Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon Faida Mohammed Bakar

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa na pumzi.
Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kama ifuatavyo:-
Kwanza napenda kukishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniamini kurejesha jina langu kuwa mgombea wa Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na kwamba nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu wa Chama cha Mapinduzi kwa kura zenu za kishindo. Nawashukuru sana na sitawaangusha, tutafanya kazi kwa pamoja kukiendeleza Chama chetu cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, mdogo wangu Mheshimiwa Ummy, kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ushirikiano mkubwa na Naibu wake, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, kwa kazi kubwa wanayoifanya. Kwa kweli hakika wanawake tunaweza, hasa tukisaidiana na wanaume. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia hoja hii kwa kuongelea Zahanati yetu ya Bunge kwanza kwa sababu, wahenga walisema sadaka huanzia nyumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kukushukuru sana kwa jitihada za Bunge hili kutupatia Wabunge zahanati mpya ya kisasa yenye viyoyozi na kila kitu mle ndani. Zamani zahanati ilikuwa ni ndogo, chumba kimoja, tulikuwa tunawekewa yale mapazia, mtu akisema upande huu, upande huu ugonjwa wa mwenzake anaujua, lakini mkaona kwamba Wabunge ni watu pia wa kuhifadhiwa. Kwa hiyo, mkatupatia zahanati iliyopo pale mbele kwenye geti kubwa pale kwa mbele, nafikiri wengi labda watakuwa hawaijui, lakini naomba kushukuru Bunge kwamba zahanati hii ni nzuri sana sasa hivi. Sisi Wabunge tunasitirika vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuwashukuru hawa Madaktari. Naomba kuwataja kwa sababu jamani hawa Madaktari wanatusaidia sana, Dkt. Chaula wa kwanza huyu, Bingwa wa Magonjwa ya Ndani (Physician). Dkt. Temba, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura, Dkt. Kiboko, Dkt. Solomon, Sister Sanya, Sister Disifa, Sister Solo, Sister Habiba huyu wa Maabara, Sister Jacquiline huyu Mfamasia. Jamani tunaomba kumshukuru Mwenyezi Mungu na kulishukuru Bunge kwa kitendo kile pale kuwekewa sisi Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ila tunaomba sana yawepo maboresho mbalimbali, naomba kwamba, ikubalike iwe ya saa 24 isiwe ya saa 12. Kwa nini nikaomba hivyo, naomba hata sisi Wabunge tutakapopata matatizo tuweze kulazwa pale yaani tupatiwe vitanda pale, tutakuwa tumesitirika zaidi na vilevile tutakuwa na usiri mkubwa. Vilevile kuwe na maboresho ya haraka ya vifaa tiba, nafikiri vifaa tiba vipo, lakini viongezwe na madaktari pia, waongezwe kama itakuwa ni ya saa 24. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huduma ya afya. Tunaishukuru Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kutujengea Hospitali kubwa ya Benjamin William Mkapa iliyopo hapa Dodoma. Hospitali hii inatibu magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya figo. Pia naomba kuishukuru Serikali kwa kuweka kile Kitengo cha Matatizo ya Moyo kule Muhimbili. Sasa ninachokiomba ni kwamba, matatizo haya ya figo yawe especially yanatibiwa hapa Dodoma kwa sababu, Dodoma pia ni Makao Makuu, yawe yanatibiwa hapa na kule Muhimbili ibakie tu matatizo ya moyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mauaji ya wazee, wenzangu waliongea; kila siku nikisimama hapa naongea mauaji ya wazee, vikongwe. Wazee wetu ni vikongwe na wengine wale wenye matatizo ya ngozi (albino), wanauliwa sana katika nchi yetu hii, ingawa Serikali imefanya jitihada kubwa kuondoa tatizo hili, lakini inatokea kwa siku na siku huwa wazee wanauliwa. Mheshimiwa mmoja alizungumza hapa, ingawa wengine labda watakuwa na matatizo, lakini zisichukuliwe sheria mikononi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na mimi naungana na yeye, wazee wetu hawa ni wazee na sisi pia tutakuwa wazee. Inaniuma sana kuona wazee wanauliwa; kwa nini wazee wanauliwa? Wanauliwa kwa kuhusishwa tu na mambo ya kishirikina kwa sababu ana macho mekundu. Mheshimiwa Waziri hili, wewe ni mwanamke mwenzangu, uwe mbele na imara sana katika kuliimarisha hili na kuwachukulia hatua kubwa sana wauaji wa wazee wetu.
