Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia jioni hii ya leo. Kwanza kabisa, nami niungane na wengine wote ambao wametoa pongezi nyingi sana kwa mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu, Rais wetu ambaye kwa kweli amefanya mambo mengi sana makubwa na mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna usemi unasema kwamba mzigo mzito umpe Mnyamwezi, lakini kwa kazi nzuri mama anayoifanya, inaonesha kwamba sasa tubadilike, tuseme kwamba mzigo mzito mpe mwanamke na wanawake tumekuwa tukibeba mizigo mizito sana na ninyi akina baba mnajua kwamba mizigo mizito huwa haitushindi. Tuna imani kabisa mama hatashindwa. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitoe pongezi...

MWENYEKITI: Nilisikia kuna taarifa upande huu. Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, endelea na mchango wako. (Makofi/Kicheko)

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawe ni lazima uunge mkono kwamba wanawake huwa hatushindwi, mizigo mizito yote huwa tunaiweza. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Naibu wake na Watendaji wote wa Wizara kwa kutuletea Mpango ili tuweze kuujadili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitakuwa sijatenda haki kama nisipompongeza Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Bajeti Mheshimiwa Dkt. Sillo na Wajumbe wote wa Kamati ya Bajeti, kwa kweli wametufafanulia vizuri sana huu Mpango na ndiyo maana tumeweza kuuchangia vizuri. Nawapongeza sana kwa kazi nzuri, wala hawakufanya kosa kuwachagua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kwa kweli niungane na wote, nianze mchango wangu kwa kuchangia Sekta ya Kilimo. Sekta ya Kilimo kama ambavyo imesemwa kwamba Watanzania zaidi ya asilimia 65 ni wakulima. Vilevile Sekta ya Kilimo inatoa ajira karibu asilimia 66.3; pia inachangia katika viwanda asilimia 60; na pato la Taifa ni asilimia 26. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niungane na Wajumbe wote kwamba bado kabisa Wizara ya Kilimo haijaweza kupewa kipaumbele cha kutosha. Bajeti ya Wizara ya Kilimo ni ndogo sana. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Kilimo. Siku zote tumekuwa tukilalamikia Bajeti ya Wizara ya Kilimo.

