Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi nijielekeze moja kwa moja kwenye sekta ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi sekta ya barabara nchini imekuwa na changamoto nyingi sana na hii ni kwa sababu ya kukosa vipaumbele, yaani hatufikiri kimkakati. Nitoe mfano hapa upande wa REA. REA wameanza kusambaza umeme kwenye vijiji vyote na wanahitimisha na sasa wanakwenda kwenye vitongoji. Halikadhalika kwenye barabara tungeiga mfano huu, kwamba leo hii bado nchini kwetu kuna baadhi ya mikoa haijaungana, lakini bado tunakwenda kujenga barabara za wilaya, mimi nadhani hapa tuna-misuse resources. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukilinganisha upatikanaji wa rasilimali fedha na mahitaji makubwa ya barabara nchini hayafanani. Kupanga ni kuchagua. Wachumi wanasema opportunity cost, una-foregone for the best alternative. Sasa, niombe na niishauri Serikali ianze kwa kukamilisha kuunganisha mikoa yote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalan Mkoa wa Morogoro. Mkoa huu katika uchumi wa Taifa letu ni mkoa wa tano katika Pato la Taifa lakini bado mkoa huu mpaka leo haujaunganishwa kwa kiwango cha lami na Mikoa ya Lindi, Ruvuma pamoja na Njombe; na ukiangalia mkoa huu uko kimkakati. Kwa hiyo, niombe tu, kwamba Wizara ya Ujenzi; na niseme kwa dhati kabisa; jamaniee! Katika eneo hili tusi-politicize, tusifanye maamuzi ya kisiasa katika ujenzi wa barabara zetu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kuna madhara makubwa sana na hasa ya kiuchumi. Barabara ya mkoa na mkoa wanufaika ni wengi ukilinganisha barabara za wilaya na wilaya. Vile vile kiuchumi barabara ya mkoa na mkoa na wilaya na wilaya ni tofauti kabisa, lakini madhara yake makubwa katika ugawaji wa rasilimali za nchi kunakuwa na uneven distribution of national income, kabisa. Kwa sababu leo hii wilaya na wilaya wana barabara ya lami, ukija Morogoro na Njombe hawana lami, kwa hiyo kuna Wilaya ngapi hazina lami kwa Mkoa wa Morogoro? Ni nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali, kwa kuwa tunakwenda kwenye kipindi hiki cha bajeti, tuje na mpango wa kukamilisha lami kwenye mikoa yote kwanza ili twende kwenye wilaya. Hii itawatendea haki Watanzania. Mfano mzuri ni wa barabara ya Morogoro – Njombe – Boarder. Barabara hii inaunganisha mikoa za nyanda za juu kusini. Nikitaja mikoa hiyo, ni mingi kweli, mpaka Rukwa mpaka Ruvuma barabara hii kwa sababu inapitia hapa Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, itoshe tu kusema, naishukuru Serikali imeanza kuchukua hatua, ila hoja yangu ya msingi, tunazungumza kwa Habari ya zile kilometa 50, barabara ya Morogoro - Njombe Boader kutoka Ifakara ipite Mlimba iende Madeke – Lupembe mpaka Kibena Junction, barabara hii mpaka sasa naambiwa iko kwenye mchakato wa manunuzi, na mwaka wa fedha unaisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli naomba niseme tu kwa dhati, kipindi cha bajeti, Wizara ya Ujenzi ijiandae kisaikolojia, nitashika shilingi. Sitakubali kuona kama lami inayozungumziwa kilometa 50 kutoka Ifakara - Mlimba haijaanza kujengwa. Nitashika shilingi, na nitakuwa wa kwanza. Haiwezekani tunafanya maamuzi ya kisiasa katika mambo ya msingi ya wananchi. Naomba tuanze kuunganisha mikoa ili sasa twende kwenye wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kuna mtu mmoja anaitwa GN. Huyu GN ni mtu gani? Najiuliza GN yuko sayari gani? Yuko sayari hii au yuko sayari nyingine GN? Huyu ni mtu gani ambaye amekuwa adimu sana kupatikana? Kosa tunalofanya wame-centralize; leo hii GN inatoka TRA Makao Makuu, kwani kudai centralize kuna kosa gani? Si tuna Meneja wa Mkoa wa TRA! Zitoke GN huko. Leo hii miradi karibu 600 anatoa mtu mmoja kule Makao Makuu TRA, ataweza kazi hiyo!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naishauri Serikali na hasa Wizara ya Fedha iachane na ku-centralize mamlaka inayohusika na GN; iji-centralize katika level za mikoa, wanaweza kufanya kazi hiyo ili miradi yetu iendelee haraka. Vile vile procurement process zinakwama sana kwa sababu ya GN, mkandarasi haanzi kazi kwa sababu ya GN. Huyu GN ni mtu gani? Anapatikana sayari ya hii dunia au yuko sayari ya Mars?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuwasilisha. (Makofi)