Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami niungane na wachangiaji waliotangulia kuipongeza Serikali ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu, kwa namna ambavyo wameweza kuweka ule mpango, hasa matumizi ya ile hela trilioni 1.3. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa namna ambavyo waliendelea kumshauri Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mimi kuanzia kwenye hela ile ambayo kimsingi ni hela ya stimulus yapo maeneo ambayo ningeomba tuyafanyie kazi. Kunapokuwa na mdororo wa uchumi kwa sababu yoyote ile fedha kama hii inatusaidia kurudi, ku-bounce back, kwenye kuendeleza uchumi. Tunayo bahati hatukufunga biashara zetu, hatukujifungia na ndiyo maana katika record hata kwenye taarifa hii sisi ndiyo pekee tulikuwa tuna ukuaji chanya mwaka 2019, wenzetu walikuwa na 0.3, 0.8, wengine -3.4, sisi tulikuwa tuna 4.6 kwa sababu hatukujifungia tuliendelea na kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hatujapeleka kwenye ku-stimulate biashara kama stimulus, ningeomba sana tuziangalie biashara zile zilizodhurika sana moja kwa moja na kuwepo kwa UVIKO-19 hasa kwenye utalii na hoteli. Kwa sababu, hatuwezi kuwapa hela na kwa sababu Wabunge wengi wameongelea riba za benki kwa ujumla, mimi ningesema tuwe na kipengele sasa cha kuzisaidia kabla hatujaja kwenye riba za ujumla. Kwamba, kampuni zile nyingi zina mikopo benki, zimefanyiwa restructuring, zinalipa interest bado na baadaye watatakiwa walipe na ile principle, tuweke restructuring ambayo tutaziangalia zile sekta na zile biashara tuzielekeze benki ziwapunguzie riba, ikiwezekana zisimamishe riba mpaka watakapokuwa wame-stabilize ili kuweza kuimarisha uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ushauri huo niende kwenye mpango wetu huu. Watu wengi wameongelea kilimo na mimi sitaacha kuongelea kilimo. Kuna vitu bado tunaendelea kuchanganya, kuna suala la mchango wa sekta ya kilimo kwenye GDP, hiyo ndiyo asilimia 29.1, lakini kuna suala la mchango wa kilimo katika ukuaji wa uchumi, ile asilimia Nne tuliyoitaja ambayo inaonekana ndiyo tulikuwanayo 2019 ilichangiwa sana na sekta ya kilimo ambayo kwa kipindi kile ilichangia kwa asilimia 26.1. Sasa kwenye kilimo kuna nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa sababu wewe ulitoa mwongozo kwenye bajeti iliyopita. Katika bajeti iliyopita ya trilioni 36 kwenye kilimo ilienda bilioni 294, it is less than 1%, wakati imeajiri directly zaidi ya asilimia 55 ya Watanzania, lakini kwenye mnyororo wake, usafirishaji, usindikaji, na adhalika ni asilimia 70 ya watu wameajiriwa pale, lakini tumewapa less than one percent ya bajeti yetu, hatuwezi kusonga mbele kwa namna hiyo. Kwa hiyo, ninashauri sana hata ikiwezekana bajeti ijayo hata asilimia 10 ikiwezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea umwagiliaji siyo vitu vya kutoka mbinguni. Bwawa la Nyumba ya Mungu limetengenezwa miaka ya 70, siyo ziwa ni bwawa lilitengenezwa na ni baada ya uhuru. Tunaweza kutengeneza mabwawa ya namna hiyo maeneo mbalimbali yakasaidia umwagiliaji pamoja na kilimo cha uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba bajeti ijayo iangalie sana hii sekta ya kilimo. Tungetamani yale maeneo ambayo yamefanyiwa research yanaonekana mazao fulani yanafaa tu-substitute, hawa vijana wa bodaboda, bodaboda inauzwa milioni mbili na laki tano, ukiangalia tukiweka maeneo ya ardhi yenye rutuba ambayo yana tija hawa vijana tunawahamishia kule wanalima na pato letu linaongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na sekta ya kilimo ni kwenye mifugo. Wafugaji wetu ni wafugaji wa kitamaduni, hawafugi kwa ajili ya kuuza kwa sababu, wao wanaamini wale ng’ombe ndiyo hela yao. Inahitajika elimu tujitoe hapo. Hapo Kongo soko la nyama lina thamani ya bilioni 70 kwa sasa au zaidi na wananunua nyama kutoka Belgium, Netherlands, Ujerumani, South Africa na India, lakini sisi hatuuzi nyama hapo na wako jirani tu. Tuwafunze wale wakulima wetu