Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Rashid Mohamed Chuachua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia kwenye Wizara hii adhimu kwa mustakabali wa afya za Watanzania. Nitumie pia fursa hii kumpongeza Waziri na timu yake kwa hotuba nzuri waliyoitoa, inayoonesha mwelekeo wa suala zima la utekelezaji wa sera ya afya katika awamu hii.
Mheshimiwa Spika, ninapoiangalia Wizara ya Afya, nashindwa kabisa kutenganisha majukumu yake na TAMISEMI na kwa maana hiyo basi kama majukumu hayo tunaweza tukayatenganisha katika actual practice, acha tuseme katika kiwango hiki cha kuchangia, ili tuweze kueleza matatizo na changamoto zilizopo katika Wizara ya Afya, halafu hao wenyewe kwa sababu Serikali ipo, watagawana, watajua hiki ni cha TAMISEMI na hiki ni cha Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno haya, niseme tu kwamba kama ningekuwa napata fursa ya kuangalia changamoto za Wizara zote, basi Wizara ya Afya ningesema namba moja, inawezekana katika Majimbo mengine ni tofauti, lakini katika Jimbo langu Wizara ya Afya ni Wizara ambayo ina changamoto kubwa sana kuliko Wizara nyingine zote.
Mheshimiwa Spika, jambo hili kwanza linatupeleka katika kuhakikisha kwamba, fedha wanazoomba zinapatikana na zinafika kwa wakati. Pili, ni jambo ambalo nadhani linatakiwa liwekewe msisitizo maalum na Serikali ili kila mwaka tusiendelee kuimba changamoto za Watanzania katika eneo hili la afya.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwa kuakisi moja kwa moja Jimbo la Masasi ambalo kimsingi Jimbo hili kabla halijagawanywa na hata kabla ya Wilaya haijagawanywa tulikuwa tuna Hospitali moja tu ya Wilaya inaitwa Hospitali ya Mkomaindo. Tumegawanya Wilaya na sasa tuna Wilaya ya Nanyumbu, Hospitali kubwa ni ile ile. Tumegawanya Majimbo, lakini bado tunategemea hospitali moja. Hospitali ambayo inahudumia watu wa Wilaya takribani mbili, pamoja na watu wanaotoka nje ya nchi ya Tanzania kwa upande wa Msumbiji. Ni hospitali iliyoelemewa sana.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa tunapozungumza, hospitali hii ina changamoto kubwa ya dawa, hospitali hii ina changamoto kubwa ya vifaa tiba na hospitali hii ina changamoto kubwa ya majengo. Labda tu nitoe mfano, tunayo wodi ya wazazi ambayo kwa mwaka hospitali hii inapokea takriban wazazi 4,200, ina vitanda 10 tu. Hii ni changamoto kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, nina imani kwamba, mwanamke ndiye kiumbe anayekwenda hospitali mara nyingi zaidi kuliko mtu yeyote. Kama hatutaangalia kwa jicho la kipekee huduma zinazowagusa wanawake, hatuwezi kusema tumepiga hatua katika sekta ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali liwe suala hili linahusu TAMISEMI au liwe linahusu Wizara ya Afya, waje na majibu, ni lini upanuzi wa wodi ya akinamama katika Hospitali ya Mkomaindo utafanyika ili kusudi akinamama hawa wasilale chini au wasilale wawili wawili? Mheshimiwa Ummy amefika Hospitali ya Mkomaindo ameiona. Mheshimiwa Jafo pia amefika, ameiona na changamoto zake. Tunaomba tupate majibu ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kwamba huduma zinasogea karibu na wananchi, tunaiomba Serikali izipandishe hadhi baadhi ya zahanati zinazozunguka Jimbo la Masasi ili kusudi kuisaidia Hospitali ya Mkomaindo. Naomba ipandishwe hadhi zahanati ya Mwengemtapika, zahanati ya Mombaka na zahanati nyingine ya Chisegwe, tuwe na vituo vya afya. Wenyewe mtagawana majukumu mjue ni nani ambaye anahusika na kupandisha zahanati hadhi na nani anahusika na kuwepo kwa zahanati hizo. Naiomba Serikali iangalie eneo hili.
Mheshimiwa Spika, tunapozungumza hapa, Jimbo la Masasi lina takribani ya mitaa na vijiji 60 na zaidi, lakini tunazo zahanati tano tu. Tuna uhaba mkubwa sana wa watumishi wa afya, tunapungukiwa na watumishi 400 na kibaya zaidi kama wiki mbili zilizopita watumishi 19 tena wamesimamishwa kazi kwa kosa la kughushi vyeti na kwa maana hiyo, hatuna kabisa watumishi. Naomba Serikali iliangalie hili na ilifanye kama jambo la dharura, hali sio nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na haya yote niliyoyaeleza, lakini tuna magari mawili tu kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa. Haiwezekani, mambo hayawezi kwenda. Tunaiomba Serikali na hili nalo iliangalie.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2014 kuna ubadhirifu wa fedha ulifanyika na baadhi ya watumishi wa Hospitali ya Mkomaindo, fedha za dawa. Naiomba nayo Serikali itoe majibu, hatua gani mpaka sasa zimeshachukuliwa? Shilingi milioni 29 hazijulikani zilitumika vipi. Naomba Serikali itoe majibu hatua ambazo imezichukua ili wale wanyonge waendelee kupata matibabu.
Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia suala la utekelezaji wa huduma za afya bure kwa wazee, nalo jambo hili ni zito na gumu sana katika Jimbo langu. Hapa ninapozungumza toka mwezi wa Kwanza hakuna hata shilingi iliyopelekwa kwa ajili ya kuwahudumia wazee katika Jimbo la Masasi. Wazee hawa wanapata shida, wanawaona madaktari kwa shida na wakiwaona hawapati dawa. Kwa hiyo, tunakosa kuona umuhimu wa kuwepo hilo Dirisha la Wazee. Naomba pia Serikali iliangalie hili kama ni suala la Serikali Kuu au kama ni suala la Serikali za Mitaa, lakini sisi shida yetu watu wa Masasi, wazee wapate huduma zao.
Mheshimiwa Spika, yapo mambo mengi katika Wizara hii hatuwezi kuyamaliza yote, lakini kimsingi na kwa namna ya kipekee tuone namna ambavyo Serikali inatoa msisitizo maalum katika kuboresha vyuo vyetu vya maendeleo. Tunavyo vyuo takribani 55 ni vyuo vichache nchi nzima, tunahitaji vyuo hivi viongezwe, lakini kikubwa zaidi vyuo hivi havina wataalam na havina vifaa vya kutosha.
Mheshimiwa Spika, nadhani umefika wakati sasa pamoja na pendekezo la vyuo hivi kwenda Wizara ya Elimu, lakini lazima utoke msisitizo maalum kuhakikisha kwamba vyuo hivi ndivyo ambavyo tutakuja kuvitegemea kwa ajili ya kutengeneza vijana watakaoingia kwenye soko la ajira tunapokwenda kwenye uchumi wa viwanda. Vyuo vilivyopo chini ya mamlaka ya VETA havitoshi na kwa maana hiyo, vyuo hivi vina nafasi kubwa sana. Naomba Serikali itazame vyuo hivi, kikiwemo chuo kilichopo katika Jimbo langu cha Masasi FDC. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema yako mambo mengi, nimeongea kwa kifupi. Naunga mkono hoja, lakini naiomba sana Serikali ije na majibu ya maswali niliyoyauliza. Ahsante sana.