Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Dr. Christina Christopher Mnzava

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia fursa hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Mapendekezo na Mwongozo wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kujikita katika maeneo mawili ambayo ninafikiria ni vizuri na mimi nikatoa mchango wangu, nipende kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia, kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha kwamba anatuletea maendeleo na kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hivi karibuni amekuwa akisafiri huku na huku kuhakikisha kwamba Watanzania tunaendelea kunufaika na mambo yote mazuri ambayo yako duniani, hasa katika suala zima la janga ambalo lilikuwa limetupata la UVIKO-19. Tumeona ni jinsi gani ambavyo ameweza kutafuta fedha na kupata zaidi ya trilioni 1.3 kwa ajili ya kupambana na UVIKO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hakuishia hapo, alifikiria mbele zaidi akaona fedha hizi ni vizuri kuzipeleka kule ambako ndiyo kuna chanzo cha tatizo. Zimekwenda kujenga shule, kupunguza msongamano, lakini zinakwenda kujenga vituo vya afya kuhakikisha kwamba huduma zote za kukabiliana na UVIKO-19 zinaimarika. Haitoshi, tunajua chanzo na njia moja wapo ya kujikinga na UVIKO ni kunawa mikono, ameimarisha mfumo mzima kupeleka fedha kwa ajili ya kupata maji safi na salama. Kwa hiyo, ninampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujikita katika suala zima la kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu. Uchumi bila viwanda haiwezekani, itakuwa ni ndoto. Ninapongeza sana Wizara kwa kuona kipengele hiki kuhakikisha kwamba inajenga uchumi shindani na maendeleo kwa watu. Lakini maendeleo kwa watu hayawezi yakaja kama viwanda vyetu nchini haviongezeki au vilivyopo havifanyi kazi kwa tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Shinyanga kuna kiwanda cha nyama kimejengwa mwaka 1951. Toka kilipojengwa hakijawahi kuzalisha hata kilo mbili za nyama, kina eneo kubwa sana la uwekezaji, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imekuwa ikijitahidi kuhakikisha kwamba inaomba lile eneo kwa ajili ya kutengeneza mazingira ya uwekezaji, kuwavutia wawekezaji wengine ambao wanahitaji kuja katika Mkoa ule kuwekeza ili waweze kupata ardhi na kuweza kujenga viwanda vingine au kuboresha kiwanda kilichopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo ni kwamba lile eneo la kiwanda cha nyama liko chini ya Wizara ya Mifugo pamoja na Wizara ya Fedha. Tumekuwa tuki-struggle sana tuweze kupata lile eneo ili wanapokuja wawekezaji Mkoa wa Shinyanga ardhi ipatikane bure, wenyewe waweze kujenga viwanda, waweze kulipa kodi, lakini waweze kuajiri vijana ambao ni vijana wengi sana hawana ajira sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imefanyika Kahama, kulikuwa kuna eneo Kahama linaitwa Zogomela, lina hekta zaidi ya 2,000. Halmashauri iliomba Wizara ya Mifugo – lilikuwa eneo la Wizara ya Mifugo, likatolewa kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, wameweza kuweka uwekezaji. Sasa hivi mwekezaji anapofika Tanzania akitaka kuja kuwekeza katika baadhi ya Halmashauri ambazo zina fursa ya kuwekeza moja wapo ni Kahama, mwekezaji anapewa ardhi, anajenga kiwanda, analipa kodi zote za Serikali za ardhi na kadhalika lakini anazalisha ajira nyingi kwa wazawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Wizara ya Mifugo na Wizara ya Fedha zisitoe lile eneo ambalo liko Tanganyika Packers pale Shinyanga na eneo lingine la Chibe ambalo lina zaidi ya hekta 8,000, limekaa tu halina kazi, Wawekezaji wanapokuja wakitaka ardhi kwenda kulipa fidia kwa wananchi wa kawaida inakuwa ni gharama kubwa sana. Anaangalia mkoa mwingine ambao una fursa ya ardhi ambayo haina masharti makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ninaomba katika suala zima la kutaka kuhakikisha kwamba uwekezaji wa viwanda kwa maendeleo ya watu tuangalie na maeneo ambayo tuna ardhi kubwa, iko chini ya Serikali, wawekezaji wanakuja wanahitaji kupata lile eneo ili waweze kuwekeza, basi kusiwe na milolongo mingi ya kuweza kutoa lile eneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuzungumzia kuhusu suala zima la kilimo. Kila Mbunge anayesimama hapa anaongea kuhusu suala la kilimo, na wengine wataendelea kuchangia sekta ya kilimo kwa sababu ndiyo uti wa mgongo. Suala zima la kilimo tumeona kabisa kwamba katika mpango huu sekta ya kilimo inachangia Pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 26, lakini huu ni ule ulimaji wa kawaida wa kutegemea mvua, na tumeshaambiwa kabisa mwaka huu mvua zinaweza zikawa siyo nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali Tanzania tunajipangaje kwa mpango wa muda mrefu kuhakikisha kwamba nasi tunabadilika kama nchi ya Israel ilivyobadilika, kama jinsi ambavyo Dubai imebadilika. Nchi zile ni majangwa lakini wameweza kuhakikisha kwamba wanaboresha kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huku kwenu Kongwa huku, kipindi cha masika kuna maji yanapotea hovyo, ukishavuka sehemu moja ya Chamwino huku kama unakwenda Dar es Salaam masika maji yanajaa sana mpaka magari yanachukuliwa na maji.

Ukienda Bahi Road huku kama unakwenda Shinyanga kuna eneo pale la Bahi, maji yanajaa mpaka yanapotea, Serikali ije na mpango wa kuhakikisha kwamba na sisi tufike hatua Tanzania tuweze kuvuna maji. Mbona nchi nyingine wameweza? Hawakuanza mara moja, ni mpango wa muda mrefu, ni ambao unatumia fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tufikirie sasa kwamba kwa miaka ijayo tuhakikishe kwamba tunatafuta fedha za kuweza kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji ili sasa tutoke pale kwenye Pato la Taifa la asilimia 26 tuweze kwenda juu. Tumeona kabisa kwamba kuna uhitaji lakini mbali na suala zima la umwagiliaji bado kuna tatizo la bei kubwa za pembejeo.

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)