Tunao Mawaziri wazuri sana tu katika Wizara ya Kilimo; ni wazuri sana kwa sababu tunafanya nao kazi, lakini katika Kamati yetu ya Kilimo tunao wabobezi wazuri sana. Tuna Wajumbe wazuri ambao siku zote wamekuwa wakitoa michango yao, tumekuwa tukitoa michango yetu pale, tumekuwa tukitoa hoja zetu, tumetoa ushauri mzuri kuhakikisha kwamba kilimo chetu kiwe na tija, lakini je, hii michango, huu ushauri unachukuliwa wakati gani na kufanyiwa kazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tumeona Mpango umekuja, lakini mambo mazuri ambayo tumeishauri Serikali yetu, bado hatujaona kama yamechukuliwa katika huu Mpango. Sasa nilikuwa naomba kuwepo basi na mkakati tuone yale tuliyoyashauri yamefanyiwa kazi kiasi gani? Yametekeleza kiasi gani? Kwa nini hayatekelezeki? Nini tufanye ili tuwe na mipango mizuri kuhakikisha kwamba kilimo kinaweza kuisaidia nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima nchini kwa kweli wamekuwa wakilima tu kilimo cha mazoea. Wakulima wetu wanalia, wakulima wetu wamekuwa wanafanya kazi kubwa, lakini hamna wanachokipata. Watu wanajuta hata kuwa wakulima. Ili kilimo chetu sasa kiwe na tija, tunahitaji tuwe na Mpango mzuri. Tuhakikishe tunakuwa na Maafisa Ugani. Tunaona wakulima wengi wanalima bila kuwa na elimu ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukienda mkoa wetu wa Iringa unaona hata kusafisha mashamba wanachoma. Leo Iringa wanalia, misitu imeungua; ukienda Kilolo au Mufindi, sasa hivi tumeunguza mashamba mengi kwa sababu wakulima hawana elimu ya kutosha kuhakikisha kwamba wanasafisha hata mashamba tu kwa utaalamu. Vilevile wanalima kilimo ambacho hakina tija kwa sababu wanafundishana wao wenyewe. Kuna shortage kubwa sana ya Maafisa Ugani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuwepo na ruzuku katika pembejeo. Ukifanya ziara sasa hivi tatizo kubwa ni bei kubwa ya mbolea. Wananchi sasa hivi wameanza kuandaa mashamba, bado mbolea iko bei juu sana, hawajui wafanye nini. Naomba ruzuku ya pembejeo ni muhimu sana tupate mbolea, bei iwe chini, lakini pia hata mbegu bora ziwe bei ya chini kabisa ili wakulima wetu waweze kulima kilimo chenye uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuwepo na uzalishaji wa mbegu bora, lakini vilevile masoko ni tatizo kubwa sana kwenye nchi yetu. Wakulima wanalima mazao mengi lakini hawana uhakika wa soko la kesho litakuwaje, wanakuwa wanalima kwa hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba vilevile ujenzi wa vihenge pamoja na maghala, ni muhimu sana. Sasa hivi wakulima wengi hawana sehemu za kuhifadhia mazao yao, changamoto ni hiyo sasa mazao hayo yanashambuliwa na wadudu. Tumpongeze sana Mheshimiwa Rais, alikuwa ametoa zile bilioni 100 kwa ajili ya soko la mahindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, unaona kutokana na kutokuwa na maghala sehemu ambayo wakulima wapo wameshindwa kwenda kuuza yale mahindi kwa sababu ukiangalia gharama ya kupeleka yale mahindi sehemu ya kununulia yale mazao, ni mbali na ni ghali, kiasi kwamba bado hawajafaidika, waliofaidika ni madalali ambao wao wanachukua mahindi wanayapeleka kwenda kuyauza kule kunakotakiwa kununuliwa yale mahindi. Kwa hiyo niombe maghala ikiwezekana yawepo kila kata ili kusaidia wakulima kupata urahisi wa kuhifadhi mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, wakulima hawakopesheki benki; benki zetu haziwakopeshi wakulima. Kwa sababu tunayo Benki ya Kilimo tulitegemea sasa hii benki ingekuwa msaada kwa wakulima, wangepewa ruzuku ya kutosha ili wakulima wakope kwa riba nafuu, lakini benki hii bado hatujajua sasa imekuja kumsaidia mkulima au imekuja kufanya biashara, kwa sababu bado riba iko juu sana. Kwa hiyo, naomba uwepo mpango mkakati kuhakikisha wakulima wetu wanakopesheka ili waweze kulima kilimo chenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nizungumzie kuhusu jitihada ya Serikali kulipa madeni ya wazabuni, lakini vilevile hata wazabuni wa pembejeo wengi bado wanadai. Nilitegemea hawa wazabuni wangelipwa kwa wakati ili waweze kuleta sasa hizo pembejeo kwa wakati na ziweze kufikia wakulima kwa wakati. Hata hivyo, wazabuni mpaka leo hii bado wanadai madeni makubwa, wanashindwa kwenda kununua hizo pembejeo, kuwasogezea wakulima ili waweze kulima kwa wakati. Misimu inakuja bado ukienda kuwaona wale wa pembejeo wanasema bado wanadai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uwepo mkakati madhubuti wa kuhakikisha kwamba wazabuni hawa wanalipwa. Wengi wao wamechukua mikopo benki, wengi wao wanatishiwa kuuziwa mpaka mali zao. Sasa naomba kwa kweli wazabuni wa pembejeo wapatiwe pesa zao kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mfano kuhusiana na mkulima wa nyanya, kwa sababu hata mimi ni mkulima wa nyanya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele ya pili Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati.

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)