Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. STANSLAUS H. NYONGO – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA YA MAENDELEO YA JAMII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Niendelee tu kushukuru na kupongeza sana Wabunge wote. Tumepata wachangiaji 15; na kwa kweli Wabunge wote wameunga mkono hoja, hakuna hata mmoja aliyepinga. Vilevile, tumepata wachangiaji ambapo tumesikia Naibu Mawaziri wawili ambao wamechangia pamoja na Mawaziri wawili ambao wametoa ufafanuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Kamati niendelee kupongeza sana Mawaziri hawa, wamefanya kazi vizuri na Kamati yangu kama unavyoifahamu ina sasa Wizara nne. Kwa kweli mambo ni mengi na tulipata muda mdogo kidogo wa kuweza kutoa ufafanuzi. Pia tumetoa kwenye maandishi na kila Mbunge anaweza akapitia na imeonesha ni jinsi gani ambapo Kamati imeweza kutoa ushauri kwa kina kwa wizara zote hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nisisitize mambo mawili matatu kwa kila sekta. Mambo makubwa yaliyojitokeza, kubwa ni hili suala la; kwanza kabisa tunaipongeza Serikali kwa kutoa fedha nyingi kwenye fedha hii ya mkopo ambayo ni shilingi trilioni 1.3 ambapo kwa kweli Mheshimiwa Rais ameitendea haki nchi yetu kwa kuweza kuelekeza hizi fedha ziende zikajenge miundombinu ya elimu na afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika fedha hizi zimekwenda karibu shilingi bilioni 800 na ushei, ambazo zimekwenda kwenye miundombinu ya elimu na afya. Nii sawa sawa na kama 75% hivi zimekwenda kujikita kwenye kupeleka huduma kwa wananchi. Jambo hili kwa kweli Mheshimiwa Rais tunampongeza sana kwa sababu hii changamoto ilikuwa ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyosikia Wabunge, pamoja na kutoa pongezi hii, ni kwamba tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi wa afya na elimu. Kwa wastani, kwa sekta zote hizi mbili tunaona kabisa tuna upungufu wa watumishi karibia 50% kwa kila sekta. Walimu pamoja na madaktari na watumishi wa afya, kwa kweli naipongeza Serikali, Waheshimiwa Mawaziri wamezungumza, lakini kwa kweli Serikali ichukue juhudi za kipekee kuhakikisha kwamba tunaajiri watumishi wa sekta ya elimu na afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa walimu, tuhakikishe tunazalisha walimu wenye ubora. Tunaweza tukawa na madarasa ya kutosha lakini kama hakuna walimu, bado watoto wetu wanaweza wasipate elimu inayostahili.

Kwa hiyo, tunapenda kuishauri Serikali na kuisisitiza kwamba tuzalishe walimu wa kutosha ili waende wakawafundishe watoto hawa. Kwa kweli juhudi zilizofanyika ni kubwa, kwa hiyo, lazima tukamilishe kwa kuweza kupeleka walimu wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo, tunawapongeza sana Wizara ya Afya, walitoa mwongozo wa masuala ya kuulinda au kuhakikisha kwamba wale wafanyakazi au watumishi wasiokuwa na ajira, wanaojitolea (volunteers) waweze kwenda kufanya kazi kwenye vituo vya afya na zahanati. Kwa kweli hili nalo lifanyike kwa Wizara ya Elimu. Volunteerism ifanyike ili kusudi watu wapelekwe kule hata ambao hawana ajira, basi itafutwe namna bora au program bora ya kuajiri kama parttime ili waweze kutoa huduma kwa wananchi, kwa sababu wananchi wanahitaji huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fikiria kijiji kilikuwa hakina zahanati, leo kina zanahati, majengo yamejengwa pale, lakini hakuna mganga; what do you expect? Wale ambao hawajaajiriwa, basi waende pale wakatoe huduma kwa wananchi halafu iangaliwe namna ya Serikali kuwalipa hawa hata kama ni kidogo, basi waweze kutoa huduma. Ajira ikija, siku mkiamua kuajiri hawa waliojitolea muwape kipaumbele cha kuwapa ajira. Kama ni walimu wapewe ajira kwa kipaumbele kwa sababu walijitolea; na kama ni waganga na manesi, nao wapewe kipaumbele cha kupewa ajira kwa sababu wamejitolea na kwa kweli wametoa huduma na wameshirikiana na Serikali katika wakati mgumu, nao muweze kuwajali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la MSD limezungumzwa na kila Mbunge hapa. Suala la upatikanaji wa dawa, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri ametoa ufafanuzi, lakini