Mheshimiwa Spika, wazee ni wazee wetu, wametuzaa, wametuweka matumboni mwao miezi tisa mpaka kumi mpaka wametuzaa. Kama mzazi anataka kukuua, angekuua alipokuzaa pale kitandani, asingekuja kukuua wewe umeshakuwa mtu mzima. Jamani tuwahifadhi wazee. Wazee ni dua kubwa, tuwapende wazee. Mheshimiwa Waziri naomba hili alichukue sana na kulifuatilia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vituo vya kulelea wazee. Tanzania tunaishukuru Serikali kwamba vituo vipo vingi vya kulelea wazee, lakini jamani aaa, hapana! Vituo vya kulelea wazee vingi vyao vibovu, vifaa hawana, vyakula hawana, hawana nguo, hali zao ni duni sana, utawahurumia! Vituo vipo, lakini tunaomba ipangwe bajeti maalum ya vituo vya kulelea wazee wetu jamani. Wazee ndiyo kila kitu katika maisha yetu, bila wazee sisi tusingefika hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukatili wa watu wenye ulemavu. Ukatili wa watu wenye ulemavu ndiyo sana, unajua ukatili siyo lazima mtu kumuua au kumpiga, lakini hata kama mtu mwenye ulemavu ana elimu yake nzuri, ni msomi mzuri, lakini akibisha hodi kwenye Ofisi, anadharaulika eti kwa sababu hana miguu, hana mikono, hana macho yaani inasikitisha sana.
Mheshimiwa Spika, watu wenye ulemavu ni watu wa kuwahifadhi sana kwa sababu na wewe hujijui. Leo wewe uko mzima una midomo, una miguu, una mikono, lakini kesho utakuwa na wewe mlemavu. Tusipende sana kuwadharau watu wenye ulemavu kwa sababu Mwenyezi Mungu atuepushie, lakini na sisi ni walemavu watarajiwa. Napenda sana kuwaomba wananchi wa Tanzania tusiwadharau watu wenye ulemavu kwa sababu watu wenye ulemavu na wao ni binadamu kama sisi, ni wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho, naomba kuzungumzia kuhusiana na Benki ya Wanawake. Toka niingie Bunge hili, toka ianzishwe Benki ya Wanawake natetea Benki ya Wanawake Zanzibar mpaka leo. Kila siku jibu ninalolipata process zinaendelea, mchakato unaendelea. Mheshimiwa Kigwangalla karibuni tu alinijibu na nikamsifia sana bajeti iliyopita Mheshimiwa Samia ambaye alitoa ofisi yake pale Bwawani. Naomba tu kuulizia, hii Ofisi imefikia hatua gani au ni kitu gani kinachokwaza mpaka Benki ya Wanawake isianzishwe kule Zanzibar? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Zanzibar pia, kuna wanawake, kuna wazee kuna vijana. Pia nao kuna wafanyabiashara wadogo wadogo na wakubwa wanahitaji huduma hizi za Benki yao ya Wanawake.
Naomba sana Mheshimiwa, sana sana, leo nafikiri nitakuja kushika shilingi hapa, lakini mpaka nijibiwe hii Benki ya Wanawake isiwe tu ni mdomo mdomo. Kila siku mdomo mdomo tu hapa. Naomba sana Benki ya Wanawake leo nijibiwe inaanza lini kule Zanzibar? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana.