Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Namshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia uzima kuweza kufika siku hii ya leo, lakini niwapongeze Wenyeviti wa Kamati zote mbili wakiongozwa na wewe Mheshimiwa Spika kwa kweli, nimewaona super woman, mambo yanavyokwenda ni moto tukiongozwa na Mama yetu Samia Suluhu Hassan, Rais wa nchi yetu. Na Wabunge wanaume wanaona mambo yanavyokwenda, nchi iko kwenye mstari. (kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu umesema Serikali ipo nitajikita zaidi kwenye Wizara ya Kilimo. Sitazungumza kwa sababu siwaoni, lakini kwa sababu umesema Serikali ipo naendelea.

Mheshimiwa Spika, nitajikita zaidi kwenye mradi wa ujenzi wa vihenge na maghala ya kuhifadhi nafaka. Kwenye mradi huu Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliingia kwenye mkopo na Serikali ya Jamhuri ya Poland, mkopo wa dola za kimarekani milioni 55, ni jambo jema kwa sababu, lengo lilikuwa ni kwenda kujenga hayo maghala. Tulipata wakandarasi wawili kwenye huo mkataba. Wakandarasi hao wanatoka Poland, masharti yaliyopo kwenye mkataba vifaa vyote vitoke Poland. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mkopo huu ulikopwa lini; tarehe 28 Septemba, 2015, nataka Wabunge tuangalie hapo hicho kipindi ni cha uchaguzi na mara nyingi mambo yanaharibika sana hapo kuanzia kwenye halmashauri, ukifuatilia hiyo trend utaona kuna jambo fulani hapo. Mikataba hii inatufundisha nini; kabla sijaenda kwenye kushauri tunamuona Mheshimiwa Rais anazunguka huko kwa ajili ya kutumia resources tulizonazo kwenye nchi zitusaidie kama Taifa. Lakini asiposhauriwa vizuri kwenye mikataba ya hovyo lazima ataingia chaka kama hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nini wajibu wetu kwenye hili jambo; mkandarasi kati ya hao wawili ambaye alikuwa anatekeleza mradi Dodoma, Shinyanga, Makambako, Songea na Mbozi, ambaye alipata dola za kimarekani milioni 33.14 amefika asilimia 73 akaja kuomba nyongeza ya dola za Kimarekani milioni 12. Hakuna nyongeza ya aina hiyo! (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana Waziri wetu wa Kilimo pamoja na NFRA waligoma baada ya kuona hilo jambo, lakini wao hawakuingia kwenye huo mkataba, walioshiriki ni Wizara ya fedha. Nawashukuru kwa busara yao waliyoifanya, lakini huyu bwana kwa sababu anajua kuna nini nyuma ya pazia na yeye ameweka mguu chini kwamba, hataendelea na hiyo kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nini kinatokea; amegoma akaondoka, leo mkitaka mumchukulie hatua yoyote fedha hizo ambazo tulikopa ziko Poland. Ni kitu gani hiki kwenye Taifa letu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni mambo ambayo hayafurahishi hata kidogo. Kuna haja sasa ya CAG kwenda kufuatilia vizuri nini kilitokea kwenye huo mkataba. Na mikataba ya aina hii lazima sasa kuna haja ya kuwa wazi tuiangalie mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri kabla ya kuingia kwenye mikopo ya aina hii kwanza waangalie sifa za hiyo nchi. Na huko nyuma iliwahi kufanya hivyo kwa nchi ngapi?

Je, imefanya vizuri au imefanya vibaya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wote tunajua sifa za nchi ya Poland, lakini hayo mengine hatutasema, tuache hapo, lakini tunaamini huu mkataba ulipitiwa na wasomi wetu tena wanasheria. Unakubalije mkataba wa aina hii kuliingiza Taifa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo umenikopesha fedha halafu fedha unazo wewe mwenyewe. Vihenge havijaisha mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali ifanye haraka iwezekanavyo kumaliza mgogoro huu unaoendelea kati ya huyo mkandarasi, ili kazi imalizike. Tofauti na hapo tutaiingiza nchi kwenye Mahakama za kimataifa. Hamuwezi kujua kiburi cha huyu mtu kinatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya dakika tano, nitazungumzia tena deni la bilioni 166 kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu ambalo NFRA wanadai. Tuliomba fedha kile kipindi imetokea tafrani kwa ajili ya zao la mahindi. Serikali ikaja hapa kupitia Waziri Mkuu kwamba tumepewa fedha bilioni 50, tukaona ni jambo jema, lakini kumbe ule ni mkopo amekopa CRDB. Kukopa CRDB sio jambo baya, sasa kama NFRA wanadai Ofisi ya Waziri Mkuu bilioni 166 kwa nini wasingelipa sehemu ya deni badala ya kwenda kukopa benki ya CRDB? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nakushukuru. Mengine tutaendelea kushauri, ahsante. (Makofi)