Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mheshimiwa Spika, lakini kabla sijaanza kuchangia, napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa sababu tangu uchaguzi umefanyika ametuteulia viongozi na tumepata jembe, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Pia napenda kukishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa jinsi ambavyo mmekuwa nami tangu kipindi chote cha uchaguzi na hadi sasa tumepata nafasi ya kuingia Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nasema afya kwanza kwa sababu hakuna Mbunge au mwananchi yeyote ambaye anaweza akafanya shughuli za maendeleo pasipokuwa na afya. Katika kampeni zangu nilikuwa nasema afya kwanza na leo hii ikibidi naomba iwe slogan ya Taifa kama Mheshimiwa Waziri atakubaliana nayo. Napenda kuwashukuru Mawaziri kwa kazi nzuri mnazozifanya pamoja na Naibu Mawaziri kwa jinsi ambavyo mnajituma na kwa kweli hakika hapa kazi tu, tunaiona hii kazi inafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri nimekuwa katika sekta hii ya afya kwa kufanya kazi na mashirika ya watu wa Marekani kupitia Jeshi la Amerika. Kwa hiyo, nafikiri Mheshimiwa Waziri ataweza kupata ushauri wangu katika mambo mbalimbali. Nikianza kwanza na Jimbo langu la Busokelo. Busokelo ni Jimbo ama ni halmashauri mpya ambapo hadi sasa ninavyosema tuna watumishi wanne tu ambao ni specialist, kwa maana ya wanaume wawili na wanawake wawili. Ni sawa na kusema asilimia 100 hatuna watumishi kwa mujibu wa takwimu za kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 140.
Mheshimiwa Spika, lakini pia katika Halmashauri ya Busokelo, tuna kituo kimoja tu cha afya kwa maana ya kata 13, kituo kimoja. Najua hili lipo chini ya TAMISEMI lakini kwa sababu hizi ni Wizara ambazo zina mahusiano, napenda pia Mheshimiwa Waziri alifahamu hili. Pia hatuna hata hospitali ya wilaya tunatumia Hospitali ya Kanisa inaitwa CDH. Eneo tumeshaliandaa na tumeshaanza harakati lakini tunaomba pindi tutakapoomba msaada kutoka Serikalini muweze kutukumbuka katika hili.
Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu katika Kituo cha Afya cha Kandete ambacho ndicho kituo pekee, kinahudumia wananchi wengi sana kwa maana ya Bonde zima la Mwakaleli. Ukianzia na Kata za Itete, Kandete yenyewe, Isange, Mpombo mpaka Wangwa. Huduma zinazotolewa pale ni ambazo hakika, kama hujapata huduma pale maana yake inabidi usafiri umbali wa zaidi ya kilometa 50 kufuata huduma hizo mjini ambako ni Tukuyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba kituo hiki kiwezeshwe tukianzia na masuala ya mochwari hatuna na hata dawa nazo zinafika kwa kusuasua sana. Kwa mfano MSD wamepewa jukumu la kusambaza ama kusimamia tunasema Medical Store Department nchi nzima. Wakati mwingine MSD wanachokifanya utashangaa imebaki kama mwezi mmoja, ama miezi miwili kusambaza hizo dawa kwa maana zinakuwa expired lakini wanazisambaza. Kwa hiyo, zinakuwa hazina manufaa kwa wale wanaopelekewa kwa sababu kipindi kifupi tu zinakuwa tayari haziwezi tena kutumika kwa afya ya binadamu.
Mheshimiwa Spika, nizungumzie sasa suala la huduma za UKIMWI katika nchi yetu ya Tanzania. UKIMWI ni janga la Kitaifa na Kimataifa na kwa bahati mbaya sana bajeti ya Serikali imekuwa kidogo sana ukilinganisha na uhitaji wa huduma kwa ugonjwa huu wa UKIMWI. Kuna mashirika mawili hapa nchini, kuna Global Fund na PEPFAR. PEPFAR ni President’s Emergency Plan For AIDS Relief, ni shirika ambalo liko chini ya Serikali ya Marekani, lilianzishwa enzi za Rais, Mheshimiwa Bush. Pamoja na kwamba tunatumia Global Fund ambayo ni nchi mbalimbali lakini asilimia kubwa bado inachangiwa na Serikali ya Marekani.
Mheshimiwa Spika,In case imetokea hawa Wamarekani wanasema sasa stop kuchangia Afrika na Mataifa mengine hakika Tanzania hatutakuwa sehemu nzuri. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali kupitia Wizara hii waongeze bajeti ya kutosha katika masuala ya UKIMWI. Wakati mwingine wengi wetu tunaonesha kidole kimoja hivi kwamba yule yule ndiye anaishi na HIV lakini kwa tafiti ambazo tumefanya kwa miaka yote, kumbuka vidole vitatu vinakuonesha wewe.
