Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Salma Mohamed Mwassa

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu na pia napenda kushukuru Chama changu kwa kunipa jukumu hili kubwa, ni makini chenye maamuzi makini. Vilevile nikushukuru wewe Spika kwa kuliongoza Bunge lako kwa umakini kabisa wa hali ya juu. Nimshukuru Waziri wa Wizara hii mwenye dhamana kubwa na majukumu mengi, hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kuchangia hoja kwa kuishauri Serikali. Kwanza kabisa, naomba nijikite kwenye vifo vya akinamama wajawazito, hili ni tatizo kubwa sana. Akina mama 42 kwa siku ni watu wengi mno, hiyo inatutisha hata sisi wanawake wenyewe katika kutimiza hilo jukumu zito. Maana tunaona sasa uzazi ni probability, kujifungua ni tatizo na linaweza kupelekea maisha yetu kuwa hatarini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri atambue kwamba dhamana aliyopewa, Mheshimiwa Rais hakukosea kumchagua yeye mwanamke makini kwa maana anajua kabisa uchungu huu mzito wa jambo hili. Kwa sababu aliona kabisa Mpango wa Maendeleo ulivyofeli kupunguza hivi vifo vya akinamama ndiyo maana akatafuta mwanamke makini kama Mheshimiwa Waziri. Vilevile hakukosea kumtafuta professional ambaye ni Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla awe Naibu wako. Kwa hiyo, naomba mpambane kweli kweli kwenye hili tatizo la wajawazito, vifo ni vingi sana ukilinganisha na takwimu zilizopo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza tujiulize vifo hivi vinatokana na nini, kuna mambo mengi. Kwanza siyo tu vifaa tiba, wataalam lakini vilevile kuna mambo ya mimba za utotoni. Mimba za utotoni pia ni tatizo kubwa kwa sababu ukienda kujifungua ukiwa chini ya umri wa miaka 18 pia ni tatizo. Kwa hiyo, tuangalie tena tatizo hili kubwa. Pamoja na mikataba mbalimbali mliyoingia lakini vilevile tuliangalie hili tatizo la mimba za utotoni.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile saa nyingine vifo hivi vinatokea kutokana na handling ya wale watumishi wa afya. Nashauri kwamba Waziri aendeshe semina za mara kwa mara kwa watumishi wa afya jinsi ya kuwa-handle hawa wajawazito, wawe na special care kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kupunguza hivi vifo sijaona ikiongelewa mambo ya walemavu. Mwanamke mlemavu pia katika kujifungua anatakiwa umakini wa hali ya juu. Je, tuna hizo labour kwa ajili ya walemavu? Nashauri tuwe na vitanda special kwa ajili ya walemavu na labour special kwa wanawake walemavu kwa ajili ya kujifungua maana hilo pia ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nijikite kwenye ukatili wa kijinsia. Wengi wameongelea juu ya ukatili wa kijinsia na tumeongelea zaidi wanawake na watoto, lakini Wizara hii ni jinsia kwa ujumla. Naomba pia niongelee wanaume kwani nao wanafanyiwa sana ukatili wa kijinsia japo kwa idadi ndogo, lakini wao huwa hawana taratibu zile za kusema. Kiukweli wanaume wengi wanapigwa ila hawawezi kusimama hadharani wakasema kwamba tunapigwa kutokana na hizi sheria zetu za kiafrika, lakini wanapigwa na kufanyiwa mambo mengine mengi. Kwa hiyo, nimesimama pia kuwatetea wanaume pia na wao waangaliwe.
