Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwanga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii. Awali ya yote niipongeze sana Kamati, kwa kweli taarifa ya Kamati ni nzuri sana, imeturahisishia kazi na imetufungulia vizuri jinsi ya kuchangia. Kamati imefanya kazi nzuri, tunaipongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo napenda kusema ni kwamba sheria ndogo ni sheria kama sheria nyingine. Kwa bahati zenyewe zinagusa zaidi maisha ya kila siku ya wananchi. Kwa hiyo tunapozungumzia juu ya utungaji wa sheria ndogo nadhani tunahitaji kuwa makini sana kwa sababu zina umuhimu kwa vile zinagusa maisha ya kila siku ya wananchi. Kwa hiyo hata tunapozungumza suala la utawala wa sheria, ambayo katika hiyo pia nataka kutumia nafasi hii kuipongeza Serikali, suala la sheria ndogo ni sehemu ya sheria kwa hiyo utungwaji wa sheria ndogo nzuri na usimamizi wake unachangia sana katika suala la utawala wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema naipongeza Serikali kwa sababu ukiona utulivu mitaani, haiwezi kuwa asilimia 100 ya utulivu, lakini ukiona hali ya utulivu mitaani, ukiona haya mambo ya kukua kwa uchumi na mambo mengine yote, hayo yote yanatokana pia na kuwepo kwa utawala wa sheria kwa sababu kila jambo ambalo linafanyika linapaswa lifanyike kwa mujibu wa sheria. Sasa ni sheria za namna gani, ndiyo hili ambalo tunalizungumza kwamba lazima ziwe ni sheria bora ambazo zimezingatia viwango katika utungaji wake na zinaweza kusimamiwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama nilivyosema, kwamba Kamati imezungumza mambo mengi mazuri na wachangiaji wamezungumza vizuri, nizungumzie labda mambo matatu tu. La kwanza ni jambo ambalo limesisitizwa juu ya hizi sheria ndogo kuzingatia sheria mama na kuzingatia Katiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli yako mambo mengine ambayo ukiyatazama unaweza ukafikiri ni madogo, lakini yanatisha kidogo. Kwa mfano hili suala la ombaomba ambalo kumekuwa na utaratibu wa kusema haya, wamekamatwa warudisheni kwao. Sasa unajiuliza kwao ni wapi? Maana Katiba ya Nchi inasema una haki ya kuishi mahali popote ilimradi huvunji sheria. Sasa nikivunja sheria hapa Dodoma nitahukumiwa tu, lakini sitaambiwa nirudi kwetu. Sasa hii ya kusema warudi kwao, najiuliza hivi kwao ni wapi? Kwa hiyo nadhani hizi sheria ndogo kuna haja ya kuzipitia kila wakati kuhakikisha kwamba hazivurugi mambo katika misingi kama hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni kuzingatia uhalisia pamoja na utafiti. Kwa mfano, kwenye Jimbo la Mwanga, kuna Bwawa la Nyumba ya Mungu pale; sheria na hata ukisoma kwenye leseni zao wanasema kwamba huruhusiwi kuvua samaki ambaye ukubwa wake ni chini ya inchi tatu. Sasa kwa miaka karibu 20 pale sasa hivi samaki wa pale hawavuki inchi tatu, wako hivyohivyo, wanataga mayai, wanajukuu hivyohivyo wakiwa wadogo. Kwa hiyo ina maana ukiamua kufuatisha hiyo sheria ni kwamba pale mahali hapatavuliwa kabisa na ukiifuatisha matokeo yake kila siku tutakamata wavuvi haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi haramu nasema kwenye inverted commas kwa sababu nashindwa kusema ni haramu wakati ambapo huwezi kupata halali kwa vile samaki hawavuki kile kiwango. Ndiyo maana nikasisitiza kuangalia uhalisia na utafiti, kwamba sasa hapa tumefika mahali ambapo hatuwezi kupata hao samaki ambao umewaweka kwenye leseni.
Kwa hiyo, ni lazima kuwe na exemption kwa sababu haiwezekani sheria hiyohiyo ika-apply Ziwa Victoria, iende Ziwa Tanganyika, bado iende kwenye kabwawa kadogo kama kale ka kwangu ka Nyumba ya Mungu. Kwa hiyo kuzingatia uhalisia na pia utafiti wa mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu; ni vizuri by-laws zetu nyingi zikawa zinazingatia kwenye kuwezesha kuliko kuzuia. Nitoe tu mfano, hapa katikati kulikuwa na shida kubwa sana kwamba mtu alikuwa anakatazwa hata kukata mti ambao aliupanda yeye mwenyewe. Sasa unarudi kwenye Katiba ya Nchi, kwamba mtu ana haki ya kupata kipato halali kutokana na kazi halali aliyoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mtu amepanda mti wake ili ukiiva auvune apeleke mtoto wake shule, siku ya kuukata unamkataza kwa sababu ya sheria. Nadhani sheria zingekuwa zimesisitiza zaidi kwenye kuwezesha upandaji wa miti ili tusije kugombana na mtu anayekata kamti kake kamoja shambani wakati kuna maeka na maeka ya maeneo ambayo haya miti ambayo yangeweza yakawekewa sheria yakapandwa miti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani tukizingatia hayo; kwanza tukizingatia huo uandishi bora uliozungumzwa na Kamati, tuzingatie kwamba hizi by-laws zifuate sheria mama, zifuate Katiba; pili, utafiti pamoja na uhalisia; na tatu, kwenda kwenye uwezeshaji zaidi kuliko kuzia, nadhani tutakwenda vizuri na faida ya sheria ndogo tutaiona na utulivu wa nchi utaendelea kuwa vizuri na watu wataendelea kufaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwangu ni hayo mafupi, nashukuru kwa nafasi. (Makofi)