Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, napenda nikupongeze wewe mwenyewe kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia napenda nimpongeze Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais akiwa ni mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais tangu nchi ipate Uhuru mwaka 1961. Napenda niwapongeze Mawaziri wote mliochaguliwa katika nafasi zenu na pia nimpongeze Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Afya Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy, ukiwa kama mama kwa kuchaguliwa kuiongoza Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kumaliza hayo, ninayo machache ya kuzungumza. Katika Mkoa wetu wa Katavi tunacho Chuo cha Afya ambacho kilianza kukarabatiwa mwaka 2010 na kikasimama, lakini mwaka jana kimeanza kukarabatiwa kwa kasi. Naomba kasi hiyo iendelee na chuo hicho kiweze kufunguliwa ili kiweze kusaidia huo Mkoa wa Katavi na kiweze ku-train wanafunzi ambao watausaidia mkoa, kwa sababu mkoa upo pembezoni na watu wengi huwa wanasuasua kwenda kufanya kazi huko. Kwa hilo, naomba niishukuru Wizara ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, napenda niongelee pesa za Basket Fund. Naomba pesa hizo ziwe zinawahi kupelekwa kwenye mkoa wetu zinatakiwa zipelekwe mwezi Julai mpaka Septemba, lakini zile pesa huwa zinapelekwa mwezi wa kwanza au zinapelekwa Disemba zikiwa zimeunganishwa na pesa za Oktoba mpaka Disemba. Matokeo yake katika Mkoa wetu wazee wanashindwa kupata matibabu, wanaishia kuandikiwa cheti ili waende kununua dawa, vifaa tiba vinakosekana hospitali, pia watoto wanakosa chanjo, vitanda vinashindwa kununuliwa mahospitali kwa sababu hizo pesa zinachelewa takribani miezi sita ndiyo zinapelekwa kwa pamoja. Kwa maana hiyo, kwa muda wote huo wa miezi sita kunakuwa hakuna vifaa. Kwa hiyo, nashauri zile pesa ziwe zinaharakishwa kupelekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nizungumzie suala la MSD. Napenda Serikali iwe inapeleka pesa Wizara ya Afya ili pesa hizo ziweze kupelekwa kimkoa na ili dawa ziweze kununuliwa kwenye zahanati na kwenye vituo vya afya. Kwa mfano, kule kwenye Mkoa wetu wa Katavi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda ina vijiji 54. Katika hivyo vijiji kuna vituo vya afya 14 tu, vijiji 40 havina vituo vya afya na katika vijiji hivyo 54 tunazo kata 16, katika hizo kata vituo vya afya vipo vitatu, kwa maana kwamba Kata 13 hazina vituo vya afya. Kulikuwa na ule mpango wa MMAM. Mpango huo kadri ya rekodi za Wizara ya Afya unakwisha mwaka 2017 na kule kwetu Katavi hivyo vijiji bado havijajengewa zahanati na hivyo vituo vya afya 13 havijajengwa. Sijui ni muujiza gani ambao utatokea kwa muda wa mwaka mmoja hivyo vijiji 40 viwe vimepata zahanati na hizo kata 13 ziwe zimepata vituo vya afya.
Mheshimiwa Spika, naomba Waziri akija kwa sababu mpango wenyewe wa MMAM bado upo na unakwisha mwaka 2017 labda atatuonea huruma sisi wa mkoa wa pembezoni tuweze kupata hizo zahanati pamoja na hivyo vituo vya afya.
Naomba niishukuru sana Wizara kwa kututengea shilingi milioni 300 kwenye Mkoa wetu wa Katavi, lakini naomba muwaambie MSD wafungue duka la dawa katika Mkoa wa Katavi kwa sababu duka ambalo tunalitegemea kwa sasa hivi lipo Mkoa wa Mbeya na umbali wa kutoka Katavi kufika Mkoa wa Mbeya ni kilometa 600, kwa hiyo, naomba muangalie utaratibu wa kuweza kufungua duka la dawa kupitia MSD katika Mkoa wetu wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitu kingine nashukuru sana kwa watendaji ambao mmewapeleka katika Mkoa wa Katavi, lakini naomba watumishi mnaowaleta katika Mkoa wa Katavi wawe ni trained, msituletee medical attendant, kwa maana ya kwamba kuna vifaa vingine ambavyo wanaweza wakawa wanashindwa kuvitumia, maana yake rekodi inaonesha kwamba, mikoa ya pembezoni huwa inapenda kusukumiwa medical attendant. Naomba mtuletee watumishi ambao ni trained.
