Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi na mimi niweze kuchangia taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza Kamati ya Sheria Ndogo kwa kazi ambayo wameifanya na kutuletea taarifa ambayo kweli inaoneka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa sheria ambazo zinawakuta wananchi moja kwa moja hasa wa kule chini ni Sheria Ndogo. Kazi ya Bunge ni kutunga sheria na baada ya kutunga sheria kabla haijaanza kutumika zinatungwa kanuni na hapo ndipo kumekuwa na shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa mjumbe wa Kamati kwa Bunge lililopita Kamati ya Sheria Ndogo kulikuwa na makosa mengi sana yakiwepo ya uchapaji, kulikuwa na makosa ya uandishi wa sheria. Lakini nimpongeze kipekee Mheshimiwa Jenista alichukua hatua kubwa sana, lakini katika mambo ambayo tumekuwa tunashauri kila wakati ni pamoja na semina elekezi kwa wanasheria wetu wa halmashauri na hili jambo bado Mheshimiwa Waziri halijafanyika ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili ugundue kwamba kuna shida bado kumekuwa kuna tatizo aidha la uwezo mdogo wa wanasheria wetu kwenye halmashauri inafikia mahali yaani mtu anachukua sheria ya Tabora anaipeleka Nkasi ya Nkasi anapeleka Kalambo yaani imekuwa ni ku-copy na ku-paste hawana tena muda wa kufanya research. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna haja sasa ya kutokuwa na haraka ya kutunga kanuni zetu tuwape muda wa kutosha wakafanye tafiti kuangalia uhalisia kabla hawajatunga kanuni zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili sheria itungwe kunakuwa kuna uhitaji sasa sasa hivi kumekuwa na shida kidogo ukizungumzia ukusanyaji wa mapato kila mtu anataka aonekane amefanya vizuri na hapo ndipo shida inapoanzia. Zinatungwa sheria ambazo ni kandamizi zinaenda kuwakandamiza wananchi ili mradi tu mtu aweze kukusanya vizuri kuna haja ya kufanya utafiti wa kina kwenye hizi sheria zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Sheria za Ushuru, miongoni mwa Sheria ambazo ni kero kwa watanzania tena wananchi wa kawaida ni Sheria za Ushuru, Tozo pamoja na Ada. Kuna haja ya kupitia eneo hili tuliangalie upya, lakini sheria nyingine ni Sheria za Wavuvi. Nilikuwa najiuliza hivi kuna wakati tunatunga hizi kanuni kumfurahisha nani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumza wavuvi kwa mfano haya maziwa mawili tu; Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika ukitazama Ziwa Tanganyika kuna nchi zaidi ya moja wanaotumia kwa ajili ya uvuvi hilo Ziwa Tanganyika, lakini tunatunga sheria za kuwaumiza wavuvi wetu halafu wavuvi wengine ziweze kuwanufaisha kwenye nchi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuachane na mfumo wa kufikiri sheria za kikoloni kama tunataka kukusanya mapato, kama tunataka tuongeze pato la Taifa kwenye uvuvi lazima tutengeneze mazingira rafiki kwa wavuvi ni pamoja na sheria zetu ambazo zitawasaidia wavuvi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kanuni ambazo ni za ajabu nani za hovyo za mwaka 2009 zimeletwa hapa baadhi tunashukuru Mheshimiwa Waziri amechukua hatua kwa baadhi ya kanuni kuziondoa na kutolea matamko na nini. Lakini matamko haya kama hayatawekewa msingi hayana maana yeyote. Shida ipo kule kwenye utendaji kwa mfano kama waliokuwa wanatunga kanuni walifanya research kwenye Ziwa Victoria ukapeleka hizo kanuni ziende Ziwa Tanganyika ni kwenda kuwandamiza wavuvi wa Ziwa Tanganyika ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo, kuna haja kabla hatujatunga kanuni zetu wao wanapewa muda wa kwenda kuangalia mazingira halisi kabla ya kutunga kanuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hili suala litakwenda vizuri hasa kabla hatujatunga tukiwashirikisha wadau, wahusika wa hiyo kanuni inayokwenda kuitunga kumekuwa na shida ya ushirikishwaji. Ukimshirikisha mtu siku moja mtu anayetoka Nkasi, anayetoka Kigoma si rahisi kuja Dodoma hapa kutoa maoni yake tutoe muda wa kutosha ili tuwashirikishe na wale wakitoa maoni yao maana yake nini, utekelezaji wake wa hiyo sheria inakuwa ni rahisi kwa sababu wameshiriki kikamilifu, wameshiriki kutoa maoni yao kulingana na uhalisia wa mazingira ambayo wanatoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna dosari za uandishi wa sheria, kabla sheria haijafika mwisho kuna hatua kadhaa. Sasa mpaka inakuja kuonekana mwishoni kazi ya kamati hii si kwenda kuangalia makosa ya kiuandishi si kazi yake Kamati ya Sheria Ndogo. Lakini saa hizi wamekuwa wanatumia muda mwingi kuangalia makosa yaliyopo kwenye Sheria wakati wapo watu ambao hizi sheria zimepita mikononi mwao. Lazima tuangalie tatizo lipo wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwenye Sheria hizi ukiangalia tunajikita zaidi kwenye kuweka adhabu kwenye Sheria Ndogo kwa nini tunajikita kwenye adhabu? Na imekuwa shida sana ya uandaaji wa hizi kanuni tunajikita zaidi kwenye kuweka adhabu kwenye Sheria Ndogo kwanini tunajikita kwenye adhabu, na imekuwa ni shida ya uandaaji wa hizi kanuni, tunajikita zaidi kwenye kwenda kukusanya na adhabu kwa mwananchi. Lakini hakuna sehemu ya uwajibikaji wa Serikali wanapokuwa wanatunga hizo sheria lazima tubadilishe fikra zetu tunapokuwa tunatunga hizo kanuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie zaidi Sheria kukiuka haki za binadamu hizi kanuni. Sheria yeyote inapokiuka haki za binadamu au kukiuka Katiba kwa maana Sheria Mama inakosa sifa ya kutumika. Lakini huko vijijini wananchi wetu wanaumia sana unakuta Sheria au Kanuni bado haijawa Gazetted imeanza kutumika na imeanza kuadhibu wananchi. Nani anawajibika kwenye jambo hilo si wananchi wote wanaweza kujua kwamba hii bado haina sifa ya kutumika hii sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Jenista amejitahidi makosa yale ya mwaka 2016 mpaka sasa tayari Sheria zile ambazo zimekuwa zimefuata utaratibu zinakuwa gazetted na analeta ndani ya Bunge mambo ambayo yanakuwa yanaeleweka unapokwenda huko unakuwa unajua kwamba hiki ni sawa hiki hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado kwenye suala la uwajibikaji linahitajika kwa sababu anapoumizwa mwananchi wa kawaida kwa makosa ya uandishi, kwa makosa ya sheria kutokuwa gazetted, lazima Serikali ianze kuwajibika kwenye mambo hayo. Na ili wawajibike lazima wawe wanapitia kule chini kwenye halmashauri waone mazingira yalivyo, lakini jaribuni kuangalia kweli uwezo wa wanasheria wetu kwenye halmashauri unajitosheleza? Hapo bado kuna shida kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nilijikita kwenye ushauri nakushukuru kwa nafasi. Ahsante. (Makofi)