Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango huu. Nimeona Wabunge wanzangu wengi wamezungumzia suala la kilimo, bado na mimi nitaendelea kujikita hapo kwa sababu bado nchi yetu kwa asilimia zaidi ya 65, watu wetu wanategemea kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo taarifa ya Kamati imesema, Kamati imeongea vizuri sana na imetoa maoni mazuri sana kwa Serikali, kilimo kwa asilimia zaidi ya 26 ndio inaongoza katika pato la Taifa, lakini cha kushangaza inakuwa kwa asilimia tatu mpaka nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema asilimai 65 ya watu ni wakulima bado, leo hii pesa ya maendeleo ya kilimo bilioni 200 karibu ambazo zinatengwa 294 kwa kweli ni ndogo na Kamati imeshauri imesema ni bora pesa hiyo ikaongezeka angalau ikafika bilioni 450 ili kuweza kuisaidia Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu wakulima wetu wengi sana wanajitegemea na kikubwa zaidi ambacho kinawatesa ni ukosefu wa pembejeo, ukosefu wa Wagani na watu ambao wanaweza kusimamia kazi za kilimo. Tunaomba Serikali iweze kuona umuhimu wa kuleta ruzuku kwenye mbolea. Tunaona sasa hivi hasa Nyanda za Juu Kusini ambao sisi tunalisha almost nchi nzima, leo hii kilimo bado hakijaanza kwa sababu watu wanatafakari namna gani wataendelea kulima kwa sababu mbolea zimepanda bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wa kilimo kwenye wilaya ni wachache, leo hii Serikali haijaajiri kwa muda mrefu Maafisa Ugani na waliopo hawana vifaa vya kuweza kuwasaidia kutenda kazi. Majimbo ni makubwa na maeneo wanayofanyia kazi ni makubwa wanashindwa kuwafuatilia wananchi na kuhakikisha wanatoa mazao kama inavyopaswa. Sasa kumetokea kuna watu binafsi wanaoingia kwenye mambo ya kilimo na kuwadanganya wakulima. Naamini wewe umesikia na Wabunge wenzangu wamesikia, sehemu za Njombe kuna watu wamesema kuna mazao ambao wananchi wakiyalima watapata mapato mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna zao hili la vanila, watu wametoa fedha kwa makampuni binafsi wamelima hizo vanilla, wamedanganya kilo moja ni milioni moja na mwisho wa siku hawajapata hicho ambacho walichetegemea. Serikali ilikuwa na wajibu wa kuweka Maafisa Ugani ambao wao ndio wangekuwa waanawaambia wakulima na wala sio watu binafsi, mwisho wa siku wanawadanganya. Tunahitaji kuongeza nguvu kwa watu wetu ili kilimo kiweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masoko ya mazao ni shida, leo hii kilimo cha chai katika Wilaya ya Rungwe na Mikoa ya Njombe bado chai inauzwa kwa bei ndogo sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu amejitahidi kufika maeneo yetu na tumelalamika muda mrefu, lakini bado bei inasuasua, wakati bei ya soko la dunia bado iko juu, hatuelewi kwa nini watu wetu hawapati soko la chai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ndizi zinazalishwa kwa wingi sana. Leo hii kuna nchi kama za Jamaica wanaishi kwa sababu ya ndizi, leo sisi tuna ndizi tunalima na watu wetu wanalima mwisho wa siku ndizi mkungu mmoja shilingi elfu mbili. Naomba Wizara husika isimamie kuhakikisha zao hili linakuwa zao la kibiashara vinginevyo wanaingia wafanyabiashara wale ambao tunasema ni wachuuzi, wananunua kwa kuwalangua wakulima kupeleka ndizi Malawi, kupeleka ndizi Zambia, wakati huo wanapata wao faida, lakini mkulima wa Wilaya ya Rungwe au Mkoa wa Mbeya hapati faida yoyote. Tunaomba Wizara isimamie hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwa zao la cocoa tunafahamu kuwa cocoa ni zao ambao lkinaleta faida katika dunia na Tanzania nafikiri cocoa yake ni bora, ya pili kwa maana baada ya Ghana inafuata Tanzania. Tunaomba Wizara hii na hasa Mheshimiwa Bashe najua anajitahidi, lakini kwa hili tunahitaji cocoa iongezeke bei kutoka elfu tano ambayo imepanda msimu huu, iende mbele zaidi maana soko la dunia cocoa ina bei kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Serikali ina haja ya kuongeza fedha kwa