Mheshimiwa Spika, pia naomba nitume ujumbe kutoka kwa Wazee wa Mkoa wa Katavi, wanaomba bima ya afya iweze kutumika na mikoa mingine kwa sababu wanaposafiri wakitoka Mkoa wa Katavi, wakiingia Mkoa wa Tabora ile bima inakuwa haifanyi kazi tena. Wanaomba bima ya afya iwe kama ATM ya benki ambayo hata wakiwa Dar es Salaam waweze kutumia hiyo bima ya afya na waweze kupata matibabu yao.
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze suala la afya. Katika suala la afya naomba Wizara yako ya Afya ijaribu kuwa na mawasiliano na wale Maafisa Afya walioajiriwa ambao wako kwenye Halmashauri za Wilaya. Wale Maafisa Afya mara nyingi wanakuwepo pale, lakini unakuta miji ni michafu, unakwenda stand unakuta vyoo ni vichafu, unaenda sokoni, unakuta vyoo ni vichafu. Pia hili suala la kubinafsisha vyoo mpaka stand je, mwananchi ambaye hana pesa atatumia nini?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba haya masuala ya uchafu, kwa mfano kama sasa hivi tunakabiliwa na masuala ya kipindupindu katika nchi hii ya Tanzania. Kama hawa Maafisa Afya wangekuwa wanatoa elimu ya kipindupindu kwamba, watu waweze kunawa mikono yao michafu, wasiweke uchafu, kusiwe na maji ya kutiririka nadhani hili suala la kipindupindu lingekuwa halipo.
Mheshimiwa Spika, pia naomba Wizara ya Afya itoe elimu ya homa ya bonde la ufa, elimu ya ugonjwa zika kwa wananchi kwa sababu kuna mbu anayeeneza huo ugonjwa na wananchi wengi hawajajua athari yake. Hivyo, ikiwezekana basi tuwe kama nchi nyingine ambazo zinapita kuua yale mazalia ya mbu, kwa sababu mfano mzuri, kuna nchi nyingine kama Zambia wanaua mazalia ya mbu ambayo matokeo yake yanapunguza malaria na hayo magonjwa ya zika yanaweza pia kupungua.
Mheshimiwa Spika, naomba pia liangaliwe suala la usafi wa barabara ambazo mifereji unakuta imeziba na yale maji hayatembei na ndiyo yanayosababisha matatizo yote ya magonjwa ya milipuko ambayo yanaathiri sana nchi yetu ya Tanzania na yanaathiri watu wanakwenda kuugua magonjwa hayo ya mlipuko kama vile kipindupindu.
Mheshimiwa Spika, naomba vilevile akinamama wapewe elimu ya kutojifungulia nyumbani, wawe wana-attend kliniki ili kupunguza vifo vya akinamama ambavyo katika kitabu chako umeeleza ni vifo ambavyo vinatisha. Siwezi nikasema idadi hapa, lakini kila mtu amesoma, kwa hiyo, akinamama wangepewa elimu, wasiwe wanajifungulia nyumbani, wanapokuwa wajawazito waweze kwenda kliniki ili waweze kupata matibabu na kuelekezwa jinsi ya kufanya.
Mheshimiwa Spika, kinachotokea sasa hivi ni kwamba, akinamama wale wanakosa elimu na kwa sababu kwa mfano kwenye Mkoa wetu wa Katavi hakuna hizo zahanati kama nilivyosema mwanzo, kwa hiyo, matokeo yake mama anatafuta njia nyingine ili aweze kujifungua atamtumia mkunga wa jadi, kwa sababu katika eneo lake hakuna zahanati na miundombinu ni mibovu, hivyo hawezi akatoka kijijini kule akaenda kufuata hospitali ambayo unakuta hospitali iko kilometa kama 200. Kwa hiyo, naomba hilo lizangatiwe.
Mheshimiwa Spika, naomba kama huo mpango wa MMAM upo Waziri atakapokuwa anafanya majumuisho aje atueleze kama anaweza akatupatia zahanati na hivyo vituo vya afya kwenye Mkoa wetu wa Katavi ili tuweze kupunguza vifo vya akinamama ambavyo vimekuwa vinaathiri sana Mkoa wetu na vinaathiri Taifa kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia kuzungumzia suala la dawa na huo Mfuko wa NHIF ambao watu wengi wamejiunga na hiyo bima ya afya lakini wanapokwenda hospitali matatizo yanakuwa ni hayo ya ukosefu wa dawa, lakini kwenye hiyo mikoa yetu mingine inakuwa ni tatizo la hizo funds ambazo zinakuwa zimechelewa kufika ndio zinasababisha...
NAIBU SPIKA: Tayari dada muda, haupo upande wako.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Afya.