Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Ruth Hiyob Mollel

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nimshukuru Mungu kwanza kwa kuweza kusimama hapa na nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia kwenye hoja hii iliyopo hapa mezani.
Mheshimiwa Spika, naungana na Wabunge wote ambao wameshazungumza kuhusu afya, kwamba afya kwa kweli, ni msingi mkubwa sana wa uchumi. Taifa lenye afya ndiyo linaweza kujenga uchumi wa nchi hii. Kwa hiyo, nasema Mawaziri mna kazi kubwa sana ya kuona kwamba, Taifa hili linakuwa na afya njema.
Mheshimiwa Spika, ningependa kuzungumzia suala la mfumo wa afya. Mfumo wa afya umekaa vizuri kwa sababu tunaanza zahanati, tunakuja kituo cha afya, tunakuja mkoa na kadhalika. Mfumo umekaa vizuri sana kama tutautumia kwa ajili ya kuboresha afya ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, niseme kwamba, tukiangalia katika Hospitali ya Muhimbili kwa mfano, imejaa wagonjwa sana na huu mrundikano wa wagonjwa unatokana na kwamba hizi peripheral hospitals hazijawa na vifaa vya kutosha ambapo wagonjwa watatibiwa kule, kupunguza huu msongamano ulioko Muhimbili. Huu msongamano hautakwisha mpaka hizi peripheral hospitals Mwananyamala, Temeke, najua zimepanuliwa, lakini bado hazikidhi kuweza kupunguza msongamano ambao uko pale Muhimbili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashauri kwamba, Hospitali hizi za peripheral health centres, kuna hizi Hospitali za Rufaa ambazo zimeteuliwa za Mikoa zingepewa vifaa tiba vya kisasa kama CT Scan kusudi ianze kuchuja wagonjwa tangu pale mwanzo halafu Muhimbili waje wale ambao kwa kweli wanahitaji specialized treatment.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunapendekeza tuwe na CT Scan katika hizi referral hospitals, tuwe na CT Scans pia katika Hospitali za Mbeya najua pengine ipo, Bugando na KCMC kusudi hii influx kubwa inayokuja Muhimbili ipungue. Hata influx pia katika hizi Hospitali nyingine za Bugando, KCMC na Mbeya bado nao wanakuwa na wagonjwa wengi, lakini kama hizi referral hospitals za mkoa tulizoziteuwa zikifanya kazi, basi tutapunguza msongamano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nina mawazo kwamba hizi hospitali nyingine za Super Specialisation za Bugando, KCMC, Mbeya na Muhimbili na zenyewe zipewe vifaa tiba vya kisasa. Kwa mfano, tukiwa na vifaa tiba vya kisasa kabisa huu utaratibu wa kupeleka wagonjwa wengi nje utapungua.
Kwanza wagonjwa wengi watatibiwa hapa nchini na kwa yale maeneo ambayo hatuna uwezo nayo, kama kuna eneo ambalo hatuna specialization, tunaweza kuleta madaktari kutoka nje wakaja hapa kwa bei nafuu, wakatibu wagongwa wengi.
Mheshimiwa Spika, baada ya kutibu wagonjwa wengi vile vile tunajenga uwezo wa wataalam wetu ndani ya nchi, kama tunavyofanya katika Kitengo cha Moyo, hii system ingeendelea pia kwenye maeneo ya magonjwa mengine ambayo tunapeleka wagonjwa nje.
Kwa hiyo, ni maoni yangu na maoni ya Kambi ya Upinzani kwamba, tuzi-strengthern tupunguze wagonjwa kupelekwa nje na wagonjwa wengi zaidi waweze kutibiwa ndani ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri na kuna eneo ambalo hajaligusia sana, amezungumzia kuhusu watoto na changamoto za watoto, lakini kuna hawa watoto ambao wako katika mazingira magumu, ukipita mitaani Dar es Salaam utakuta watoto wengi wanaombaomba, wanatumiwa kuomba.
