Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009

Hon. Amb. Dr. Pindi Hazara Chana

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009

MHE. BALOZI DKT. PINDI H. CHANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nianze kwa kupongeza Kamati kwa uchambuzi wa taarifa yao ambayo imesomwa hapa leo. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana kwa kazi nzuri ya kusimamia masuala haya ya sheria ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kabla ya kuchangia nilikuwa naongea na wananchi wangu, nikawaambia kule Njombe nakwenda kuchangia masuala ya by-laws. Sasa wakaniuliza sisi watu wa Makambako, Makete, Njombe, Ludewa, Lupemba hizo by-laws, yaani unaposema kwamba zinapaswa kuwa gazetted, hizo Government Gazettes tunazipata wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikiwa kama mwakilishi wa wananchi naomba nililete swali hili; wananchi wa kule Ludewa na maeneo mengine, hizi Government Gazettes wakitaka kuziona, ku-access wanazipataje? Maana zinatolewa kwa Government Printers, labda zinapelekwa halmashauri; je, kule ngazi ya chini, siku hizi tumeshasomesha, Bodi ya Mikopo inatoa watoto wengi, wasomi wengi, sasa wakitaka kuziona wanazipataje? Kwa hiyo nitashukuru nikipata maelekezo, wananchi wakitaka kuzisoma zinapatikanaje kwenye ngazi ya chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli napongeza sana hizi sheria ndogo, zina faida sana; kudhibiti magonjwa mbalimbali, mambo ya kipindipindu, kutotupa taka ovyo, ukataji miti; kwa hiyo hizi sheria ndogo zina manufaa makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo naomba kusisitiza tu ni suala zima la ushirikishwaji wa wananchi. Tunapowashirikisha wananchi, kwa mfano, tunasema tusikate miti ovyo, kutakuwa na jangwa; tusitupe taka ovyo, kutakuwa na kipindupindu, kwanza tuwape uelewa, tukishawapa uelewa ile awareness creation wao wenyewe watatusaidia kuelimisha jamii na watoto na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipowapa uelewa, ukamwambia mwananchi usikate miti, atakuuliza sasa nitapata wapi kuni za kupikia na huku vijijini; Ludewa, Makete, tunatumia kuni? Bado masuala mengine ya umeme na gesi baadhi ya vijiji hatujaboresha kupata gesi na umeme kwa sasa, viko kwenye mpango. Kwa hiyo ni muhimu sana kutoa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yale makatazo yote, by-laws zinazohusu kuacha kutupa taka ovyo, lazima tumwambie mwananchi usitupe taka, dampo hili hapa, au ukitaka kutupa taka dustbin hili hapa, lakini tukiwa tunasema tu labda usitupe taka, lakini hatuwaoneshi mbadala; usikate miti lakini hatumwoneshi kuni atachukua wapi; hayo ni maeneo ambayo ninaomba tuone namna ya kuboresha.

Kwa hiyo ushirikishwaji una faida na wao wenyewe wataendelea kuhubiri hiyo Injili kwa jamii, kwamba hapana, ni marufuku kutupa taka, ni marufuku kukata miti na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kuhusu suala zima la kupishana ambalo Kamati imeelezea vizuri, wakati mwingine sheria ndogo inapishana na ile sheria mama. Unakuta wakati mwingine sheria mama labda inasema faini isizidi laki moja na kifungo labda cha miezi sita, lakini sheria ndogo inaweza ikasema faini isizidi laki moja na nusu, kumbe sheria kubwa yenyewe inasema faini isizidi laki moja na ile ndogo imekwenda zaidi. Kwa hiyo hilo ni eneo ambalo ni muhimu tukaliangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kupongeza maeneo yote wanakotunga sheria ndogo, Serikali za Mitaa (Local Government) wanafanya vizuri sana na kwa kweli sheria hizi zina manufaa sana kwa wananchi wetu. Kwa sababu inategemea na culture ya hilo eneo, inategemea na jiografia ya hilo eneo. Kwa hiyo zile sheria ndogo zinasaidia kuratibu eneo hilo husika kutokana na jinsi wananchi wanavyoishi katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kuhusiana na suala zima la muda. Wakati tunapitisha hizo sheria, kwa kawaida, tuchukulie mfano za halmashauri zinapaswa kwenda mkoani na baada ya mkoani kwa kweli zinaenda ngazi ya Taifa. Kwa hiyo, wakati mwingine zikifika pale mkoani ninaweka ombi tu kwamba zisikawie, ule uchambuzi na kupitishwa. Kwa sababu zinapochelewa unakuta sasa utekelezaji wa hiyo sheria pia unaweza ukacheleweshwa. Kwa hiyo, niombe sana, zinapotoka halmashauri zinapokwenda mkoani, zisicheleweshwe, zikienda TAMISEMI pia zisicheleweshwe, zipate kurudi kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nichangie maeneo hayo ambayo nimeya-table na nitashukuru kupata majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja. Ahsante. (Makofi)