Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ENG. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia hoja hii ya Taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kumshukuru sana Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya kuliongoza Taifa letu vizuri na kuwa msikivu katika changamoto mbalimbali ambazo zinajitokeza katika taarifa hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kumpongeza Mwenyekiti wetu wa Kamati Dkt. Rweikiza kwa kazi nzuri aliyofanya ya kutuongoza sisi wanakamati katika kutekeleza jukumu hili adhimu ambalo la uchambuzi huu wa sheria ndogo kazi ambayo tumepewa na Bunge lako tukufu na ambayo tumeifanya kwa ukamilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, madaraka ya kutunga sheria zote yanatolewa na Katiba yetu katika Ibara ya 4 na Ibara ya 64 ambayo Bunge lako tukufu limepewa lakini katika Ibara ya 97 ya Katiba hiyo hiyo imetoa fursa ya kukasimu madaraka hayo kwa Idara au mtu yoyote ambaye itaona inafaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, ningependa kuchukua fursa hii kuwapongeza hawa waliokasimiwa kufanya kazi hiyo ambayo wengi ni Mawaziri, Naibu Mawaziri pamoja na watumishi kwani wamefanyakazi hiyo kwa umakini. Wametuletea sheria nyingi sana sheria ndogo lakini ni sheria 11 tu ambazo zimeweza kuleta tashiwishi na kuweza kuleta uchambuzi huu hapa Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuzingatia vigezo vya uchambuzi ambao tumefanya katika Kamati yetu mimi nitajikita zaidi katika usahihi na ufasaha wa uandishi wa majedwali katika sheria ndogo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi sheria ndogo zinapotungwa lengo lake kuu ni kurahisisha utekelezaji wa sheria mama ili ziweze kueleweka vizuri zaidi na kuelezeka kwa urahisi zaidi. Hivyo ikiwa sheria hizo hazikuandikwa kwa usahihi na kwa umakini mkubwa, basi zinaweza zikaleta mkanganyiko katika utekelezaji wake au changamoto vilevile katika ulewela ulio sahihi.
Kwa hiyo, nitaangalia katika kurejea kanuni sahihi katika utungaji wake, lakini vilevile kuangalia kama kanuni hizo ambazo zimerejewa zipo au hazipo, lakini vilevile kama maudhui yaliyotakiwa kuwepo katika kanuni hizo ni yale ambayo yalikuwa yamelengwa na sheria mama.
Mheshimiwa Naibu Spika, wajibu uliokasimiwa wa kutunga sheria ndogo unaweza kupoteza maana yake kama haya majedwali ambayo lengo lake lilikuwa ni kurahisisha badala yake linakwenda kuzua changamoto au ugumu wa uelewa katika kanuni hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mifano michache; katika sheria ndogo ya The Electricity Electrical Installation Services Rules ya mwaka 2022 ambayo imetungwa kupitia Sheria ya Electricity Act, Sura ya 131 kuna majedwali ambayo yamewekwa mle, katika jedwali la nne la kanuni hiyo linamruhusu mwenye leseni ya uunganishaji umeme akishaunganisha basi ampatie mteja wake cheti cha kuonesha nini amefanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, maudhui ya kanuni hiyo yanataka huyo muunganishaji atoe cheti hicho na kuelezea kila kitu kilichopo na yanasema kwamba muonekano wa cheti hicho ni kama ambavyo umeonekana katika jedwali hilo. Ukiangalia jedwali hilo muonekano wa cheti hicho haupo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unakuta sasa kanuni hii japokuwa imetoa mwelekeo kwamba nini kifanyike, lakini cheti ambacho kinatakiwa kitolewe au muonekano wake haupo katika kanuni hiyo. Kwa hiyo, badala ya kuwa imesaidia imeleta tena mkanganyiko mkubwa zaidi kwani imesema toa cheti kama kilivyooneshwa katika jedwali na kwenye jedwali cheti hicho hakipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine ambao nautoa ni huu wa kanuni ya The Copy Rights Enabling Rights, Licensing and Rights to Benefits Re-Sells Regulation ya mwaka 2022; kanuni hii nayo imetokana na Sheria ya The Copy Right and Enabling Rights Act, Sura Namba 218.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jedwali la sheria hii limetoa mfumo wa kutoa mgawanyo wa mapato, wao wameita distribution rules for public performance and broadcasting, lakini utakuta kwamba kanuni ambayo imetungwa hapo, maudhui yake yanatokana na kifungu cha 29 cha sheria hiyo. Lakini ukiangalia maudhui ya sheria na kanuni iliyotungwa ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo, unakuta sasa badala ya kanuni hiyo kwenda kurahisisha utekelezaji wa sheria hiyo, inakwenda kuleta changamoto kubwa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, umakini mkubwa unatakiwa na tunashukuru sana uongozi wa Mwenyekiti wetu ambaye alituongoza vizuri katika kupitia kanuni hizi ili kuhakikisha kwamba hatuleti mchanganyiko mkubwa na wajibu uliokasimu kwa hawa kutunga sheria ndogo unatekelezwa kwa usahihi na kwa umakini mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine uko katika Sheria ya The Tanzania Shipping Agencies Performance Benchmark Regulations ya mwaka 2022; kanuni hii imetokana na The Tanzania Shipping Agencies Act, Sura Namba 415. Katika kanuni hii, kanuni ya 16 inayohusu utolewaji wa notisi, notisi ya ukubalifu yaani compliance notice ambayo ni kitu muhimu kwamba ameridhia au amefanya kitu ambacho kinatakiwa kufanywa.
Mheshimiwa Naibu Spika, imeelekeza kuwa wakala wa meli atatoa notisi kwa namna ilivyofafanuliwa katika jedwali la tatu. Kwa hiyo, unakuta kwamba jedwali limetamkwa vizuri kwamba notisi itatolewa kwa mfumo huu. Ukienda kwenye jedwali hilo, unakuta kwamba jedwali hilo la tatu halipo. Sasa unakuta huku umeelekezwa uende jedwali namba tatu ukapate mwelekeo wa hiyo notisi, lakini kwenye utekelezaji utakwama kwa sababu jedwali hilo halipo. Kwa hiyo, hiyo italeta usumbufu katika utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine ambao naweza kuutoa ni kuhusu muingiliano au mchanganyiko unaoletwa na lugha katika sheria; hHii nitatolea mfano katika The Mining Government Mineral Warehousing Regulations ya mwaka 2022 ambayo inatokana na The Mining Act, Sura namba 123.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jedwali hilo utakuta linakudai fomu namba tatu ambayo imetungwa kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili, lakini ukiangalia usahihi wa maneno katika fomu ile Kiswahili na Kiingereza unakuta kwamba maana hazilingani au hazishabihiani. Kwa hiyo, unakuta kwamba hii inaleta changamoto katika ule utekelezaji, nini kifatwe, tafsiri ya Kiingereza au tafsiri ya Kiswahili?
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta kwamba katika jedwali hilo hilo, fomu nyingine zimetungwa kwa lugha moja tu ambayo ni Kiingereza, basi Kamati yetu imeona kwamba ni muhimu kabisa kwamba lugha inayotumika ieleweke vizuri na tafsiri zishabihiane ili kutoleta mchanganyiko katika utekelezaji wa hayo mambo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii na naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)