watu wanaonuna NFRA, wanaonunua mazao. Kwanza kabisa capacity ya kubeba mazao hawana kwa sababu hawana maghala mengi katika maeneo mbalimbali. Naomba Serikali iijengee uwezo taasisi hii na hasa wakati wa msimu wa kununua mazao pia wawe na pesa za kutosha waweze kununua mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoke hapo kwenye kilimo niende kwenye eneo la miundombinu. Reli ya TAZARA ilianzishwa kati ya muungano wa nchi mbili, lakini sheria iliyoanzisha reli ya TAZARA nafikiri ina upungufu kwa sasa. Tunaomba Serikali sasa ilete marekebisho ya sheria ya reli hii ili kusudi Tanzania iwekeze kwa wingi fedha zake kwenye reli hii, maana ina faida kwa Nyanda za Juu Kusini ambapo mazao mengi yanazalishwa kule. Naomba Serikali ifanye hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye sekta binafsi, sekta binafsi inasaidia sana uchumi wa Taifa letu, lakini kumekuwa na mlolongo mrefu sana kuisaidia sekta hii. Naomba Serikali iangalie makosa madogo madogo ambayo yanasababisha sekta binafsi isifanye kazi yake vizuri. Kuna urasimu mkubwa wa usajili wa makampuni mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tozo zipo nyingi, unakuta mfanyabiashara anapotaka kufungua biashara tozo zipo sehemu nyingi nyingi na zinachukua muda mrefu, anaenda kwenye dirisha moja inamchukua wiki mbili, akienda sehemu nyingine muda umekwenda, mwisho wa siku hata wawekezaji tunaowaita waje kuwekeza nchini inabidi waende nchi jirani kwa kuwa sisi tuna mambo mengi sana ya ukiritimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kabisa nchi yetu inazungukwa na nchi mbalimbali, na tunafahamu – siwezi kuitaja hiyo nchi – lakini hiyo nchi inasubiri sisi tukosee ili wao waondoe yale ambayo sisi tunayaweka kama vikwazo na kuwakaribisha hao watu waende kwao na sisi tunakosa wawekezaji. Ninaamini Serikali imekuwa ikitamka sana suala la uwekezaji na kuwaita wawekezaji wengi wafike lakini mwisho wa siku hatuna ufanisi katika kuwakubalia hao watu na kuwasaidia ili waweze kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sekta binafsi hii wanapotaka kupata mikopo kuna usumbufu mkubwa sana wa upatikanaji wa mikopo. Tumekuwa tunahangaika na kusema kila siku na riba, na wenzangu wametoka kuzungumza hapa kwamba riba zimekuwa kubwa sana. hatuwezi kusaidia sekta binafsi ikakua mwisho wa siku ambapo karibia takribani asilimia 35 inaongeza kwenye GDP ya Taifa tunashindwa kuisimamia sekta binafsi.

Tunaomba sana Serikali isimamie hilo, na katika mpango huu tunaomba sana Serikali ihakikishe kwamba inaondoa vikwazo vizivyokuwa na maana katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo kimsingi hayaendi sawasawa katika maeneo mbalimbali ya maendeleo. Tunazungumzia maendeleo ya watu, maendeleo ya watu hayawezi kukua bila kuwa na elimu bora. Leo hii wewe mwenyewe umezungumza hapo kwamba usajili wa watoto umeongezeka. Ni kweli Serikali imepeleka shule kwa ajili ya kujenga, lakini je, hizo trilioni zilizokwenda huko chini usimamizi wake ukoje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wabunge leo tumekuja ni moja ya sehemu ya fedha hizo, lakini usimamizi wake ukoje; tunahakikishaje kwamba hizo fedha zitafanya kazi kwa viwango na kutimiza ule wajibu ambao umekusudiwa? Kumbuka hili ni deni, wala siyo hisani kutoka kwa wale waliotupatia. Kwa hiyo, tunahitaji kuzisimamia, na Wabunge wenzangu naomba tuliangalie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya bado ninasisitiza kwamba tumekuwa na wimbo wa Taifa, kila siku tunarudia yaleyale lakini hayatimizi, tunapitisha kwenye bajeti ya Bunge lako Tukufu, mwisho wa siku fedha zinakwenda kidogo, tofauti na jinsi ambavyo tumeisimamia. Tunaomba kile tulichokipanga kama Wabunge kiweze kusimama kwenye Wizara husika na zikaenda kufanya kazi, hususan Wizara ya Kilimo ambayo ina asilimia kubwa ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusma hayo, ninaomba niishie hapa. Ahsante. (Makofi)