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Spika, naomba pia nijikite kwenye vifaa tiba na dawa pia ni tatizo sana hasa tukiangalia katika zahanati na vituo vya afya. Vituo vya afya kwa kweli ni tatizo havina vifaa tiba kabisa na dawa pia ni tatizo huko kwenye hivyo vituo vya afya. Kwa mfano, kama Jiji la Dar es Salaam Serikali imejitahidi kujenga vituo vya afya na zahanati kwenye kata mbalimbali lakini ni majengo tu hayana vifaa tiba wala wataam. Namwomba Mheshimiwa Waziri katika ziara zake aangalie sana hivi vituo vya afya ili kupunguza msongamano uliopo Muhimbili, Mwananyamala, Temeke na hospitali zote za kikanda kama hizo za Bugando. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niongelee huduma za madaktari bingwa. Huduma za madaktari bingwa mara nyingi unazipata kwenye referral hospital lakini huku kwenye vituo vya afya hakuna kabisa huduma za madaktari bingwa. Naona kingekuwepo kitu kama utaratibu maalum angalau daktari bingwa aweze kuzungukia hivi vituo vya afya hata kwa wiki mara moja. Kuwe na ratiba maalum ili mtu akitaka kumwona daktari bingwa basi asifikirie tu Muhimbili, Bugando au KCMC afikirie hata hivi vituo vya afya kwamba atakuja labda Alhamisi. Kwa hiyo, hizi huduma za madaktari bingwa ningeshauri zisambae zaidi kwenye vituo vya afya na zahanati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile katika ukurasa wa 92 wa hotuba, Mheshimiwa Waziri ameongelea maendeleo ya watoto. Watoto katika Taifa letu kwa kweli wana matatizo mengi especially ya kiafya. Naomba katika sera uangalie jinsi ya kuweza kujenga Hospitali za Taifa za Watoto pekee (National Children Hospital) nazo ziwe za awali mpaka referral kwa ajili ya kutibu watoto peke yake. Sambamba na vifo vya wajawazito lakini vifo vya watoto pia bado ni tatizo na tunatakiwa tuangalie kwa umakini sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niongelee Benki ya Wanawake. Benki ya Wanawake nayo ni tatizo kwa sababu iko zaidi mijini lakini hakuna wakala kama ilivyo hizi benki zingine za biashara, mfano Fahari Huduma kwa CRDB. Inatakiwa nayo iwe na huduma zake za kupeleka kwenye kata, mitaa na vijiji ili wanawake wengi wapate huduma za benki hii.
Mheshimiwa Spika, vilevile napenda kuongelea masuala ya utawala bora na hasa Wizara hii. Wizara hii inahudumia afya, wazee, watoto, kwa kweli ni Wizara ambayo ina majukumu mengi mno. Kwanza niwapongeze kweli kweli hawa Mawaziri wenye dhamana na namwomba Mheshimiwa Rais aiangalie tena hii Wizara yaani afya aiweke peke yake na hii jinsia angeiweka peke yake. Naona ameweka majukumu mazito mno halafu tena ukiangalia bajeti yenyewe nayo imeshuka kabisa. Ni vizuri Wizara hii ikajitegemea kwa maana ya Wizara ya Afya na ile jinsia ikawa sehemu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo yote nijikite kwenye kuongelea magonjwa haya yasiyoambukiza kama moyo, kisukari, figo, haya yote yanasababishwa na utaratibu mbaya wa maisha tunayoishi. Kwa hiyo, napenda kuishauri Wizara kwamba, tuwe na siku maalum ya kufanya mazoezi kama ilivyo ya usafi yaani siku hiyo tunafanya mazoezi toka asubuhi hadi jioni ili watu wapate hamasa kwamba tusile na kukaa kwenye magari, tuwe ni watu wa kufanya mazoezi na kuangalia mwenendo mzima wa maisha utakuwaje. Sasa hivi tabia ya mazoezi haipo kabisa, watu wanakula, wanaingia kwenye gari au wanapanda pikipiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niongelee vilevile maslahi ya watumishi wa Wizara ya Afya. Watumishi hawa kwa kweli ukiangalia Manesi na Madaktari saa nyingine wanaongea lugha chafu kwa sababu ya maslahi yao. Maana ukiangalia kwa mfano hospitali hizi za private hatuoni kule kama wanajibu hovyo kwa sababu wanalipwa mishahara mikubwa. Kwa hiyo, naomba Wizara pia iangalie maslahi ya hawa watu wa huduma ya afya, semina hizo waandae mara kwa mara na waangalie matatizo yao yanayowasibu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda pia kuongelea majukumu ya Maafisa Maendeleo ya Jamii. Maafisa hawa kwa kweli hawaangaliwi kama ilivyo kada nyingine. Mheshimiwa Waziri nakushauri uwatembelee hao Maafisa Maendeleo ya Jamii na uwaangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante.