Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kutoa shukrani zangu za dhati na napenda nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijaalia uzima na afya njema ya kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako hili Tukufu, napenda nitumie nafasi hii kuwashukuru wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Mkoa wa Iringa kwa kunipa kura za kuweza kuwa mwakilishi wao. Pamoja na hilo sitakisahau Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kupokea kura za wanawake wa Iringa kwa kuwa wamenituma kuwa mwakilishi wao na kunipa go ahead. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, hii Wizara ni nyeti sana kwa muono wangu mimi na nilivyoiona. Hata hivyo, baada ya kuipitia hotuba hii kuna ugonjwa huu wa UKIMWI, ugonjwa huu una magonjwa nyemelezi kuna typhoid, homa za hapa na pale. Magonjwa haya yanapelekea hawa wenzetu ambao wana ugonjwa huu wa UKIMWI kuondoka haraka kwa sababu ya kukosa kutibiwa. Naiomba Wizara hii iweke Bima ya Afya kwa hawa wagonjwa ili wakiwa na magonjwa haya nyemelezi waweze kutibiwa. Hakutakuwa na sababu ya kupewa dawa za ARV wakati wakiugua magonjwa nyemelezi wanakosa dawa za kutibiwa typhoid ili waweze kupona. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba Wizara hii ije na mpango mkakati juu ya elimu ya ulaji wa vyakula. Magonjwa sugu yasiyoambukiza kama moyo, saratani, sukari na mengine ambayo tunayafahamu, haya yanasababishwa na vyakula ambavyo Watanzania sasa hivi tunakula. Ni ukweli usiopingika tunapenda Watanzania wawe wajasiriamali ili wainue vipato vya maisha, lakini sambamba na hilo hawa wajasiriamali wanaolima mboga mboga, wanaofuga kuku ambao ndani ya siku 14 unakuwa ni mlo sahihi, hawa ndio wanaopelekea haya magonjwa kulipuka. Mkulima wa nyanya, mkulima wa mboga aina ya chinese dawa anamwagilia leo asubuhi, jioni wanachuma mboga wanakwenda kuuza. Sumu zote zinaingia kwenye mwili wa binadamu na kupelekea haya magonjwa yasiyoambukiza kukua kwa kasi katika Taifa letu
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa nchi yetu ya Tanzania ni kubwa sana. Ina square mita za mraba 947,303. Mheshimiwa Waziri mwenye Wizara hiyo nina uhakika hataweza kufikia maeneo yote. Ushauri wangu naomba atumie vipindi vya redio na tv kuelimisha Watanzania kuhusu mlo bora. Tutafika pale ambapo tumekusudia Watanzania.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kuna hili shirika la MSD. Wizara kama haitajikita kuhakikisha inakuwa na mpango mkakati wa kuweza kulipa madeni yanayopelekea shirika hili kuidai Serikali, tutapiga makelele usiku na mchana dawa hazifiki kwenye Halmashauri, haitawezekana kwa sababu MSD inaidai Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni mambo ya fedheha pale inaposadikika kuwa nchi zinazoisaidia Tanzania kwenye magonjwa, maambukizi kuleta dawa kama dawa hizi za UKIMWI, zinapofika bandarini na shirika letu kushindwa kwenda kukomboa kwa sababu wanaidai Serikali, wale waliotusaidia wanatuona sisi ni wa ajabu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichangie kuwa kwa sababu tayari zile hela za Wabunge, zilishaelekezwa kwenye madawati, zingekuwa bado, hizi ndiyo zilitakiwa ziende zikalipe kwenye shirika la MSD ili Serikali iweze kulipa, waweze kupata dawa zao na kuweza kupeleka kwenye Halmashauri zetu kama tulivyoazimia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara ya afya kwa kuipandisha hadhi hospitali ya Mkoa wa Iringa kuwa Hospitali ya Rufaa. Hospitali hii ilikuwa imeelemewa sana na wagonjwa waliokuwa wamejazana kwenye vitanda wawili wawili. Kwa wagonjwa wa kawaida unaona ni nafuu, lakini kwa akinamama wajawazito, tunafahamu akinamama wajawazito shape zao huwa zinabadilika. Sasa shape zile kulaza kitanda tunachokijua cha wastani wa Wizara ya Afya watu wawili si sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya Wizara kuipandisha hospitali ya Mkoa kuwa Hospitali ya Rufaa, Manispaa ya Iringa wameweza kujenga hospitali ya Wilaya. Jengo la utawala limekamilika, wodi ya wagonjwa wa nje limekamilika, wodi ya wazazi imekamilika. Baada ya kukamilika wodi ya Wazazi Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mheshimiwa Peter Simon Msigwa amepelekea vitanda 30 na magodoro yake kwa ajili ya kuwasaidia akinamama wajawazito hao. Kwa sababu hospitali ya Wilaya tumesema iko TAMISEMI, lakini TAMISEMI nafikiri wewe Waziri wa Afya ndiyo mwenye Mamlaka, naomba basi, kwa sababu hospitali hii imekosa vifaa tiba, kwenye bajeti yako ya mwaka 2016/2017 hebu waambie TAMISEMI watusaidie hivi vifaa vifike pale Hosptali ya Frelimo.
