Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Sheria ndogo kwa jina lake zinaweza kudogoshwa, zinaweza zikachukuliwa kama kanuni na taratibu ambazo labda hazina umuhimu sana, lakini kiuhalisia sheria ndogo ndizo zinazoendesha maisha ya kila siku ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nianze kwa kuishukuru Serikali na mamlaka zilizokasimiwa kwa kutunga sheria ndogo. Kwa kweli kama wangekuwa wanatumia vibaya mamlaka hayo, pangekuwa pana mtifuano mtaani. Tunaamani na utulivu kwa sababu mamlaka zilizokasimiwa kutunga sheria ndogo zinatendea haki mamlaka hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria ndogo zimebeba mstakabali wa haki za watu, ndizo sheria ambazo zina-define haki na usawa wa watu katika jamii, ndizo sheria zinazoleta muongozo katika haki za msingi ikiwemo haki ya kupata kipato, haki ya kupata ujira, haki ya usalama na faraha na haki ya kushirikiana na watu wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, haki hizi hususan haki ya ajira na ya kupata kipato ambazo ni muhimu kwa maisha ya binadamu ya kila siku na ambazo ni haki za Kikatiba, ni za muhimu sana ziangaliwe pale ambapo sheria ndogo zinatungwa. Kwa sababu ndizo ambazo zinagusa uhalisia wa maisha ya watanzania ya kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria ndogo mchakato wake ni tofauti na sheria mama. Sheria ndogo zinapotungwa na mamlaka zilizokasimiwa mamlaka hayo na Bunge, zinaanza kutumika kabla hazijaletwa Bungeni kupitiwa na Bunge na ndiyo maana ni muhimu sana kwa mamlaka zilizokasimiwa madaraka hayo kuhakikisha sheria ndogo zinazotungwa zinalinda haki na ustawi wa Watanzania, lakini vilevile zinazingatia masharti ya maendeleo katika jamii zetu za Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mojawapo ya changamoto ambazo zimesemwa na Kamati ni sheria ndogo kutokuzingatia masharti ya uhalisia katika jamii, yaani zinatungwa bila kuangalia uhalisia wa maisha ya Watanzania. Jambo hili limekuwa likileta changamoto za mara kwa mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, na napenda nianze kwa kusema kuhusiana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2025. Dira ya Maendeleo ya Tanzania inasema tutajenga uchumi imara, anuai, himilivu na shindani ambao utazingatia mabadiliko ya masoko na teknolojia. Kwa hiyo, lazima sheria ndogo zinazotungwa ziende kwa mlengo huu ili kuhakikisha ya kwamba Taifa letu linapata maendeleo kwa kadri ya tulivyojiwekea.
Mheshimiwa Naibu Spika, na hapa napenda nielezee masuala ya sheria ndogo yanavyoshika masuala ya teknolojia ambavyo siyo sahihi. Napenda nielezee kanuni elekezi za LATRA ambazo zimesababisha kampuni za teknolojia kama Bolt na Uber kusitisha huduma zake hapa nchini kwetu Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni elekezi za LATRA hazikuwa sahihi. Nasema hazikuwa sahihi kwa sababu zinaenda kinyume na Dira ya Maendeleo ya 2025, lakini pamoja na hilo, LATRA hawakuwa na mamlaka ya kutunga kanuni zile ambazo zinasababisha kampuni za ubunifu na teknolojia kusitisha biashara zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, LATRA inahusiana na ku-regulate usafiri siyo masuala ya teknolojia. Bolt na Uber siyo kampuni ya usafirishaji, ni kampuni ya ubunifu na teknolojia. Kwa hiyo, LATRA hawakuwa na mamlaka ya kutunga kanuni ambazo zinaenda kufungia ubunifu wa teknolojia ya Uber na Bolt. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema haya kwa sababu masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika nchi yetu yametapakaa. Kisera yako Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, lakini kiutendaji kwa kiasi kikubwa yako Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Sasa LATRA walipata wapi mamlaka ya kugusa masuala yanayoendana na teknolojia hali wakijua mamlaka yao ni kwenye masuala ya usafirishaji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na hapa napenda niishauri Serikali yangu, na ushauri huu niliutoa mwaka jana; masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu yameparanganyika, ni wakati sasa tuwekee uratibu ili kuhakikisha wabunifu hawa hawawi frustrated.
Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni za Uber na Bolt kama zilivyo kampuni zingine za ubunifu, ni kampuni za hiyari kujiunga, mtu halazimishwi kujiunga, na kampuni hizi zinagusa maslahi ya pande mbili; zinagusa maslahi ya wananchi na zinagusa maslahi ya madereva.