Mheshimiwa Spika, sasa ningependa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja aweze ku-share na sisi kuona ni hatua gani Wizara itachukua? Najua itahusisha labda na Wizara ya Elimu kwa sababu watoto wale wana haki ya kupata elimu, ni kwa jinsi gani mkakati utakaoletwa ili kuona jinsi gani hawa watoto wanasaidiwa kuondoka katika haya mazingira ambayo yanasababisha kukosa haki yao ya elimu na haki ya kutokunyanyaswa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna eneo moja pia ambalo wengine wameligusia, eneo la magonjwa ya akili. Nimeshakuwa na mgonjwa pale Muhimbili kwa kweli hali ya pale ile Faculty ya Psychiatric ni mbaya sana. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana uweze kwenda pale mahali. Pale wagonjwa wanafungiwa kama wako jela! Wanafungiwa, hawatoki na hawapati hata nafasi ya kupatiwa counseling kwa sababu yale maeneo hayawezekani.
Mheshimiwa Spika, najua kwamba kuna kazi ambayo tayari kile kitengo kimeshafanya, wameshafanya sketch ya kujenga kituo cha kisasa lakini hawana architectural drawings kwa sababu hawana fedha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, naomba uende pale uone na tutafute namna, hata kama kutafuta joint venture, kama inawezekana au donors whatever, lakini waweze kujenga kituo cha kisasa kwa sababu sasa hivi magonjwa ya akili yamezidi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, magonjwa ya akili yamezidi sana kwa sababu ya ulevi wa kupindukia, msongo wa mawazo, umaskini na madawa ya kulenya. Kwa hiyo, hawa wagonjwa wanaongezeka kwa wingi sana na kile kitengo hakiwezi kuhimili. Kwa hiyo, ni rai yangu kwako uende ukatembelee pale hali ni mbaya sana. Naomba uende pale uweze kuona hali halisi na uonane na hawa wataalam wa pale ambao tayari wana sketch na wameshakisia ni kiasi gani cha fedha kitahitajika kujenga kituo cha kisasa cha magonjwa ya akili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wengi wamezungumzia kuhusu suala la tiba ya wazee. Tunasema kwamba tiba ya wazee ni bure, lakini ukweli ni kwamba sio bure kiasi hicho. Bure ni kumwona Daktari tu lakini ikija kwenye suala zima la matibabu ambapo ndiyo msingi uliompeleka yule mzee hospitali kwa kweli inakuwa ni matatizo makubwa sana. Kwa hiyo, napendekeza kwamba tutafute namna ambayo tunaweza tukachangia zaidi hata kwenye NHIF ili zipatikane pesa ambazo tutawawezesha hawa wazee kupata hizi kadi za NHIF waende wakatibiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi pia ni mzee lakini advantage niliyonayo ni kwamba nina kadi ya NHIF lakini wapo ambao hawana advantage ya NHIF anakwenda pale hawezi kutibiwa. Huyu mtu ujana wake wote kaumalizia katika kujenga nchi hii, lakini wakati sasa ana uhitaji mkubwa hawezi kusaidiwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, kwa kweli hili jambo la wazee naomba mliangalie kwa jicho la huruma kabisa, tuone ni jinsi gani wazee wetu wanaweza kupata tiba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu wamezungumzia kuhusu zahanati, vituo vya afya na hospitali za mikoa, kweli ziko chini ya TAMISEMI. Lazima tukubali kwamba pia anayesimamia na kutoa standards na kuona zahanati inatakiwa itibu nini, vituo vya afya vitibu nini, hospitali za mkoa ziwe na vifaa gani ni Wizara ya Afya. Kwa hiyo, napendekeza katika hospitali za mkoa, Wizara ya Afya iwe na wakaguzi ambao kazi yao itakuwa kwenda kutembelea hivi vituo vya afya na zahanati kuona kwamba zile tiba zinazotakiwa kutolewa pale zinatolewa.
Mheshimiwa Spika, udhibiti huu pia utasaidia kupunguza msongamano kwenye hospitali za wilaya na mkoa. Kwa hiyo, ni mawazo yangu kwamba tuwe na wakaguzi ambao watakuwa ni waajiriwa wa Wizara ya Afya ambao wataweza kwenda kusimamia afya kwa sababu usimamizi wa afya ni wa Wizara na hakuna mtu wa kumtupia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba ufanye hivyo kama fedha zitaruhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante.