Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii, lakini mchango wangu utajielekeza sana nianze kwenye eneo la actors wa Mpango wenyewe. Maana kupanga jambo moja, kutekeleza jambo la pili, mipango yetu ni mizuri sana na kila mwaka tumekuwa tukiwa na mipango mizuri ya namna hii. Lakini nijielekeze kwa actors wa Mpango huu yaani watekelezaji wa mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kwa namna ambavyo sekta ya Utumishi wa Umma inapimwa. Taasisi zetu za Serikali zinapimwa kwenye uwajibikaji. Ukisoma Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura Na. 298 imeeleza kuhusu namna gani Watumishi wa Umma wanapimwa yaani kuna OPRAS inaitwa Open Performance Review and Appraisal (OPRAS). Mimi nimehudumu na nilikuwa Mtumishi wa Umma kama Mkurugenzi wa Jiji kwa kipindi cha miaka minne na miezi kadhaa, hapa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna jambo gumu sana kwenye kumpima Mtumishi Umma ni kwenye ujazaji wa OPRAS. OPRAS ni formula tu na kama utaratibu ambao tumeuzoea hizi business as usual. Kumpima Mtumishi wa Umma au Taasisi za Umma kwa kutumia OPRAS nadhani jambo hili limepitwa na wakati. Ukitazama eneo hili la OPRAS, ukitazama nchi zingine kwa mfano wenzetu Rwanda, Kenya na nchi zingine wanatumia Performance Contract kwenye kuwapima watumishi wake. Leo hii nikiuliza hapa bahati mbaya najaribu kuangalia Waziri wa Utawala Bora, Utumishi wa Umma sijamuona, nikiuliza hapa ni watumishi wangapi nchini wameshushwa vyeo kwa kupimwa performance yao, si tuna OPRAS yes! Mimi nimehudumu na nilivyokuwa Mkurugenzi wa Jiji ni mamlaka ya nidhamu lakini ni mwajiri pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimepata uzoefu hapo kidogo ni ngumu sana kumpima Mtumishi wa Umma kwa kutumia OPRAS, ni formula tu! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu tunaona Mheshimiwa Rais, anapambana kweli kweli, usiku na mchana kwa ajili ya Taifa letu, lakini namna gani anasaidiwa kupima performance ya taasisi zake? OPRAS nadhani imepitwa na wakati, tuanze sasa na mfumo ambao wenzetu wanautumia duniani nimetoa mfano wa nchi mbili, nimesema Rwanda, leo hii Kagame anavyomteua Mkurugenzi wa Taasisi au kiongozi yeyote anakuja anampa malengo ya mwaka na anamwambia ndani ya mwaka ukishindwa kutimiza malengo haya uje na resignation letter, yaani uandike barua ya kuacha kazi mwenyewe au vinginevyo. Sasa sisi tunapima kwa kuangalia Vyombo vya Habari na sasa hivi tunakwenda kwenye Vyombo vya Habari, hapana huu utaratibu haufai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumsaidie Mheshimiwa Rais kwa mfumo wa performance contract ndiyo mfumo unaotumika sasa duniani, ndiyo mfumo wa kisasa, kila mtu ataachia ngazi mwenyewe wala huna haja ya kuhangaika na mtu, anapewa malengo kwa sababu tuna mpango mkakati, anapewa malengo na unaainisha majukumu yake, asipotimiza analeta barua tu ya kuacha kazi mwenyewe kwa level yoyote ile. Sasa OPRAS weakness nyingine inagusa tu Watumishi wa Kada za chini, leo hii taasisi zetu kwenye ngazi za Wizara tunapimaje?

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKTI: Taarifa. Nakuruhusu uko ulipo aah! Mheshimiwa Tunza.

T A A R I F A

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemuelewa mzungumzaji nataka tu nimpe taarifa na wananchi wa Mlimba naye wampe Performance Contract ili akimaliza miaka yake mitano naye wamuone ame-perform vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Kicheko)

MWENYEKITI: Actually, Wabunge mnapimwa kwa performance contract, kabisa tofauti na wafanyakazi, hakuna OPRAS kwa wapiga kura. Ume-perform unachaguliwa tena, huja-perform wajumbe wale wanakupiga nje kabisa. Mheshimiwa endelea nimetunza muda wako. (Kicheko)

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba niendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuna Waraka mwingine ukiachana na Sheria hii Sura, 298. Mwaka 2018 kulikuwa na Waraka wa Serikali juu ya jambo hili ninalozungumza hapa, wala siyo jambo geni. Sasa hoja yangu sijui inaishia wapi na ninaomba baadae kwenye hitimisho tungepata maelezo kwamba ule waraka maana yake Waraka ni sehemu tu lakini tunaweza kuona na mimi ushauri wangu mwishoni, sasa tuitazame upya hii Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura Na. 298 tuifanyie mapitio upya, badala ya OPRAS tuweke Performance Contract. (Makofi)

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Ruhusa!

T A A R I F A

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwenye eneo la OPRAS na utekelezaji wake sasa hivi tunaona mwaka 2017 Watumishi wengi waliondolewa kazini kwa kigezo cha OPRAS. Tena hapa, OPRAS imetumika vibaya sana, kuna tick tu ya kujaza kwamba nipo form four bila kuthibitisha cheti nimekileta au sijakileta lakini ukizingatia mwajiri ndiyo mwenye sifa zangu zote wakati ananiajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo OPRAS imeondoa Watumishi zaidi ya 4000 na wameshindwa kuwarudisha kazini. Hata hawajapeleka cheti chochote cha Form Four wala Form Six, OPRAS tu imesema form four wakati miaka 20 kafanyakazi akiwa darasa la saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nampa mzungumzaji taarifa hiyo.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei taarifa hiyo. OPRAS haihusiani kabisa inahusiana na performance, nazungumza performance. Brother nazungumzia performance.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unanielewa nazungumzia performance. Kuondoka kwa Watumishi wa Umma hakuhusiani kabisa na OPRAS, OPRAS inapima.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunambi unaongea na mimi endelea. (Kicheko)

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wananitoa kwenye mstari ngoja niendelee tu. Namsamehe kwa sababu mimi ni Chief wa Waluguru ninamsamee aendelee kwa sababu yeye ni mdogo wangu huyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze katika sekta ya kilimo, nitoke huko niongelee sekta ya kilimo.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa! (Kicheko)

MWENYEKITI: Taarifa!