Mheshimiwa Spika, upande wa walemavu, Waziri nikisema hapa mimi kama mama mtu mzima, mwenye nusu karne, suala la kwenda kujifungua ni suala nyeti sana. Maeneo tunayoishi, tumeona wenzetu wenye ulemavu wa viungo wanapopata shida wakati wanapokwenda kujifungua. Kwanza kabisa mapokezi ya wale manesi yako tofauti na mtu ambaye yuko kama nilivyo mimi na pili, vitanda vile wanavyoenda kujifungulia si rafiki na wenyewe na maungo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namuomba Waziri mwenye dhamana kwa namna ya pekee, ndani ya mwaka huu wa bajeti hebu alipe kipaumble suala la wanawake walemavu wanapokwenda kujifungua. Nitaona umelitendea haki Taifa, nitaona umeweka tija sura ya mwanamke kwa mwanamke anapopata nafasi ya namna hiyo anakuwa na huruma ya pekee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo. Nakuja kwenye tatizo la meno na macho. Ni ukweli usiopingika karibu ya robo tatu ya Watanzania tunavaa miwani sasa hivi na tunaotoa meno ni takribani milioni 20. Naomba Wizara yenye dhamana iangalie mpango mkakati wa jinsi ya kutoa elimu ya vyakula vinavyoweza kupunguza watu tusiwe vipofu mapema na tusianze kutoa meno chini ya umri usiotakiwa. Masuala yote hayo yanasababishwa na hivi vyakula ambavyo tunakula, lakini kwenye mpango huu wa hotuba ya Waziri sijaona mahali ambako amewekea kipaumbele suala la macho na meno. Hivyo, nikaona ni wakati muafaka baada ya kuwa nimepata nafasi ya kuchangia, niweze kulisemea hilo.
Mheshimiwa Spika, mimi naishi Mkoa wa Iringa na nimezaliwa Iringa. Naiomba Wizara ya Afya kuhusu afya ya uzazi wa mpango ni hatari. Kwa nini nasema ni hatari? Napenda kama inawezekana sheria itungwe ndani ya Bunge hili inayokataza utengenezwaji wa viroba. Viroba ni pombe zinazonunulika kwa bei ndogo sana, kwa maana hiyo unakuta hawa watoto wa under eighteen wanaanza kulewa toka asubuhi na ndiyo inapelekea waanze kuzaa kabla ya umri wao, wakati akili ya kulea mtoto yenyewe haijakomaa. Dada na kaka kama yamkini wanaweza kuwa wameoana, je, kupata Taifa linaloongezeka kwa kasi, lisilokuwa na malezi ya kielimu, ya kiafya Taifa hili tunalipelekea wapi?
Mheshimiwa Spika, kwa sababu nimetoa dondoo kuwa uzazi huu unasababishwa na ulevi wa pombe hizi zinazonunulika kwa bei ndogo ndogo. Tuliombe Bunge letu Tukufu, tutakapokuja kujadili, hebu tutunge sheria ya kutokutengeneza pombe hizi za viroba zinazouzika kwa shilingi mia tano, mia tano tuifute kabisa. Tanzania hii tunayokusudia itakwenda kwa kasi kwa sababu tutapata watu watakaozaa watoto ndani ya umri unaotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache, naomba niunge hoja ya Kambi ya Upinzani kwa asilimia mia moja kwa maana ndiyo inayotoa mwongozo ili Serikali iweze kufanya vizuri.