Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kasulu Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii awali ya yote naunga mkono hoja zote mbili na ni Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nichukue fursa hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais kwenye ziara zake hizo za Ufaransa na Ubelgiji tumeona anasaini mkataba, wa mabilioni ya shilingi ambayo tunaamini yatakuja kwenye Taifa letu na hatimaye itakuwa ni hatua muhimu sana kuwasaidia Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaongelea maeneo mawili kwenye taarifa yetu eneo la kwanza ni kwenye kiwanda cha viuatilifu kile ambacho kipo kwenye Mkoa wa Pwani. Naanzia hapo kwa sababu ni kiwanda mahususi ambacho kilianzishwa kwa ajili ya kutokomeza malaria na kwa miaka kumi, ukianzia mwaka, 2010 mpaka mwaka, 2020 tumepoteza watanzania zaidi ya 70,000 kwa sababu ya ugonjwa wa malaria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni Majimbo kadhaa ya uchaguzi tumeyapoteza. Mwaka 2015 NDC Shirika letu lilichukua mkopo ambao ni takribani shilingi bilioni 50 kutoka Hazina kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa kiwanda hiki. Kiwanda ambacho kilijengwa na kukamilika mwaka 2017 kiwanda walisaini mkataba na Wizara ya Afya kwa maana ya kwamba Serikali, kupitia halmashauri itakuwa inanunua viuatilifu hivi na kwenda kupulizia huko kwenye mazalia ya mbu ili kutokomeza mbu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikueleze ule mkataba haujatekelezwa, kiwanda hakiuzi viuatilifu, ni kama kimetelekezwa, tunajiuliza kuna hujuma au kuna nini katika hili? Over 50 billion! Serikali inatumia mabilioni ya shilingi kila mwaka kwa ajili ya kupambana na malaria. Kwa nini tusiende kununua viuatilifu hivi tukapuliza hatimaye tuondokane na tatizo la malaria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jamaica wameondokana na malaria kwa sababu ya kutumia teknolojia hii ambayo walitupa nasi, tulinunua kwao. Kiwanda kile hakina faida hiyo tu kwa maana ya kwamba ni viuatilifu vya kupambana na malaria. Kamati tumetembelea pale walituambia kwamba kiwanda kile kina uwezo wa kutengeneza viuadudu (pesticides). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu inatumia mabilioni ya shilingi kila mwaka kwa ajili ya kununua viuadudu kwenye masuala mbalimbali, nchi hii inatumia bilioni 57 kila mwaka kununua viuadudu kwa ajili ya zao la pamba, inatumia bilioni 50 kwa ajili ya kununua viuatilifu kwa ajili ya zao la tumbaku na inatumia karibu bilioni 100 kila mwaka kwa ajili ya kununua viua wadudu kwa ajili ya zao la korosho. Ni mabilioni haya ambayo kila mwaka tunayapeleka nje ya nchi wakati tuna kiwanda na teknolojia hapa, kama tukikipa uwezo, tukawekeza pale, Serikali isikitelekeze, tunaweza tukaokoa mabilioni ya shilingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nigusie kidogo kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Kwanza Mheshimiwa Naibu Spika hongera sana kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii tunajua wanafanya biashara, lakini wanaenda kuwekeza zaidi kwenye real estate mabilioni ya shilingi wanapeleka yote kwenye real estate, wanajenga majengo hata majengo yenyewe hawayamalizi, wanaenda kujenga majengo porini kama lile la Dege Beach kule Kigamboni ambayo return yake hakuna, wameshindwa na ku-prove failure kwenye real estate. Hela za Watanzania zimewekwa kule, zimefia kule. Sasa sijui ni woga, wakitoka hapo wanaenda kwenye mambo ya investment kwenye mambo ya bonds hapo wanashindana na Wabunge na Watanzania wengine kwenda kununua bonds! Hawa wanapaswa wawaze vitu vikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, real estate ina players wengi, TBA wapo humo ndani, National Housing wapo humo ndani na akina Musukuma wapo humo ndani, akina Kishimba wapo humo ndani na wawekezaji wengine wengi, waachane na real estate, waende kuwekeza kwenye vitu ambavyo vina faida kubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunalo tatizo la mbolea hapa Tanzania kila mwaka, NSSF wakiamua kumaliza tatizo hili wanaweza, watujengee kiwanda kikubwa cha mbolea hapa ambacho kinamaliza shida ya mbolea Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo shida ya sukari, tunazo shida kwenye mambo mbalimbali, kwa hiyo nadhani mashirika haya…
T A A R I F A
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa. Mheshimiwa Musukuma.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ninapenda kumpa taarifa mzungumzaji kwamba hata hizo real estate zinazowekezwa na Taasisi za Serikali zinakuwa nje ya soko kwamba tunayo maeneo ndani ya mji ambayo wanaweza wakajenga na kupata wapangaji, wanazitoa wanaenda kuzi-dump ili wapige deal halafu na nyumba hazipati wateja. (Makofi/Kicheko)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Vuma taarifa hiyo.
MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea, naamua kukubali kwa sababu ni Mheshimiwa Musukuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme, hawa watu wajielekeze kwenye vitu, leo hii Mama amewapa hela nyingi sana, juzi tu hapa, walikuwa na madeni Serikalini, kawapa over two trillion siyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, wanatakiwa waende kumsaidia kutengeleza ajira, waende kwenye investment, business model ambayo inatengeneza ajira mbalimbali kwa Watanzania, haya mashirika yanayo nafasi ya kutusaidia, kumsaidia Mama kutengeneza ajira kwa Watanzania. Kwa hiyo waachane na vitu vidogo vidogo hivi ambayo hata vyenyewe vimewashinda, waende kuwekeza kwenye mambo makubwa ambayo yataleta faida ya kiuchumi pia na kuongeza ajira kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono tena hoja. Ahsante sana. (Makofi)