Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mikumi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuanza kuchangia Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninaomba nijielekeze kwenye kuipongeza Serikali ya mama Samia kwa kazi nzuri ambayo imefanya ya ujenzi wa madarasa, vituo vya afya na zahanati. Lakini kuna kazi kubwa ambayo inaendelea chini ya TARURA. Pamoja na kazi hii kubwa, lakini pia tunaona impact ya hii mikopo ya asilimia 10 kwenye halmashauri zetu. Ni kazi nzuri ambayo inahitaji uungwaji mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hivyo fedha ambazo zinakwenda kwenye mikopo kwa ajili ya makundi maalum ya hiyo asilimia kumi ni nyingi sana. kwa mfano kwenye bajeti ya mwaka huu ni zaidi ya bilioni 69 na kitu ambazo zinakwenda kwenye mikopo kwa ajili ya makundi haya maalum. Fedha hizi ni nyingi, ni vizuri tuka-review uendeshaji na usimamizi wa fedha hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tungependa kujua ni kiasi gani ambacho kipo kwenye mikono ya vikundi ambavyo vimekopeshwa; ni kiasi gani ambacho kimerejeshwa na nini mpango endelevu wa hizi fedha? Kwa sababu hatuwezi kuendelea kutoa fedha hizi kwa maisha yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tujue ni kiasi gani ambacho kipo ambacho kinaweza kikawa mtaji wa kutosha tukaingiza kwenye revolving fund ikazunguka yenyewe bila ya kuendelea kuchota tena kwenye bajeti kuu. Kwa hiyo ni vizuri tukajielekeza namna bora ya kuangalia uendeshaji wa hizi fedha za asilimia kumi ya mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, halmashauri zetu kimsingi zinahitaji mipango endelevu, hasa ujenzi wa miundombinu ambayo inaweza kwenda kutoa ajira endelevu kwa wananchi wetu. Ukiangalia reli ambayo inatengenezwa ya SGR kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza, Makutupora, unaweza kuona mashimo makubwa ambayo yanatumika kama chanzo cha kokoto za ujenzi wa reli hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashimo haya makubwa yanaweza sana kutusaidia kutengeneza mabwawa ambayo yanaweza kwenda kutumika kwa ajili ya shughuli za uvuvi, mifugo na kilimo kwa ajili ya umwagiliaji na ika-save fedha nyingi sana za Serikali. Ninapenda kujua ni kiasi gani cha mashimo ambayo yamechimbwa ambayo tunaweza tukabadilisha kuwa mabwawa na ikawa sehemu nzuri ya kutengeneza miundombinu kwa ajili ya wavuvi, wakulima na umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili linahitaji mahusiano ya karibu kati ya halmashauri zetu (TAMISEMI), Wizara ya Kilimo na Wizara ya Maji na huku kwenye mifugo. Kazi nzuri ambayo inafanyika katika Serikali za Mitaa inahitaji mahusiano ya karibu kati ya TAMISEMI, Wizara ya Kilimo na Mifugo ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ambayo ipo sasa hivi na mahusiano yaliyopo hayatoshi kwa sababu ukiangalia idara ya mifugo kwenye halmashauri zetu, ukiangalia uvuvi kwenye halmashauri zetu ukiangalia kilimo kwenye halmashauri zetu, haziakisi umakini katika suala zima la kuhakikisha kwamba sekta hizi zinakwenda kutoa ajira ya maana kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu; tutengeneze mfumo madhubuti ambao Wizara hizi zinaweza zikakaa pamoja kuona namna bora ya kuboresha masoko na biashara zetu. Kwa mfano unaweza ukaangalia suala zima la ghala au stakabadhi ya ghala jinsi gani ilivyo sensitive katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado hatujui role ya halmashauri katika usimamizi wa maghala; hatujui role ya Wizara ya Viwanda na Biashara katika usimamizi wa maghala; hatujui role ya Wizara ya Kilimo katika usimamizi wa maghala. Tunahitaji kujua nani ambaye ana dhamana ya kusimamia maghala na biashara, hasa katika suala zima la bidhaa na usambazaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kadhia ambayo imetokea kwenye soda inaweza ikatokea kwenye pembejeo, inaweza ikatokea kwenye viuatilifu, inaweza ikatokea hata katika usambazaji wa mazao. Hii scarcity ama deficit inaweza ikawa created kwa sababu hatuna taasisi ambayo inakwenda kusimamia maghala. Tunahitaji kuwa na sheria ambayo inatoa majukumu ya nani anakwenda kusimamia na kuratibu haya maghala.
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na ninaomba kuunga mkono hoja.