Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia. Kwanza kabisa naomba kumpongeza Mheshimiwa Waziri, dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu Waziri wake, Mheshimiwa Kigwangalla kwa hotuba yao nzuri na kwa kazi nzuri ambazo wanakuwa wakiwafanyia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujielekeza moja kwa moja katika mchango wangu. Kwanza kabisa naomba kuzungumzia Bima ya Afya, nazungumzia Bima ya Afya kwa vijana wajasiriamali. Vijana ambao wanafanya kazi kwenye maofisi huwa wanawekewa ulazima wa kukatwa asilimia fulani katika mishahara yao ambayo inawapelekea kupata Bima ya Afya; lakini kwa vijana wajasiriamali hakuna kitu kama hiki, ni baadhi ambao wanakuwa na uelewa au wanakuwa na mwamko wa kujua nini faida ya Bima ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia nguvu kazi ya Tanzania ni vijana na wanaofanya kazi ni takriban milioni 23 ya Watanzania. Wajasiriamali ninaowazungumzia hapa ni wale madereva wa bodaboda, mama lishe, fundi ujenzi, mafundi vyerehani, ndiyo ninaowazungumzia hapa. Wengi hawajajiunga na Mifuko au Bima za Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kuzungumzia ni kwamba, naiomba Wizara iiombe Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ishuke chini kwa hawa vijana wajasiriamali, itoe elimu kubwa kuhusiana na Bima ya Afya, iwaambie faida ya Bima ya Afya ni nini? Leo dereva wa boda boda ukimwambia achange sh. 50,000/= kila mwezi anaona pesa yake inapotea, haelewi umuhimu ni nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Mifuko yetu ya hifadhi ikishuka chini kwa hawa vijana wajasiriamali ikawaelezea umuhimu, ikawaambia kwamba unapojiunga na Mfuko wa Hifadhi, automatically unapata Bima ya Afya, NHIF.
Hii itakuwa ni rahisi zaidi kwa wao kuelewa tofauti na kumwambia yeye achange kila mwezi sh. 50,000/= au sh. 100,000/= na kadhalika, inakuwa ni ngumu. (Makofi)
Ndugu zangu, tuelewe tu, tuwawezeshe wajasiriamali waelewe kwa sababu kijana wa leo mjasiriamali anapoumwa anapokwenda hospitali ndipo mtaji wake unapomalizika. Dereva boda boda anapata ajali, anavunjika mguu, anaambiwa kutibiwa kwake ni shilingi milioni tatu, nne mpaka tano, huo ndiyo mtaji wake aliutafuta kwa miezi kadhaa. Anapokuwa na Bima ya Afya inamsaidia yeye kupata matibabu bila kuumiza ule mtaji ambao alikuwa ameuweka kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ninalotaka kuzungumzia ni mimba za utotoni. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri kataja baadhi ya mikoa kama sita, kataja Mkoa wa Mara, Shinyanga, Geita, Singida na Dodoma kwamba ndiyo imeathirika kwa kiasi kikubwa na mimba ya utotoni. Naomba kumwambia dada yangu na kaka yangu, mimba za utotoni zimeathiri karibu Tanzania nzima. Suala hili lipo katika kila mkoa, linawagusa watu wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna adhabu zimekuwa zikitolewa kwamba ukimpa mimba mtoto wa kuanzia mwaka mmoja mpaka miaka nane, unafungwa maisha.
(Hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walinong’ona)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia tisa mpaka kuendelea chini ya miaka 18, wengine wanaichukulia kama ubakaji wanasema au mapenzi. Unamkuta baba mwenye umri wa miaka 35, 40, 43 au 50 anakuja kumshawishi binti mdogo mwenye umri wa miaka 15, anampatia ujauzito. Kwa maisha yetu ya kawaida binti mwenye miaka 15 anakuwa bado ni mwanafunzi, kwa hiyo, anamwachisha shule kwa ajili ya ule ujauzito. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba adhabu kali itumike kukabiliana na hawa akinabab. Mara nyingi unamkuta mtu mwenye miaka 45, ni mfanyakazi TRA, ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, lakini anamharibia maisha huyu binti mwenye miaka kumi na tano. Tunajuaje huyu binti leo angekuwa Waziri kama dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu? Baadaye huko, tunajuaje labda leo angekuwa Makamu wa Rais kama Mheshimiwa Samia Suluhu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naomba sana Wizara ya Afya ifikirie ni adhabu gani au mkakati gani itakuja nao kuweza kuwadhibiti hawa akina baba wanaotuharibia watoto wetu wadogo ambao hawajamaliza masomo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine na suala langu la mwisho, nataka kuzungumzia madawa ya kulevya. Tanzania yetu nikizungumzia Mkoa wa Dar es Salaam; kituo kinachotoa dawa kwa ambao wameathirika na madawa ya kulevya, ni Mwananyamala pekee. Hakuna kituo kingine! Ukienda pale Mwananyamala utalia, utasikitika, utawaonea huruma. Kama Mkoa wa Dar es Salaam ndiyo mkoa mkubwa ambao unaathirika; ndiyo kuna waathirika wakubwa wa madawa ya kulevya. Kuna kituo kimoja ambacho ndiyo cha Mwananyamala, foleni ni ya kufa mtu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba Wizara ione itafanyaje kuunda mfumo katika kila Kanda kuweka hivi vituo vya kutoa huduma za hawa walioathirika na madawa ya kulevya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hiyo tu, naomba Wizara ije na mfumo wa Rehabilitation Centers kwa hawa ambao wameathirika na madawa ya kulevya. Siyo madawa ya kulevya tu, kuna wagonjwa wa akili, wavutaji sigara ambao ni walevi kupitiliza. Mtu mwenye madawa ya kulevya leo, anaenda Mwananyamala, anapewa pesa, anarudi Mtaani. Atarudi kila siku Mwananyamala kuomba pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutafute hizi rehabilitation ambazo mtu anakuwa anahudumiwa, akitoka pale anapelekwa kule anakaa kwa kipindi fulani, akija kutoka tayari ameshaachana na kile kitu ambacho kilikuwa kikimsumbua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile naomba Wizara itoe mwamko kwa hizi rehabilitation centers za watu binafsi. Kuna moja ipo Bagamoyo ambako amepelekwa Chid Benz, kuna moja ambayo ipo Kigamboni; basi tuwashike mkono, tuwatie moyo, tuweze kuwaongezea ili wawasaidie vijana wetu. Kama sisi wenyewe tumeshindwa kuanzisha, wamepatikana watu kama hao, wana moyo wa kusaidia vijana, tuwashike mkono, tuwape msaada waweze kuwasaidia vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri suala la madawa ya kulevya analifahamu, linaumiza sana vijana, linaumiza nguvu kazi ya Taifa na wote tunatambua kwamba vijana ni nguvu kazi ya Taifa. Naomba litiliwe sana mkazo, atakapokuja kutoa hitimisho lake na useme nia yenu ama mfumo wenu ni upi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache, nakushukuru na naunga mkono hoja.