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nimpe taarifa mzungumzaji Mheshimiwa Kunambi kwamba hata katika promotion za Utumishi wa Umma ni lazima OPRAS itumike. OPRAS ile inavyotakiwa kujazwa ni kwamba yule supervisor anamjazia subordinate wake, utendaji kazi wake na kuona lakini tunafanyia maboresho kwamba sasa tutaijaza ile OPRAS kutokana na job description yako mwenyewe badala ya kuwa one fit all sasa hivi itakuwa Mhudumu atakuwa na job description yake ambayo ataijaza pale, ukija Injinia atakuwa job description yake na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kuitumia OPRAS katika kupima performance ya Watumishi wa Umma, ila tu kuna vitu ambavyo vitaongezewa na ndivyo tutavitumia hivyo vigezo hata katika kuangalia namna gani tunafanya promotion katika Utumishi wa Umma.

MWENYEKITI: Hoja ya Mheshimiwa Kunambi ni kwamba, kupima performance kwa job description ni msingi mbovu. Pima performance kwa kupima performance indicators. Ulitakiwa ufanye, tumekupa kazi tarehe fulani, ulitakiwa ufanye 1, 2, 3, 4, 5, …10 umeyafanya? Watu hawafanyi kazi! Ndiyo maana Kunambi alitandika makofi baadhi ya watu hapa Mjini.

Mhehimiwa Kunambi endelea. (Kicheko)

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nijielekeze kwenye kilimo. Sekta ya Kilimo wote ni mashahidi ni sekta muhimu sana kwa Taifa letu na mchango wake hata kipindi hiki cha Covid kilimo ndiyo sekta iliyoongoza. Asilimia 26.9 ya pato letu la Taifa, ukiangalia inafuatiwa na sekta ya ujenzi na maeneo mengine lakini kilimo ndiyo tunasema sekta muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niombe tu, nimeona kwenye mpango tuna miradi takribani 21 ambayo imekamilika kwa mwaka uliopita kwa Bilioni 7.5. Umwagiliaji utatusaidia sana kuinua kilimo chetu Nchini, nadhani Serikali sasa iongeze bajeti kwenye umwagiliaji lakini haitoshi siyo tu kwenye umwagiliaji tuwe na Agro-Base Industries, viwanda vidogo vidogo vinavyo chakata mazao ya kilimo kuwa bidhaa, tuwekeze huko. Lakini pia tuongeze tafiti za masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mimi ni mkulima wa mpunga, nina mpunga ndani sijauza gunia moja sasa ni shilingi laki moja, kutafuta hilo gunia moja ni zaidi kama 112,000. Sasa unauza laki moja si hasara hiyo? Nimefungia mpunga ndani! Kwa hiyo, Serikali ijielekeze kufanya tafiti ya masoko pia, tulime kwa umwagiliaji lakini pia ifanye tafiti za masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihitimishe kwenye jambo la barabara. Bahati nzuri barabara ya Morogoro – Njombe border ni barabara inayofungua uchumi wa nchi yetu na ni barabara ambayo inakwenda kutoa huduma Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Lakini barabara hiyo kwenye taarifa ya mpango nikiwa naipitia imenishangaza kidogo labda Mheshimiwa Waziri aje atolee ufafanuzi jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya mwaka wa fedha tulionao sasa, imeelezwa kwenye bajeti barabara hii kipande cha kilometa 125 kitaanzwa ujenzi na tayari upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi umekamilika. Sasa taarifa ninazopata kwenye mpango ni kilometa 220 zinakwenda kufanyiwa usanifu, zinatafutwa kandarasi za usanifu na upembuzi yakinifu wa mradi huo.

Mheshimiwa Spika, barabara hii umuhimu wake ni barabara mbadala wa Kitonga, mnaufahamu umuhimu wa barabara ya Kitonga, mizigo kwenda Zambia, mizigo kwenda South Africa, mizigo kwenda Malawi inapita Kitonga, Kitonga ikifunga na bahati fulani wakati wa masika Kitonga ilifunga tulikaa karibu mwezi mzima haipitiki ile barabara, walipata shida sana wafanyabiashara wetu. Mbadala wa barabara ya kitonga ni hii Morogoro – Njombe Border ni ya uchumi wa nchi yetu na ina-service Mikoa ifuatayo ya Njombe, Mkoa wa Ruvuma, Mkoa wa Mbeya na hadi Mkoa wa Rukwa. Ukipima umbali kutoka hapo Makambako uje uitafute Mikumi kuna zaidi ya kilometa 400, ukitumia barabara hii kutoka Makambako - Njombe kuja Mikumi kilometa karibu 300 na kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inanishangaza sana kuona kwenye mpango naelezwa habari ya kilometa 220 tafuta Mkandarasi na ADB ndiyo financier sawa! Hoja yangu ya msingi, hizi kilometa 125 ambazo upembuzi yakinifu na usanifu wa kina za mradi zimekamilika na bajeti inaeleza kilometa 50 zianze kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba maelezo ya kina kwenye hili. Ahsante sana. (Makofi)