Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buchosa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu katika kupitisha Azimio hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ni-declare interest kwamba ni makamu mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara na nilikuwepo kwenye mjadala mrefu sana kuhusiana na mkataba huu. Cha kwanza niliposoma mkataba huu mambo mawili yalinikuta la kwanza niliingia hofu, hofu yangu ya kwanza kabisa ilikuwa ni kwamba mkataba huu utaua viwanda vyetu, mkataba huu utaondoa ajira zetu, huo ni upande mmoja, lakini kuna upande mwingine mzuri sana wa mkataba huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ambao ulikuwa ni kwamba Afrika sasa inakwenda kufanya integration, Afrika inaanza kuuziana Afrika kwa Afrika, Afrika inaanza kufanya biashara Afrika kwa Afrika jambo ambalo huko nyuma lilikuwa halifanyiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipofika hapo nikaamua kuchagua upande wa uzuri wa mkataba, nikaamua kabisa kuachana na hofu ambayo ilikuwa imenikamata na hivi sasa nimesimama hapa kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote kwa ujumla wetu tuweze kuridhia Azimio hili nchi yetu ikaweze kuingia katika mkataba huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale waliowahi kusoma kitabu cha Walter Rodney how Europe underdeveloped Africa, alisema Walter Rodney ukitaka kuichezesha Afrika isababishie tu iwe na disintegration yaani tu tuwe hatuna ushirikiano na wakoloni walifanya jambo hili kwa umakini kabisa na wakatugawa wakaweka mipaka ardhini baadaye mipaka hiyo ikaamia kwenye vichwa vyetu. Kwa hiyo, tunatembea hapa Watanzania nikivuka tu pale Namanga kuingia upande wa Kenya hofu inaniingia. Na wakati narudi nyumbani nikivuka Namanga nikiingia upande wa Arusha kiburi kinaanza. Kwa hiyo, kuna mipaka tunayo ndani ya vichwa vyetu hiyo ndiyo itakayotuchelewesha kuweza kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba huu au Azimio hili linakwenda kuondosha barrier zote ambazo zilikuwepo ili sasa Afrika ifanye biashara Afrika kwa Afrika, ukijaribu kuangalia data ambazo zipo Afrika kwa Afrika kwenye Intra business, biashara ya ndani ya Afrika kwa Afrika ni asilimia 17, lakini ukiangalia Asia ni asilimia 69, ukiangalia North America ni asilimia 31. Kwa hiyo, ninachojifunza hapa ni kwamba tunafanya hii biashara sisi kwa sisi kidogo sana hatuwezi kukua mpaka tuweze kuondoa barriers, tuanze ku-trade kati ya Taifa na Taifa. Hapa tunazungumza tuna mahindi si ajabu kuna nchi haina mahindi, inahitaji mahindi lakini unaweza ukashangaa ikaagiza mahindi Brazil badala kuagiza mahindi Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naunga mkono Mkataba huu na ninaomba kabisa Waheshimiwa Wabunge wote turidhie kwa nia moja tuachane na hofu, tukubali kwenda kujifunza tukiwa tunafanya kuna learning unapokuwa unafanya na kuna kujifunza kwanza ndiyo ufanye. Ninawaomba tukubali nchi yetu iingie tukajifunze tukiwa tunatenda, tutarekebisha huko ndani kwa ndani, tutabadilisha mikakati tukiwa tunavyozidi kwenda tuta-change strategies, hatimaye tutaweza kuweza tutaweza kufanya vizuri hatutaweza kupata faidia kwenye mwaka wa kwanza au mwaka wa pili lakini nina uhakika kabisa baada ya muda si mrefu tutafanya vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la muhimu sana ni capacity building ni lazima nchi yetu iwawezeshe wafanyabiashara wetu. Ni lazima wapewe mikopo yenye riba ndogo, ni lazima tutambue ya kwamba Nigeria uchumi wake ni mkubwa sana kuliko uchumi wetu sisi. Ukinipambanisha mimi na Okwonko sasa hivi kuna uwezekano wa ku-fail, lakini kama nimewezeshwa na nchi yangu kama nchi yangu inadhamira ya kweli political will kwamba tunawapeleka hawa watu vitani wakapambane tutahakikisha kwamba wanashinda lazima tutashinda vita hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, South Africa ilifanya hivyo wakapatikana wakina Patrick Motsepe ni wakati wa nchi yetu tutengeneze mabilionea wengine wapya. Tumekuwa na mabilionea wale wale miaka hiyo tangu tukiwa watoto ni wakati sasa tuanze kusikia majina ya Aweso, tuanze kusikia majina ya kina Kigwangalla wakiwa mabilionea tumechoshwa na majina yale yale kila mwaka. Kwa mkataba huu nina uhakika wakiwezeshwa vijana wa kitanzania tutasikia majina mapya, kuna uwezekano kabisa wa kutengeneza wakina MO wengine, kutengeneza wanakina Bakharessa wengine kwa mkataba kama huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu niseme kwamba tariff za kodi; tariff za kodi tusipoziangalia vizuri zitatuumiza. Nitatoa mfano mmoja hai nilitembelea kiwanda kimoja cha mapipa pale Mbagala, Mhindi anatengeneza mapipa mazuri tu lakini anashindwa kuuza Kenya, kwa sababu gani anashindwa kuuza kenya Kodi, Wakenya wanapoagiza sheet za chuma pale kwao hawatozwi kodi kwa sababu wananunua kwenye COMESA, wananunua Egypt. kwa sababu wako ndani ya COMESA hawalipi kodi asilimia 10, lakini yeye anapoagiza hapa analipa ten percent na Wakenya wakitengeneza mapipa yao pale kwa sababu ni EAC wanauza soko la Tanzania. Kwa hiyo matokeo yake mapipa yale yanakuwa chini kwa asilimia 10 upande wa bei lakini mapipa ya Mbagala yanakuwa juu, hawezi kuuza Kenya, hawezi kuuza hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kodi zetu tuzitazame vizuri wenzetu tunapotoa tariff ya kodi wanaziangalia hivi Tanzania import duty wameweka shilingi ngapi, wao wanapunguza kidogo ili waweze kushinda kwenye soko/wawe competitive kwenye soko. Ombi langu tariff za kodi tuwe smart kwenye eneo hilo, tuzipitie tuziangalie na tuwe smart kuwashinda wenzetu. Kwa nini mtu anatoka hapa anaenda kununua masharti Kampala anakuja kuyauza Dar es Salaam anapata faida, hapo kuna tatizo kwenye types za kodi kama mnataka bidhaa zetu ziweze kushinda kwenye soko tuziangalie types za kodi na ziweze kupunguzwa kushindana na wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono Azimio. (Makofi)