Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Kipekee nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima na afya njema. Nitajielekeza moja kwa moja kuchangia mifuko ya hifadhi na muda ukitosha nitachangia Shilika la NIDA. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika, mifuko ya hifadhi ya jamii imebeba maisha ya watanzania, wafanyakazi na wakulima kutokana na umuhimu wa mifuko hii. Lakini ripoti ya CAG imeonesha uwepo wa deni kubwa ambalo ni la muda mrefu. Tukiangalia taarifa ya Kamati ukurasa wa 28 & 29 napenda kunukuu. “Hoja kubwa ambayo imepewa msisitizo na CAG katika mifuko ya hifadhi ya jamii ni uwepo wa deni la muda mrefu ambalo mifuko inadai kwa Taasisi mbalimbali na hasa Serikali.” Deni hili limekuwa likikwamisha sana wastaafu kupata mafao yao kwa wakati. Na nikilitaja deni hili ambalo Shirika la NSSF linadai ni shilingi trilioni 1.1 ambalo hadi sasa limefikisha miaka 10 deni hili halijalipwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati mwingine tunailaumu mifuko hii hailipi mafao kwa wakati lakini inakuwa na mzigo mzito wa deni hili ambalo sasa inafanya kutowalipa wastaafu kwa wakati. Kwa upande mwingine wa Shirika letu la NHIF Serikali inadaiwa kiasi cha shilingi bilioni 209.7. Ningeishauri Serikali iweze kulipa fedha hizi kwani zinaharibu mizania ya hesabu na kufanya utendaji wa shirika kutokufanya kazi ka ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulichangia ni Shirika letu la NIDA. Nielezee kwa masikitiko makubwa sana. Upatikanaji wa vitambulisho vya NIDA umekuwa na usumbufu mkubwa na hasa kwa wananchi wangu wa Mkoa wa Singida na Kagera. Nikielezea tu mfano mdogo, Wilaya ya Manyoni ina halmashari mbili, halmashauri ya Itigi na Manyoni. Lakini kituo kinapofanyikia usajili wa vitambulisho hivi vya NIDA ni Wilaya ya Manyoni. Mwananchi kutoka Rungwa anatembea kilomita 200 kufuata kitambulisho cha NIDA ambapo sasa kituo cha kusajili kipo Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.
Mheshimiwa Spika, niiombe sana Serikali iangalie uwezekano wa kupata vituo vingi vya kuweza kusajili vitambulisho hivi na wote tunatambua kwamba vitambulisho hivi vina umuhimu sana na vinamtambulisha mtanzania. Mfano tu, ukitaka kufungua akaunti, kusajili line, kufungua biashara au kupata mkopo ni lazima uwe na kitambulisho cha NIDA. Kwa hiyo, unaweza kuona kwamba, umuhimu mkubwa wa vitambulisho hivi.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Kamati ya PAC ukurasa 31 imeonesha ukaguzi uliofanywa na CAG kwa mwaka 2020/2021; na umebaini uwezo mdogo wa kuzalisha vitambulisho hivi. Pamoja na kununua mashine mbili mpya ambazo zilianza kufanya kazi Januari, 2021. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, NIDA inatakiwa kujitathmini je, inayo uwezo wa kutoa huduma kwa wananchi? Mpango kazi wa NIDA wa 2020/2021 uliitaka NIDA kuzalisha vitambulisho milioni 13.7 lakini hadi kufikia Juni, 2021 lengo hilo halikufikiwa. Ni vitambulisho milioni 3 tu ndivyo vilivyoweza kuzalishwa na kufanya jumla ya vitambulisho milioni 9.4 ambavyo vyote vilikuwa vimezalishwa. Unaweza kuona ni jinsi gani huduma hii inavyosuasua na jinsi wananchi wanavyotaabika kupata vitambulisho hivi.
Mheshimiwa Spika, niishauri Serikali, ihakikishe vitambulisho hivi vinapatikana kwa wakati. Lakini pia ripoti ya CAG imebaini kwamba mkandarasi hakulipwa madeni yake.
Mheshimiwa Spika, napenda kuunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)