kwamba, hawa ng’ombe unaweza kuwaweka benki kwa kuwafuga vizuri, kwa kuzingatia njia za kisasa tukauza nyama tukapata hela za kigeni tena kuanzia hapa jirani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza Serikali, imefanya kazi kubwa sana kwenye sekta ya afya. Tatizo kubwa sasa baada ya kuboresha hospitali za Wilaya na kutengeneza vituo vya afya na hospitali za Mikoa ni watumishi na kila tukiuliza tunaambiwa kuna utaratibu unaitwa wage bill kwamba, hatuwezi kuajiri tena tusubiri. Sasa kama chanzo cha mapato hospitali za Kanda ziwezeshwe kwa sababu, tumeshaweka vifaa. Tuangalie namna ya kutumia wataalam hata kwa contracts siyo kwa kuwaajiri ili tuangalie soko la medical value tourism ambayo India mwaka 2020 walikuwa wanatabiriwa kuwa na kipato cha kama Nine billion dollars kutokana na watu wanaoingia pale kwa ajili ya kutibiwa, ikifika 2022 wanasema itakuwa na thamani ya 13 billion dollars. Kwa hiyo, hizi hospitali za Kanda tukishaimarisha hizi za chini zile tuziwekee utaratibu ambao tutaweza kuzitumia kama sehemu ya kipato nchi za jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa mfano ni rahisi mtu anayetoka Mombasa kutibiwa KCMC kwa distance na gharama kuliko kwenda Nairobi na imekuwa ikitokea hivyo hata katika level hii tuliyopo. Tukiangalia na Kanda nyingine za Mwanza na huko Kusini tunaweza tukaingiza hela kupitia kwenye medical value tourism. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo kingine cha mapato ni upimaji wa ardhi yetu. Ukishapima ardhi kinachofuata ni kodi. Ikiwezekana, ingewezekana tungepima nchi nzima kila mahali kuwe na hati, lakini mimi maeneo haya nina special interest, miji mingi ukiangalia tunafanya kazi sasa hivi ya kurasimisha makazi kwa sababu, hatukupima kule ambako Mji unapanukia kwa hiyo watu wakajenga kiholela. Tunarasimisha makazi ambayo siyo mazuri ni holela na hayawezi kuboreshwa kwa namna yoyote ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini miji yote katika fedha ambazo tutazipata karibuni tuweke vifaa kwenye Halmashauri au kila Mkoa vya kupima ardhi kila Mji unaonekana unakua kuelekea wapi, tupime maeneo yale, tutoe hati, watu walipe kodi, hicho ni chanzo cha mapato kizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kwa kukuza uchumi wetu. Miradi mikubwa yote wanapewa Wakandarasi wa kutoka nje, siyo jambo baya ni mahusiano, lakini ikumbukwe kwamba, wakishamaliza fedha kubwa au sehemu kubwa ya fedha ile inaenda nje. Sasa kama fedha tayari tunazo na tunaogopa kuwapa wakandarasi wetu tunaona kama hawatafanya vizuri, kwa nini tusitengeneze utaratibu ambao tutawasimamia vizuri zaidi fedha zile zibaki hapa? Hao mabilionea tunaongelea 5,000 wawe 10,000 keshokutwa wafike 1,000,000 kwa kuwasimamia vizuri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunakuwa na miradi mikubwa unaona hela yote inaenda kwa wakandarasi kutoka nje. Yaani kwa mfano sasa hivi hata hao mabilionea ukiwaita, nadhani ukiwaangalia wazawa hasa utaona ni wachache tu watakuwa hapo, lakini hawa waswahili wa kawaida…
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Priscus pokea Taarifa.
T A A R I F A
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa Taarifa mzungumzaji kwamba, anachosema ni kweli, mbaya zaidi tuna bodi…
MWENYEKITI: Anachokisema kipi?
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la kuwapa kazi kubwa wakandarasi wa nje, uhakika ni kwamba, tuna Bodi ambayo inasajili Wakandarasi wa ndani na tuna fedha nyingi Serikali inawalipa waajiriwa wa bodi ile, lakini tuna-entertain kufanya kazi kwa kutumia force account wakati tunajua value ya private sector katika nchi yoyote ya maendeleo duniani.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Priscus unapokea Taarifa hiyo?
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante kengele imeshalia. Mheshimiwa Priscus unadhani kuna mabilionea wangapi Moshi pale?
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ngumu kusema maana hatuna access ya kujua. (Kicheko)