Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalenga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia jioni ya leo hotuba nzuri sana ambayo imewasilishwa na Waziri wa Afya, dada yangu Mheshimiwa Ummy. Vile vile nakushukuru sana kwa sababu nafasi hii niliyopewa ni nyeti lakini vile vile ni nafasi ambayo inaenda kuonesha kwamba Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi imejipanga vipi kwa ajili ya masuala mazima ya afya katika kipindi kinachofuata cha mwaka mmoja. Kwa hiyo, napenda kuchukua nafasi hii kuweza kumshukuru sana Waziri wa Afya na msaidizi wake, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla. Nawashukuru sana kwa kazi nzuri mnazozifanya na sisi tuko nyuma yenu tukifanya kazi kwa ajili ya Taifa letu la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza tu, napenda kugusia masuala muhimu ambayo wenzangu wengi wameshayaongelea, masuala ya Mfuko wa Jamii. Tukitaka kuangalia kiundani suala la Mfuko huu wa Jamii (CHF), bado una changamoto, tena kubwa sana, lakini naamini kabisa kwamba bajeti hii itakwenda kutibu maeneo mengi ambayo Mfuko huu una matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, CHF kwa ujumla wake ukiangalia katika ile Act ya mwaka 2001 ya Community Health Fund utaona kwamba tatizo kubwa la CHF ni mpangilio na namna gani huduma hii muhimu inatolewa kwa wananchi. Katika kuangalia hilo, utagundua kwamba katika Act ya mwaka 2001, suala la walemavu bado halijawekewa mkazo katika CHF. Namaanisha kwamba katika utaratibu huu wa CHF kuhakikisha kwamba wananchi wanachangia pesa kwa ajili ya kupata huduma za afya, watu wenye ulemavu hawajapa nafasi katika kupatiwa exemption.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko huu haujaeleza ni namna gani ambavyo watu wenye ulemavu wanaweza wakapata huduma hii bure moja kwa moja kulinganisha na watu wenye uwezo au wale ambao wana uwezo wa kufanya kazi moja kwa moja ambao sio disabled. Kwa hiyo, Mfuko huu bado una changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiondoa hilo suala la walemavu, CHF bado utaona kwamba ina uhaba wa madawa. Watu wanachangia katika jamii, lakini madawa bado hayapatikani. Hii bado ni changamoto. Vile vile ukiangalia CHF pamoja na NHIF, statistic inaonesha kwamba mwaka 2012 ni asilimia 27 tu ya Watanzania wote ambao walikuwa wamejiunga na CHF pamoja na NHIF. Kwa hiyo, bado kuna idadi kubwa ya watu ambao aidha hawana elimu ya kutosha au imeonekana kwamba Mifuko hii bado haijawanufaisha wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Kalenga tatizo hili bado ni kubwa, nami nimejitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu kuongea na wananchi, lakini bado wananchi wanasuasua na bado hawana uhakika juu ya suala hili. Kwa hiyo, napenda sana kuona Serikali inakuja na mkakati maalum wa kuweza kuleta mabadiliko ili wananchi waweze kuwa na imani na Mfuko huu na Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo napenda kuchangia, ni tatizo kubwa katika Hospitali ya Ipamba pale Jimboni Kalenga. Jimbo la Kalenga lina watu zaidi ya 200,000 lakini vile vile hospitali ya Ipamba inahudumia Wilaya nzima, nikimaanisha Jimbo la Kalenga na Jimbo la Isimani ambalo ni la Mheshimiwa Lukuvi, lakini bado hatuna gari la wagonjwa. Hili ni tatizo kubwa. Napenda Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujumuisha, aweze kutoa majibu mahsusi ambayo yatakwenda kuwagusa wananchi wa Jimbo la Kalenga na Iringa Vijijini kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Iringa Vijijini kama Wilaya yenye watu zaidi ya 300,000, hakuna gari la wagonjwa katika hospitali kubwa kama Ipamba. Hospitali hii inahudumia wananchi mpaka wa Manispaa ya Iringa Mjini, lakini vile vile inahudumia wananchi wanaosogea mpaka maeneo ya Mafinga kwa ndugu yangu Chumi. