Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuweza kunipa nafasi nami niweze kuchangia michango ya Kamati kutokana na taarifa ambayo imewasilishwa hapa Mezani.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la Ngorongoro mimi itabidi niliruke, naona wadau wenzangu wamelichangia vizuri vya kutosha. Sasa ni kazi kwa Serikali kulichukulia hatua na kwenda kulifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze zaidi katika sekta ya utalii na hapa nitazungumzia kuhusiana na Serikali yetu kujikita na utalii wa aina moja, nao ni utalii wa wanyamapori. Tunaona utalii wa wanyamapori unatuletea mapato mengi ndani ya Taifa letu, lakini kwa nini tunajisahau kuwekeza zaidi katika sekta nyingine? Maana yake kuna utalii wa masuala ya bahari ambapo nakumbuka kwenye Bunge la Bajeti nilisimama hapa na nikachangia vizuri sana. Tuna utalii wa malikale ambapo leo malikale zetu ukizitembelea kwa kweli ni masikitiko makubwa sana kama Taifa. Ninaumia kama mdau wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni ushauri; ukipitia ripoti ya CAG, ameshauri kwamba sasa kama Taifa tuna haja ya kwenda mbele kujiwekeza zaidi katika sekta ya utalii na tuachane na sekta ya wanyamapori, twende na sekta nyingine. Kwa sababu tunategemea sekta hii ya wanyamapori peke yake, leo ikitokea janga la Taifa, Mungu aliepushe, wanyama wamepata magonjwa ama wamepoteza maisha, maana yake hatuna utalii Tanzania. Kwa hiyo, kuna haja kama Serikali kujiwekeza zaidi katika sekta nyingine. Tuna utalii wa kiutamaduni, utalii wa masuala mazima ya bahari, lakini kuna utalii wa wafuga nyuki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hizi sekta za utalii wa utamaduni pamoja na wafuga nyuki nimekuwa interested nazo sana kwa sababu ni sekta pekee ambazo wanaweza kupewa akina mama na wakaziendesha vizuri. Kwanza wataisaidia Serikali kupata mapato na akina mama hawa watatengeneza fedha kupitia sekta hizi. Utamaduni ni muhimu sana. Sasa hivi katika Taifa letu watu wanaiga sana utamaduni wa nje, itafika kipindi hapa wajukuu zetu watasahau asili ya Mtanzania. Sasa tukiwekeza zaidi katika sekta ya utamaduni tunaweza kulisaidia Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nishauri, kama haitoshi, Serikali kama inaona ni mzigo mkubwa kutumia nguvu katika sekta nyingine, kuna haja pia ya kuita ama kuwapa nafasi wawekezaji aidha wa ndani, ama wa nje, kwa ajili ya kuendeleza utalii wetu katika nafasi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie sera. Kamati yangu pendwa ya Ardhi na Maliasili imeshauri hapa na ikawaambia kwamba kama Taifa linahitaji kupeleka mbele utalii wetu, kuna haja sasa ya kubadilisha sera zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiipitia Sera ya Utalii ya mwaka 1999, hebu tuangalie kuna gap ya miaka mingapi mpaka kufikia 2022 leo tunapouzungumza utamaduni wa 1999 na 2022? Hapo tunaweza kupata picha kwamba bado tuna safari ndefu. Kwanza tubadilishe sera zetu. Hata hivyo nishauri katika kubadilisha sera; tusikimbilie kama Wizara tu na department ya utalii wakajifungia peke yao kuanza kuzichambua sera. Ni lazima wajaribu kuwaalika wadau wengine wa Wizara nyingine. Kwa sababu sekta ya utalii ni sekta mtambuka, ukizungumza; uvuvi inaikuta ndani ya sekta ya utalii, ukizungumza mazingira utakuta ndani ya utalii, ukizungumza maji, unakuta ndani ya utalii na Wizara nyingi kama ardhi na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashauri kwamba Wizara ya Utalii ikae sambamba na Wizara nyingine wakati wanatengeneza hii sera, iwe ya utalii ama ya nyuki kwa maslahi mapana ya Taifa ili tupunguze zile contradiction zinavyokuja hapa. Maana yake wakati mwingine unakuwa na swali hujui ulipeleke kwenye Wizara ipi? Kwa hiyo, Mawaziri wakikubaliana kwamba hiki ni kitu cha utalii, lakini kinamhusu wa maji au wa kilimo, au mfugaji, ama mazingira, watakubaliana kwa pamoja ili tuweze kwenda mbele kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kujikita zaidi kwenye suala zima la masoko na utalii. Sekta yetu ya utalii bado hairidhishi ama haturidhiki na masoko ambayo yanafanywa ndani ya sekta hii. Kamati imeshauri, nami pia nashauri zaidi waweze kujiwekeza zaidi katika matangazo. Kwa sababu kuna msemo unasema, “biashara itakangazwayo ndiyo itokayo.” Kwa hiyo, wajiwekeze zaidi kwenye matangazo kwa njia mbalimbali ili tuweze kuisaidia sekta hii iweze kukua zaidi.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, sekta hii ya utalii kuna TV wanaita Safari Channel. Ukiifungua hii TV sometime ina- bore, kwa sababu ukifungua tu unakutana na wanyamapori tu. Yaani dakika kumi, ishirini wanyamapori; baada ya dakika kumi, ishirini, wanyamapori. Kwa hiyo, mtu ataangalia wanyamapori, kesho akifungua akikuta tena wanyamapori, hawezi kufungua tena hiyo TV. Ataangalia vitu vingine. Kwa hiyo, tunatakiwa tubadilishe zile ladha ili tuweze kulisaidia Taifa na kutangaza vyema utalii wetu na vivutio vyetu kwa maslahi mapata ya Taifa hili ili tuweze kupata mapato ya Serikali kuweza kupiga hatua. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.