halafu wayahifadhi na yaende kutumika labda wakati wa majanga. Pia tunatamani wafanyabiashara wa nje nao waje wanunue mahindi yetu Tanzania. Sasa swali ambalo sisi kama Watanzania tuna haja ya kujiuliza, mahindi yetu yana ubora sawa na mahindi yanayolimwa Kenya? Kwa nini Wakenya wasi-saturate kwanza market yao halafu wakaja kuchukua kwetu kiasi kidogo kwenda kujazilizia kwa sababu ya tofauti ya ubora?

Mheshimiwa Naibu Spika, hili liko wazi, tulifanya semina na ndugu yangu Mheshimiwa Engineer Ezra hapa alisema kidogo suala la GMOs; mpaka sasa watu wanaotumia kilimo cha kisasa au kutumia GMO ili kuweza kupata mazao bora, ni wachache sana Tanzania, kitu ambacho kinatusababisha tushindwe kuingia vizuri kwenye soko bora kwa sababu ya ubora wa mbegu hata tunazozalisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, siku moja jaribu kufanya utafiti, chukua mahindi ya Tanzania halafu chukua mahindi ya Zambia, yaweke yote Mezani. Kuna kipimo wanachotumia, ni kama kanyundo fulani kadogo ili kuweza kuangalia ubora wa ile grain. Hindi la Tanzania ukiligonga linatawanyika, lakini ukichukua hindi la Zambia ukiligonga, litakatika vipande vine, vitano au sita. Ndiyo kipimo wanachokitumia, kwa hiyo, mwisho wa siku wanasema mahindi yetu hayana ubora kwa sababu watapata takataka nyingi zaidi kuliko ambavyo unaweza ukapata unga ulio bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninachotaka kusema ni kwamba tunaingia kwenye ushindani wa soko; na katika ushindani huu, pale ndani kuna sheria nyingi. Kwa mfano, Kifungu Na. 39 kinasema kinataka kulinda viwanda vidogo vidogo vya ndani. Sasa unavilinda viwanda vya ndani ambavyo vinatumia malighafi ambazo siyo bora sana ukilinganisha na nje ambako tunategemea ndiyo sehemu utakakokwenda kuuza kama wao wanavyokuja kuuza kwetu, kama ambavyo sasa hivi tumekuwa tukilalamika labda tumevamiwa na soko la China au tunavamiwa labda na soko la jirani hapo Kenya. Kwa hiyo, lazima tuangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa namwomba sana Mheshimiwa Waziri kwamba pamoja na kutaka kuridhia Mkataba huu, lakini lazima tukatoe elimu ya kutosha kwa Watanzania kwamba sasa hivi tunakwenda kwenye mashindano ya kibiashara na tunaongezewa mkataba mwingine mpya. Kwa hiyo, kama hatujaweza kwenda vizuri, kwa mfano, kwenye Mkataba wa Afrika Mashariki, tumekuwa hapa kila mara tunasema tunaona labor mobility, tunaona na masuala ya movement of labor; Wakenya wanapokuja Tanzania kwenye hospitality businesses unafurahia zaidi huduma kuliko ambavyo sisi tunaokwenda kutoa kule kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na maboresho yote, nakushukuru kwa kunipa nafasi, lakini tuwatake Watanzania tuendelee kujifunza ili tuweze kutoa kilicho bora. Ahsante sana. (Makofi)