Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BALOZI DKT. PINDI H. CHANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naanza na pongezi kwa Rais wetu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, kumshukuru sana Waziri na Baraza zima la Mawaziri kwa kutuletea mapendekezo haya ya Mpango na vile vile naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Njombe, kwa kweli wanatoa shukrani nyingi sana kwa mambo mengi makubwa ambayo Serikali hii imekuwa ikiyafanya, hususan suala zima la ununuzi wa mahindi na kuboresha upande wa kilimo. Wananchi hawa pamoja na shukrani hizi, jana na juzi nimekuwa naongea nao wa Makete, Ludewa, Wanging’ombe, Njombe Mjini, Lupembe, Makambako, wanasema Mheshimiwa pamoja na mambo mazuri haya, hivi kwa nini bei ya mbolea ipo juu? Nikawa nawaelezea kwamba mbolea hii inaagizwa kutoka nje. Wakasema bee Mheshimiwa, yaani mpaka leo tangu Uhuru karibia tunakwenda miaka 60 ya Uhuru bado tunaagizaga tu mbolea Nje! Kwa nini tusizalishe wenyewe mbolea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mjumbe hauawi, nafikisha. Wananchi wanauliza, lini tutazalisha mbolea ya kujitosheleza? Wanasema siyo tu mbolea, zana zote za kilimo; iwe ni majembe, power tiller, iwe ni trekta, wakati umefika sasa Tanzania tuzalishe bidhaa zetu. Maana asilimia 60 tumejikita kwenye kilimo, sasa utaratibu huu wa kuagiza zana za kilimo nje watakuwa wanatupangia bei na tutakuwa tunaendelea kusema bei imekuwa kubwa, bei imekuwa kubwa. wa kweli tuzalishe zana zetu za kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyo viwanda mbalimbali vya mbolea. Tukae nao tuwaambie, mahitaji ni haya, sasa hapa tunasaidiana vipi wazalishe mbolea ya kupandia, mbolea ya kukuzia ya kutosheleza? Kwa hiyo, naomba nilete salamu hizi kutoka Mkoa wa Hunzombe, wanaomba sana hili suala la mbolea tuone jinsi ya kuzalisha na litosheleze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na taadhima niendelee kumpongeza sana Rais wetu, Mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassan. Upande wa Diplomasia, ziara za Mheshimiwa Rais zimeijengea heshima sana nchi yetu. Mheshimiwa Rais amefanya ziara katika Mkutano ule wa United Nations General Assembly na alihutubia pale Marekani na vile vile Mkutano wa Cop 26. Mikutano hii, imekuwa inazaa matunda mengi sana. Tanzania tunaendelea kuwa kwenye ramani ya Kimataifa, kwa kweli niendelee kushukuru sana, ziara hizi zinasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mapendekezo haya ya Mpango tumeona kwamba baadhi ya Balozi zimeendelea kufunguliwa na last time wakati nachangia niliomba sana tuendelee kufungua Balozi pale Vienna tumefungua, tumefungua pia pale China, Guangzhou na maeneo mengine.
Sasa wakati ni huu wa kuendelea kufungua Balozi. Tuendelee kuwaalika nchi nyingine pia waje wafungue Balozi hapa Tanzania na kutokea Tanzania waendelee kuhudumia nchi za SADC na Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mchuchuma na Liganga kwa kweli ni la kulitia maanani. Wengi wamesema, lakini hivi karibuni tumeanza kupeleka Makaa ya Mawe India. Ninaipongeza sana Serikali kwa kuanza kupeleka Makaa ya Mawe India kupitia Bandari yetu ya Mtwara. Nasi wananchi wa Njombe, Ludewa tunasema na Ludewa Makaa ya Mawe tuone jinsi gani ya kuendelea kuyakuchukua na kuendelea ku-export, na ule mradi uendelee kuwekewa vipaumbele vya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, salamu nyingine kutoka Njombe hususan wanawake, wanashukuru vifo vya vya akina mama wajawazito na watoto vimeendelea kupungua. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. BALOZI DKT. PINDI H. CHANA: Kengele bado eeh!
MWENYEKITI: Malizia dakika moja.
MHE. BALOZI DKT. PINDI H. CHANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa hiyo, wanaomba Bima kwa wote, wanapiga na magoti. Bima kwa wote itaongeza muda wa maisha, lifespan ya Watanzania. Bima kwa wote itasaidia, tutakuwa tuna afya nzuri, kwa hiyo, tutachapa kazi zaidi. Ofisi yangu pale Njombe nimeanza pilot kuwakatia akina mama Bima. Wanaishukuru sana Serikali, wanashukuru Bunge kwa kupitisha Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe mwenyewe wamekushukuru sana, wanaomba uje kule Njombe ufanye ziara ukiwa kama Spika kuangalia utekelezaji wa sheria mbalimbali zinazotungwa na Bunge. Kwa hiyo, wanaulizia Sheria ya Afya kwa Wote (Universal Health Care) inakuja lini? Kwa hiyo, mpango huu ukizingatia, tutashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)