Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye jambo hili.
Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kweli bila kusema maneno mengi mama anaupiga mwingi kama taarifa ya Kamati yetu inavyosema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni ukweli pongezi zangu nizimalizie kwa sehemu mbili moja Wizara ya Fedha wamekuwa wasikivu, wizara hii kupitia Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba na Naibu wake Mheshimiwa Hamad Chande, lakini pia wakiongozwa na Katibu Mkuu Emmanuel Tutuba kwa kweli ni wasikivu wameendelea kufanya kazi vizuri na kamati lakini mpaka kufikia katika makubaliano haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukweli hata Kamati yetu wenyewe nimpongeze sana Mheshimiwa Daniel Sillo, Mwenyekiti wetu wa Kamati lakini na Makamu Mwenyekiti CPA Omar Kigua wanatusimamia vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hayo tuko hapa nakubali kabisa hoja hii na naomba Waheshimiwa Wabunge wakubali kuidhinisha hizi trilioni 1.3 iweze kupata nyongeza ya ukomo wa bajeti ya mwaka 2021/2022.
Mheshimiwa Spika, tulikuwepo hapa tukaidhinisha bajeti ya mwaka 2021/2022 ya shiingi trilioni 36.6. lakini ni ukweli nyongeza hii ya trilioni 1.3 inatupekeka kwenye ukomo wa bajeti ya Serikali ya mwaka 2021/2022 kuwa trilioni 37.98. Hili ni jambo la kisheria chini ya Sheria ya Bajeti ambayo imesomwa kifungu cha 43(3), lakini vilevile, na Katiba yetu Ibara ya 137 Katiba ya nchi. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge ni jambo lipo kwa mujibu wa Sheria ni jambo ambalo ni kubwa na ni zuri kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, mkopo huu umesemwa kwenye Kamati, mkopo huu ulikuwa uwe na riba ya asilimia 1.5 lakini kwa jinsi ambavyo mama yetu amekuwa anao uwezo wa ushawishi mkubwa imeenda kutolewa hii riba ya 1.5 mpaka sifuri. Sasa mkopo huu hauna riba yoyote, lakini si hivyo tu mkopo huu mrejesho wake uwe wa miaka mitatu, lakini ameweza kujadiliana mpaka mrejesho (payback period) imeongezwa mpaka miaka mitano. Hili ni jambo kubwa lakini lazima tumpongeze sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini ukweli leo Watanzania wote wanajua juu ya mkopo wa trilioni 1.3; kila mmoja ukimwambia anajua, hatusemi ya nyuma walikuwa wanajua, lakini kuna uwazi mkubwa sana ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita. Tumpongeze sana Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini matumizi; si kawaida leo kila Mtanzania na wale wananchi wa Kibamba wanajua maana ya trilioni 1.3; kwenye eneo la afya zimepelekwa zaidi ya shilingi bilioni 466, Watanzania wanajua zaidi ya ICU 67 zinaena kupelekwa huko, lakini kuna ambulance za advance karibu 20 lakini ninaambiwa na ambulance basic za kawaida karibu 253, si jambo dogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kwenye elimu wamesema wengine leo madarasa 15,000; madarasa 12,000 ya kawaida ya sekondari, lakini madarasa 3,000 ya shule za msingi shikizi; si jambo dogo ndani ya madarasa hayo wananchi wa Wilaya ya Ubungo wanajua madarasa 151 yameenda katika Wilaya ya Ubungo; katika Jimbo la Kibamba madarasa 104 si kitu kidogo Mbunge wao ameyatembelea yote, ameyaona yote na kwa kweli namshukuru sana Mama Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaambiwa viko VETA 26 kwenye Wilaya zote na VETA kubwa za Kimkoa sita; si jambo dogo hizi zikikamilika wananchi wa kibamba katika eneo tuliopewa na Mheshimiwa Rais tunaenda kupata kwenye bajeti ya 2022/ 2023 VETA mpya kwa sababu zilizokuwa zinajengwa zote zitakuwa zimepata fedha na sasa zitakuwa zimekwenda mpya na sisi tunaomba wananchi wa Kibamba kupewa VETA nyingine. Hii ni kazi kubwa alizozifanya Rais na kufungua hizi fursa katika majimbo mengine. (Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Mtemvu kuna taarifa kutoka Mheshimiwa Jerry Silaa.
T A A R I F A
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa mzungumzaji na Bunge lako taarifa siyo Jimbo la Kibamba peke yake, kwenye Jimbo la Ukonga jumla ya madarasa 129 sawa na shilingi bilioni 2.5 zimejengwa na wananchi wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Mtemvu malizia mchango wako.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, hayo ndiyo mambo makubwa ya Mama Samia Suluhu Hassan - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais bora kabisa, Rais bora Afrika na duniani ndiyo maana hayo mambo unayaona katika kila jimbo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilikuwa nasema la maji; zimepelekwa shilingi bilioni 139.4 lakini ukweli wananchi wa Wilaya ya Ubungo Jimbo la Kibamba wanajua kwenye zile shida za maji tumeshasaini mkataba wa shilingi bilioni 5.4 pale Mshikamano. Sasa tunataka nini watanzania wanataka nini wanaenda kuyaona maji, shida ya maji inaenda kuisha katika muda mfupi mambo ya utalii Covid-19 ilituletea shida kwenye utalii lakini zimepelekwa fedha za kutosha karibia bilioni 90.4, sasa hivi mambo yanaenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, kwa kumaliza ni kweli tunalo ombi hapa la shilingi bilioni 693 kama nakisi sehemu ya pengo katika bajeti yetu tuliyokuwa tunaenda nayo ili kujazia tunaomba Waheshimiwa Wabunge mkubali kukopa kiasi hiki katika mkopo nafuu wa shilingi bilioni 693 ili mambo yazidi kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nikushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)