Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuanzia Januari, 2021 hadi Februari, 2022 pamoja na Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuanzia Januari, 2021 hadi Februari, 2022 pamoja na Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na mimi niungane na wenzangu kukupongeza sana kwa kupata nafasi hii na tunakutakia kila la heri katika kutekeleza majukumu yako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia mimi nitajikita katika eneo la usalama wa chakula kwa maana ya food safety. Nasema hivi kwa sababu duniani kote masuala mazima ya usalama wa chakula kwa maana ya food safety yanaratibiwa chini ya Wizara ya Afya kwa maana ya kuwa chini ya mamlaka ya Kudhibiti Ubora wa Chakula na Dawa na hata Tanzania miaka ya nyuma ndivyo ambavyo tulikuwa tunafanya chini ya TFDA, na hata nchi za Afrika Mashariki zilikuja kwetu kujifunza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini miaka ya karibuni Serikali iliamua kuivunja TFDA na badala yake kuunda TMDA na jukumu la usalama wa chakula kwa maana ya food safety wakaliweka chini ya Shirika la Viwango (TBS). Sasa jambo hili mtaniwia radhi sana kusema lakini limeweka maisha na afya za watanzania rehani.

Mheshimiwa naibU Spika, nasema hivyo kwa sababu TBS ina jukumu la kuangalia ubora wa matairi, ubora wa mabati, ubora wa misumari mabati na kadhalika na hapo hapo iweje tena TBS hiyo hiyo ipewe jukumu la kuratibu na kudhibiti ubora wa usalama wa chakula kwa maana ya food safety.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa hawa TBS ndiyo wanaotoa vibali kwa wazalishaji wa chakula, halafu hao hao tena waende waangalie kama ule ubora kile kibali walichotoa kimekidhi, tayari hapo kuna conflict of interest.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo mahsusi ambalo lilijitokeza ambalo linadhihirisha kabisa TBS haiwezi kuendelea kubeba jukumu la usalama wa chakula kwa maana ya food safety. Mwaka jana kwenye tarehe 13 au 14 Oktoba, 2021 Shirika la Chakula na Madawa la Kenya lilitangaza kwamba linarudisha juice aina ya Ceres ya apple ambazo zilikuwa na aina moja ya sumukuvu ambayo ni hatari kwa maisha ya wanadamu. Mpaka siku hiyo kwa huku Tanzania TBS ilikuwa haijasema kitu chochote.

Mheshimiwa Naibu Spika, gazeti la Mwananchi likawatafuta TBS na nakumbuka Mkurugenzi mwenye Idara husika alisema kwamba mpaka muda ule wa kwenye tarehe 14 Oktoba juice aina ya Ceres ilikuwa haijaingia nchini na wanaendelea kufuatilia na pale ambalo zitaingia nchini basi watazizuia na watatoa taarifa na watafanya uchunguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, siku ya tarehe 16 Oktoba TBS ikatoa taarifa ya umma kuelezea kwamba wamejiridhisha juice zile hazijaingia nchini juice aina ya Ceres na barcode ambazo zilikuwa zimewekwa wakasema na waiambia umma kwamba kila kitu kiko sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa masikitiko makubwa TBS walitudanganya Watanzania kwa sababu kwenye tarehe 22 mimi kwenye kiosk kimoja hapa Dodoma nilikuwa zile juice za Ceres aina ya apple zikiwa zinauzwa na nilichukua jukumu la kupiga picha na kumtumia Waziri mwenye dhamana wa wakati ule wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ambaye akapokea akasema atalifanyia kazi. (Makofi)

Kwa hiyo, moja kwa moja inaonesha kwamba kwanza TBS hawachukulii serious jambo la usalama wa chakula kwa maana ya food safety; TBS hawana muda wa kuangalia masuala ya usalama wa chakula na TBS wanaendelea kuhatarisha maisha ya Watanzania kwa kuendelea kulimbikiza mambo mengi ambayo hayaendani pia na mambo ya usalama wa chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi kwa unyenyekevu mkubwa sana naiomba Serikali ipitie upya uamuzi wake wa kuondoa masuala ya usalama wa chakula kutoka Wizara ya Afya na kuyapeleka kwenye eneo la mambo ya Viwanda, Biashara na kadhalika turudi kwenye basic practice. Hii haitakuwa mara ya kwanza ya Serikali kufanya mapitio na maboresho ya uamuzi wake kadri ambavyo itaonekana inafaa.

Kwa hiyo, mimi kwa kumalizia na kwa unyenyekevu mkubwa sana na kwa maslahi mapana ya kulinda afya za Watanzania, kulinda mzigo mkubwa ambao Wizara ya Afya unao, kulinda mzigo mkubwa wa ongezeko kubwa la magonjwa ya kansa ambayo hayaeleweki, suala la usalama wa chakula kwa maana ya food safety lirudi ndani ya Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja ahsante. (Makofi)