MSD iwezeshwe. MSD kama haijawezeshwa, bado litakuwa ni tatizo. Tunashukuru kwamba fedha zimetolewa shilingi bilioni 373 lakini kuwezeshwa huko, na mfumo urekebishwe wa kuweza ku-monitor usambazaji wa dawa. Kama hakuna mfumo thabiti, upotevu wa dawa utakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunawapongeza sana MSD kwa kuamua kuzalisha dawa, tumeona essential drugs zinazalishwa na Keko Pharmaceuticals; tumekuta uzalishaji a hundred percent. Sasa kama uzalishaji wa essential drugs upo kwa 100%, kwa nini kunakuwa na upotevu na huu upungufu wa dawa kwenye vituo vya dawa? Kwa sababu wanaangalia mahitaji na uzalishaji, sasa huu upungufu umetokea wapi? Inaonekana hapa katikati kuna upotevu wa dawa. Basi ingaliwe namna ya kuwekeza katika kuweka mifumo mizuri ya kuweza kuhakikisha dawa inasimamiwa wakati wa kuzalisha, wakati wa kununua,wakati wa ku-stock, kusambaza na kupeleka kwa wagonjwa na watumiaji. Hili ni jambo la msingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasisitiza hivi kwa sababu gani? Kama tumeweza kujenga Kituo cha Afya kwa shilingi milioni 400, umejenga zahanati kwa shilingi milioni 100, umejenga Hospitali ya Mkoa kwa mabilioni ya fedha, tunashindwa nini ku-invest kwenye Kituo cha Afya shilingi milioni tano ya kuweka mfumo ambao uta-monitor mapato, dawa, matumizi na kuwezesha kujua kwamba stock hii ipo eneo hili na hili na stock hii kuna upungufu eneo lingine, mfumo unakueleza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri, kwenye blood bag imeonekana. Kuna maeneo MSD wametueleza blood bag ipo Mkoa X, halafu Mkoa Y hakuna blood bag. Maana yake nini? Pangekuwa na mfumo unao-monitor Mkoa X una blood bag in excess, basi huo mfumo umwelekeze blood bag zitoke Mkoa X kwenda ku-supply Mkoa Y ili hawa watu wa Mkoa Y nao wapate blood bags. Hili ni suala la mfumo tu. Kwa hiyo, tunasisitiza sana mfumo ufungwe katika ku-monitor hizi shughuli za ku-control stock.

Mheshimiwa Mwenyekiti, issue ya mitaala, tunaishukuru sana Serikali, wameeleza vizuri na mwaka 2026 tunategemea kwamba tutapata mitaala mipya na ianze kufundishwa. Tunasisitiza waendelee kufanya kwa haraka, lakini lazima uangalie, mtoto anayemaliza Kidato cha Nne ambayo sasa hivi tumesema ndiyo basic education, mnapomfundisha, basi afundishwe na utaalam, atoke na utaalam fulani ili hata asipoendelea Kidato cha Tano, akienda mtaani awe utaalamu fulani wa kuweza kufanya kazi. Atakapomaliza chuo cha kati, awe na ujuzi, yaani tupate namna ya kupata wataalam wadogo wadogo ambao wanaweza kwenda kuzalisha katika viwanda vidogo vidogo. Hili ni jambo la msingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la michezo limezungumzwa vizuri, tuwekeze. Hizi kampuni zinapotoa misaada kwenye michezo, basi ile gharama inayotolewa kwenye michezo iwe inatambulika kwenye mahesabu ya kikodi, kwamba mtu anaye-finance; mfano, kampuni imetoa fedha ya kununua mipira, iweze kutambulika kikodi ili waweze kupunguziwa katika corporate tax. Hili ni jambo la muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie suala la Mheshimiwa Mulugo; suala hili linatisha kwa kweli kama kweli hiyo hali ipo. Tunaomba wadau pamoja na Serikali tukae, tujadili tuone. Ku-control ufundishaji kwamba mwezi wa Tatu topic moja na mbili ziwe zimeshafundishwa, hiyo sawa; lakini kumzuia mtu kufundisha zaidi eti kwa sababu anawahi sana, hilo tunaomba tukae na kuweza kuli-review. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kuhusu mimba za utotoni Mheshimiwa Bidyanguze amezungumza vizuri, tunahitaji elimu, watoto tuwafundishe. Biologically mtoto akishakuwa matured anapokwenda kwenye secondary growth ana-develop kitu kinaitwa ovulation period, ndiyo kipindi cha hatari yeye kupata ujauzito. Aambiwe kipindi hiki kina dalili zipi, ili asijihusishe. Bila ya kufanya hivyo, tutaendelea na dropouts kwa watoto na utoro utaongezeka na hii inakuwa ni hasara kwa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Basi baada ya kusema hivyo, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. KASSIM HASSAN HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti naafiki.