Mheshimiwa Naibu Spika, LATRA kwenye kanuni zao walisema wanafungia Uber na Bolt kwa sababu wana-charge madereva commission ya asilimia 20 mpaka 25. Wanataka Uber na Bolt wa-charge commission isiyozidi asilimia 15, sawa labda hoja ipo. Labda hoja ipo, lakini LATRA baada ya Uber na Bolt kusitisha huduma ndiyo wanasema tutakaa nao mezani. Jamani kila siku tunasema hapa, nyenzo namba moja ambayo inachagiza ajira duniani kote ni nyenzo zinazoendana na sayansi na teknolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweka commitment ya ajira milioni 10. Ajira hii kwa urahisi itapatikana kwa nyenzo za sayansi na teknolojia, siyo popote pale. Sasa LATRA walitakiwa kukaa mezani na kujadili kabla ya kufunga na siyo wamefunga ndiyo wanasema watajadili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii zaidi ya vijana 100,000 ambao walisema walikuwa wanawatetea wako mtaani. Ile asilimia 15 wanapata? Hawapati, wameanza upya kwa applications nyingine. Sasa tunaenda mbele, tunarudi nyuma? Wale waliokuwa wanawatetea hawafanyi biashara, wananchi ambao walikuwa wanapata ahueni na wenyewe mambo yao ni magumu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ngoja niwaambie, ile shilingi 30,000 ambayo labda mwananchi alikuwa analipa akitoka Mwenge kwenda Posta, alikuwa analipa kwa shilingi 10,000. LATRA unaumia nini mwananchi akilipa shilingi 10,000? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu nia yetu, nia ya teknolojia ni kurahisisha maisha kwa wananchi. Mwananchi maisha yake yamerahisika sasa sisi tunaumia nini? Kama kulikuwa kuna jambo si wanakaa mezani tunalitatua? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, uliangaliwa upande mmoja, upande wa wananchi ambao maslahi yao na haki zao ambao maisha yao yamerahisika hawakuangaliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi napenda niishauri Serikali yangu wawashauri LATRA, kanuni hizi wazivute nyuma. Kwa kweli ni kanuni ambazo hazina maslahi kwa madereva wala kwa wananchi ambao walikuwa wananufaika kwa huduma ya Bolt na Uber. Lakini vilevile tuangalie na document zetu kama dira za maendeleo. Kwa sababu kama tukiwa tunatunga kanuni kama hizi kwakweli inakuwa hatuwatendei haki Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi Kampuni za Uber na Bolt hizi siyo teknolojia zao kwa hapa Tanzania, wananunua hakimiliki. Kwa hiyo, na wenyewe wanazilipia, walipaswa kusikilizwa kwenye commission wanayoipata asilimia ngapi ni faida yao wenyewe binafsi? Investment yao wanailipiaje? Lakini siyo kuwafungia tu, kwa sababu hizi siyo teknolojia zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mfano wa nchi nyingine, kwa mfano ukilipa shilingi 70,000 kama nauli ya Bolt ama ya Uber kuna charge nyingine ambazo zinaenda kwa mwananchi ambazo zinakaribiana na nusu ya ile bei karibia shilingi 30,000. Lakini kwa wenzetu hizi Uber na Bolt zinaendeshwa na wale wamiliki wa gari wenyewe, yaani kama mimi nina IST yangu ndiyo najisajili naendesha mwenyewe. Kwa hiyo, ile faida ya moja kwa moja naipata mimi mwenyewe. Tofauti na sisi, watu wengi ambao wanaendesha Bolt siyo wamiliki, ni watu ambao wameenda kuomba ajira kwa wamiliki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa hapo ndiyo changamoto inapoanzia, kwa sababu ule ujira inabidi waugawanye ambao siyo tatizo la Uber. Kwa hiyo, kama mtu hanufaiki siyo tatizo la Uber, ni tatizo la mfumo wenyewe uliopo. Kwa hiyo, kanuni hizi zilitungwa kwa kuangalia juu juu siyo kwa kufanya utafiti wa kina na kuhakikisha kwamba tunalinda makundi yote. Wale vijana ambao wamejiajiri, lakini vilevile na wananchi ambao wanatumia huduma zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, LATRA ilibidi wajielekeze kwenye masuala ya muhimu kabisa na kanuni ambazo zinashika mustakabali wa Taifa, kwa mfano, suala la ving’amuzi kwenye mabasi. Ving’amuzi vilivyofungwa kwenye mabasi havidhibiti mwendo, vinatoa tuu alert kwamba speed imezidi, yaani baada ya pale dereva anakanyaga mwendo kama kawaida. Vinaishia kupigia abiria tu kelele gw’igw’igw’i kwenye mabasi, havidhibiti speed. Yaani siku hizi dereva speed inazidi 80 anakanyaga mwendo king’amuzi kinalia tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ving’amuzi vilivyofungwa kwenye mabasi havidhibiti mwendo. Labda tufikirie upya kanuni ambazo tumezitunga. Je, tuna ulazima wa kuweka ving’amuzi ambavyo vinadhibiti mwendo ambavyo mtu akizidi 80 gari yenyewe ina-stabilize palepale havizidi. Haya ndiyo masuala ya msingi kabisa ambayo mamlaka tulizozipa mamlaka zinapaswa kuyaangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siku hizi teknolojia zimekuwa, kwa hiyo lazima tuyaangalie masuala haya kwa umuhimu sana, lakini vilevile control systems zinafanya nini? Kwa sababu dereva anaongeza speed lakini no control systems. kwa hiyo, tuangalie ving’amuzi, lakini vilevile TBS hawakuthibitisha hivi ving’amuzi, walisema havina ubora lakini vimefungwa kwenye mabasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kweli mimi napenda kuhimiza mamlaka ambazo Bunge imezikasimu mamlaka ya kutunga kanuni kwa niaba yake lazima zitunge sheria ndogo kwa ufanisi mkubwa na kwa kuzingatia haki, usawa na maslahi ya Watanzania wote kwa ujumla. Kwa kweli napenda kuishauri Serikali masuala haya, kanuni hizi elekezi za LATRA ziangaliwe kwa jicho la upekee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi. (Makofi)