Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tumbe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hoja hii iliyotolewa na Kamati ya Sheria Ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria yoyote duniani ipo kwa ajili ya kudhibiti hisia za wanadamu kwa kuwa mwanadamu anaweza kuamka leo vizuri, kesho vibaya, anaweza kukasirika, anaweza kufurahi sana akatoa maamuzi ambayo siyo sahihi. Sasa baadhi ya sheria ndogo zinaeleza kabisa kwamba jambo hili lililokosewa ataachiwa Mkurugenzi labda wa halmashauri fulani aamue kwa namna atakavyoliona kosa. Sasa nadhani tuiombe Serikali ifikirie kipengele hiki. Mwanadamu yeyote anaweza akamhukumu mtu vibaya kwa sababu tu hata ya mwonekano wake. Kwa hiyo tukiruhusu kwamba tumuache tu Mkurugenzi ahukumu atakavyoona naona haitakuwa sahihi. Kwa hiyo naiomba sana Serikali jambo hili wafikirie kwamba lengo la sheria ni kudhibiti hisia za wanadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kwamba kuna sheria hii ya madawa yaliyoharibika au yaliyo-expire, yasiyofaa, kufanya recall, kwamba labda yameathiri huko au yanaonekana yana madhara yakarejeshwa, Serikali ikaamua kurejesha zile dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sheria mama, mtu aliyefanya kosa hili anatakiwa alipe faini ya shilingi milioni moja. Hata wale wadau wa sheria hii walikuwa wanaona kwamba adhabu hii ni ndogo sana kulinganisha na kosa hili kwa sabbau hapa ni maisha ya mtu. Anaweza akala dawa ikamgharimu kuondoa maisha yake duniani au akapata athari kubwa ikamsababishia ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu anaweza kulifanya kosa hili kwa sababu tu hakutegemea kwamba atapigwa faini ya shilingi milioni moja ambayo dawa ile ikiuzwa anaweza kupata hata milioni 100 ya faida. Ni vyema sasa sheria hii ikaangalia vizuri au ikaangaliwa upya ili sheria ndogo zinazotungwa zikaweza kupata unafuu wa adhabu angalau watu wakapata hofu ya kujali maisha ya wengine ambao ni wanyonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii naihisi kama vile ni kama sheria ile ya mpira, mtu mpirani anaweza kuvunjwa mguu kabisa, lakini aliyevunja mguu hukumu yake aoneshwe tu kadi nyekundu, yaani anaoneshwa tu. Sasa nadhani Waziri na Serikali ifikirie maslahi ya wanaotumia dawa, kwamba wanaweza kuondoa maisha kwa sababu ya sheria kama hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, naiomba Serikali ione huruma sana juu ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Chama hiki ni chama kinachopenda wanyonge sana, kinachopenda kuondoa kabisa ubaguzi, hakina ubaguzi kabisa; watu wenye ulemavu, wasio na ulemavu, wanadamu wote ni sawa. Sasa inapotungwa sheria ya kuwadhibiti ombaomba halafu ukaainisha kabisa mtu mwenye ulemavu, sijui unawafikiriaje hawa ambao ni viongozi wetu wa Chama cha Mapinduzi, viongozi wenye busara, viongozi mashujaa, mahiri sana, unawafikiriaje hawa na Ndiyo chama kinachoongoza Serikali hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa najiuliza mpaka tunafikia kutunga sheria ya kudhibiti ombaomba, hawa Maafisa wa Serikali waliopo pale wilayani, kuna Mkurugenzi na wasaidizi wake, kuna Mkuu wa Wilaya na wasaidizi wake, hawa wote wana maafisa wanaowasaidia. Sasa malengo ya kuweko maafisa wengi hawa ni nini kama siyo kuwasaidia hawa wengine ambao ni wanyonge?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo dogo tu. Kama ni ombaomba, wewe ndio Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, fanya utafiti; hawa ni ombaomba kwa uzururaji, kwa ulemavu, kwa ugonjwa au kivipi? Maana yake mpaka unafika kutoa hii sheria ya kuwadhibiti ni kwa sababu gani unafanya hilo jambo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ombaomba wamo walemavu ambao sheria ya halmashauri inasema kwamba wewe uwapatie asilimia mbili ili kuwawezesha. Tungetegemea sasa halmashauri imwombe Waziri au itengeneze sheria kuliomba Bunge kwamba sasa hawa ile ruzuku wanayopewa kwa mkopo basi wapewe tu bila kurejesha kwa sababu ni walemavu, lakini leo halmashauri inasema inataka kuwadhibiti. Inakuwaje Serikali yetu ya wapenda wanyonge inayoongozwa na viongozi wenye busara sana, leo unasema kwamba ombamba wadhibitiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Sheria kama itatekelezwa, maana yake haitamalizia hapo. Kuna watu wataharibikiwa na safari njiani, wataenda kwenye taasisi za dini; kuna mtu ataenda Kanisani, mwingine ataenda Msikitini ataomba, jamani nimekuja hapa nimeharibikiwa na safari; na watu wakiwa na roho mbaya wanaweza kumshitaki, kwa sababu ni ombaomba pia. Kuna watu wanaojenga taasisi za dini kwa kupitia michango ya wanadini wenzao, watu wakiwa na roho mbaya wanaweza kumshitaki kwa sababu sheria hii ya kudhibiti ombaomba ipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba sana waliotunga sheria hii watuonee huruma sana, hasa Chama chetu cha Mapinduzi kinachopenda wanyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)