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iweze kuangalia kwamba, akinamama ambao wanatoka maeneo ya milimani, maeneo ya mbali wanapata shida kubwa sana kuhakikisha kwamba wanafika katika hospitali kubwa kama Ipamba kupata huduma kwa sababu tu ya kutokuwa na gari la wagonjwa. Kwa hiyo, napenda sana Serikali iweze kuja na majibu muhimu kuweza kuhakikisha kwamba hospitali hii inapatiwa gari la wagonjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo moja kubwa ambalo nchi yetu ya Tanzania inalipata sasa hivi. Tuna tatizo moja katika masuala ya afya ya akili ya binadamu. Nchi yetu ya Tanzania kwa takwimu za haraka haraka inaonesha kwamba kuna watu zaidi ya 450,000 ambao wana matatizo ya afya ya akili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tatizo hili ni kubwa na statistic inaonesha kwamba miaka inavyozidi kuendelea kutakuwa kuna changamoto kubwa na watu wataendelea kupata matatizo haya kwa sababu mbalimbali hususan matumizi ya sigara, vile vile bangi, bila kusahau matatizo makubwa ya vileo. Kwa hiyo, napenda sana Serikali iweke umakini zaidi katika eneo hili kwa sababu idadi kubwa ya vijana au idadi kubwa ya watu wanaangamia kwa sababu ya kukosa elimu ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajaribu kugusia maeneo kadhaa. Hospitali yetu ya Milembe ambayo ndiyo hospitali kubwa ya Taifa ina changamoto kubwa. Leo hii hospitali ile inahudumia wagonjwa 250 mpaka 300 kwa siku, watu wenye matatizo ya afya ya akili. Tatizo hili bado ni kubwa katika nchi yetu ya Tanzania, ukienda pale utaona kwamba miundombinu haijakaa vizuri, utaona kwamba hakuna wahudumu wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile utaona kwamba, uwezo wenyewe wa hospitali katika kujiendesha nikiwa naamanisha masuala mazima ya kuletewa bajeti kwa muda hayafikiwi kwa muda. Kwa hiyo, unakuta hospitali inapata changamoto kubwa na inakosa namna ya kujiendesha yenyewe na hivyo basi, kuendelea kusuasua kuhakikisha kwamba ndugu zetu hawa wenye matatizo ya akili wanaweza kupata tiba kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kuona Serikali inakuja na majibu. Sehemu mojawapo ya kuweza kupata majibu haya ni kuhakikisha kwamba referrals zinatengenezwa, tunajenga vituo mbalimbali katika mikoa ili ndugu zetu hawa wasiweze moja kwa moja kutoka mikoani kuja Dodoma; kwa sababu kuna ndugu wanatoka Zanzibar, wanatoka Mwanza na Arusha wanakuja Dodoma kwa ajili ya huduma hii. Kwa hiyo, napenda referrals ziweze kutengenezwa, ziimarishwe katika mikoa yetu ili ndugu zetu wasiwe wanasafiri umbali mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ukiangalia utaona kuna wale ambao wanakaa majumbani. Wanapokaa majumbani wanahudumiwa na familia zingine zenye uwezo mdogo sana kifedha. Akinamama wanahangaika kuwahudumia watoto wao wenye matatizo ya akili, wanashindwa kupata nafasi ya kuweza kusafiri umbali mrefu kuwaleta Dodoma. Kwa hiyo, napenda sana hospitali hizi ziweze kuimarishwa kuhakikisha kwamba huduma hizi zinapatikana katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile napenda kuangalia masuala ya UKIMWI. Nyanda za Juu Kusini tunaongoza katika tatizo hili kubwa la HIV. Naomba Serikali iweze kuja na mikakati maalum, kuweza kuangalia Mkoa kama Njombe wenye zaidi ya 14%; Mkoa wa Iringa wenye zaidi ya 9% ya maambukizi, Mkoa wa Ruvuma, yote ni Nyanda za Juu Kusini, napenda mikakati maalum iweze kuwekwa ili tuweze kupata majibu, namna gani tunaweza kuzuia tatizo hili la maambukizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kuendelea zaidi, lakini napenda tu kuwasihi ndugu zangu wa upande wa pili kwamba tunavyochangia bajeti ya Serikali tuangalie kwa makini sana, kwa sababu Serikali inafanya kazi pande zote mbili. Ikiangalia masuala ya afya hakuna ambaye atasimama hapa na kusema kwamba hajatengenezewa mikakati maalum na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, napenda kumalizia kwa kusema kwamba, kama nitapata ruhusa yako nisome Mathayo 7:9 – 10 unasema hivi: “Au kuna mtu yupi kwenu ambaye mwanaye akimwomba mkate atampa jiwe; au samaki akampa mkate?”
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili nalisema kwa sababu kuna watu wako upande wa pili wanadhani Serikali haifanyi chochote. Serikali inawahudumia na nawaomba, kama wameshindwa kukaa upande wa pili, waje upande wetu, tutawaletea raha na hatutawaletea matatizo. Nawashukuru sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, nakushukuru sana.