Mheshimiwa Spika, niwape mfano mmoja, nilipokuwa nasimamia Nyanda za Juu Kusini, Mikoa ya Ruvuma, Katavi, Rukwa, Mbeya, nililia sana nilipofika Hospitali ya Rukwa Mjini, nilimkuta bibi mmoja kizee sana ni mgonjwa, anasema mjukuu wangu hapa sina hata Sh.1,000 ya kununua dawa. Sasa umepataje huu ugonjwa? Anasema nilikuwa namlea mjukuu wangu na kwa sababu hatuna elimu ya kumtunza mtu wa aina hiyo ndiyo nikaupata maana alikuwa hatumii hata gloves. Hakika ilikuwa ni masikitiko makubwa, hata Sh.1,000 za kununua dawa hana. Kuna dawa kwa ajili ya kuzuia opportunistic infections, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla atakuwa anafahamu, Serikali haitoi hata wafadhili pia wamejitoa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lazima kama Serikali tutie nguvu sana kwa upande huo kwa sababu dawa hizi za opportunistic infections zinazuia mambo mengi. Kuna zile ambazo zinazuia fungus, magonjwa ya ngozi na vitu vingi ukiachana na zile tunazoita TLE (Tenofovir/Lamivudine/Efavirenz) ambazo hizo zinatumika hasa hasa kwa upande wa matibabu kwa mama mjamzito na anayenyonyesha. Kwa hiyo, kwa sababu wafadhili nao wanajitoa kuleta hizi dawa za opportunistic infections, ni vizuri sasa tutenge bajeti ya kutosha ili kuzuia maradhi ambayo nimeyatamka hapo awali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia nichangie kidogo katika suala la Hospitali ya Rufaa Mbeya. Hospitali hii inahudumia Kanda nzima, iwe Njombe, Iringa, Rukwa, Ruvuma, Katavi watu wanakwenda kutibiwa pale. Kipindi kile wakati inajengwa ilikuwa ni watu milioni mbili, lakini sasa ni zaidi ya watu milioni nane. Kwa hiyo, tunaomba Serikali hata kupitia Wizara ya TAMISEMI tuweze ku-expand ili iweze sasa kuendana na mahitaji ya sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, si hivyo tu hata Wabunge wenzangu wamezungumzia masuala la CT-Scan, hawana CT-Scan pale na hiyo ndiyo hospitali ya rufaa. Kama hakuna CT-Scan tusitegemee watu wale wanaweza wakapata huduma zilizo bora na sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, naomba nizungumzie suala la TEHAMA, mimi pia ni mtaalam wa mambo ya TEHAMA. Leo hii tunazungumzia ulimwengu wa sayansi na teknolojia ni lazima tuhusishe pia Wizara ya Afya. Mtu kutibiwa popote pale alipo. Tunazungumzia suala la uhaba wa Madaktari Bingwa lakini kuna solution ama majawabu ambayo yanaweza yakatusaidia kama tutaweza ku-adopt, inawezekana isiwe leo au kesho lakini tuwe na wazo kwamba kuna kitu hiki kinafanyika duniani na Mataifa mengine yaliyoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna kitu kinaitwa Telemedicine. Telemedicine ni suala la kutibu mgonjwa popote pale alipo. Kwa maana ya kwamba unaweza ukafanya naye appointment lakini utafanya baada ya kumsaidia kwa kutumia hata hizi simu za mkononi, wengi wetu tunatumia tu WhatsApp, Facebook na vitu vingine lakini simu inaweza ikafanya vitu vingi zaidi ya hivi. Kwa hiyo, Wizara naomba ilichukue wazo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nimeshiriki sana kuandaa na kufanya analysis za Wizara kwa maana ya kutumia tools zinaitwa database, C2C database, DHIS - District Health Information System, LAS - Lap Assessment Response System. Hizi database ni nzuri sana kwa maana ya kwamba inaweza ikaunganisha nchi nzima kufanya analysis ya tuko wapi, ni mkoa gani unaongoza na tufanye nini kwa ajili ya intervention zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninachoiomba Wizara ni kwamba, inabidi hizi system ziwe integrated. Kwa mfano, C2C database ina version nyingi sana lakini ni muhimu sasa iwe ni web-based sasa hivi ni stand-alone, nikisema stand-alone najua mnafahamu nyie Madaktari hasa wale wataalam wa Wizara kwa maana ya kwamba ukipeleka kituoni iko pale pale inabidi tena uhamishe kwa njia ya flash ama external kuipeleka sehemu nyingine. Pamoja na hayo hii LAS - Lapla Response System imekuwa na combined na Post Training Follow-up na itasaidia sana kwa maana ya ngazi ya Wilaya. Kwa ngazi ya Wilaya itakuwa inatuma ripoti moja kwa moja kwa Wizara na haya ndiyo maboresho katika sekta ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla sijamaliza naomba nizungumzie suala la huduma kwa mtoto, maambukizi ya virusi vya UKIMWI (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Kwenye hotuba ya Waziri, ukurasa wa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.