Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Sita na Mkutano wa Saba wa Bunge pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa kwenye Mkutano wa Tatu na Mkutano wa Nne wa Bunge

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Sita na Mkutano wa Saba wa Bunge pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa kwenye Mkutano wa Tatu na Mkutano wa Nne wa Bunge

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kidogo katika suala hili muhimu sana la sheria ndogo ambazo kiuhalisia ndiyo zinazowaongoza wananchi wetu katika kuishi katika maisha ya utawala bora na maendeleo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze Mawaziri, lakini zaidi nimpongeze sana Rais wangu Mama Samia kwa jinsi ambavyo muda wote amekuwa akiwaza maendeleo ya Watanzania na maisha bora kwa Watanzania. Rais wetu amekuwa halali, hapumziki, kuhakikisha kwamba wananchi wetu tunazidi kupata maisha bora na kwa kweli tuendelee kumuombea Mungu ili atimize lengo lake la kufanya Watanzania tuwe tuna maisha bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria ndogo zimetungwa au zipo kwa ajili ya kufanya sheria mama ambazo zinatungwa na Bunge pamoja na kanuni zinazotungwa na Mawaziri ziweze kufanya kazi kiuhalisia katika jamii. Kwa hivyo, sheria hizi zinapokuwa hazina uhalisia zinafanya maisha ya wananchi wetu kuwa magumu na pengine kuingia kwenye hatia bila kukusudia au kuingizwa kwenye hatia au kurudishwa nyuma kimaendeleo. Kwa hiyo, Kamati inaposema kwamba sheria hizi ndogo marekebisho yake yafanyiwe mapema tena kwa time line ni jambo la muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano sheria kwenye TS No. 105 ya tarehe 25 Februari, 2022 sheria inayotoa mamlaka The Tax Administration Act Sura Na. 438 ambayo inaipa sheria ndogo The Tax Administration of Tax Ombudsman Service Regulation ya 2022 kanuni ya sita inakataza mtu aliyeajiriwa kuwa mchunguzi wa kikodi wa masuala yote ya matatizo ya kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, unafahamu kwamba wafanyabiashara wamekuwa na matatizo mengi kuhusiana na kodi, sasa yuko mtu hapa anaitwa ombudsman ambaye kazi yake ni kuchukua yale matatizo yote ya wafanyabiashara halafu anapochukua haya matatizo anayakabidhi kwa Waziri, ili Waziri aweze kuchukuwa hatua katika sehemu zinazohusika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu huyu anaambiwa kwamba kwa kufanya kazi hii asifanye kazi nyingine yoyote inayompatia kipato cha mshahara anapofanya kazi hii. Kazi nyingine yoyote, lakini kanuni hii wala haijaeleza kwamba kazi zipi labda zinazoingiliana na kazi yake ile ya kupokea matatizo ya kikodi, imemzuia moja kwa moja. Kiuhalisia unaona kabisa kanuni hii haitekelezeki ina maana huyu mtu yaani anakuwa amekaa tu yani hata kuandika write up labda amuandikie mtu afanye biashara haruhusiwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kanuni hapa ailezi zile kazi hasa ambazo zina muingiliano na kazi yake ya kupokea matatizo ya kikodi imeacha tu wazi. Kwa hiyo tunaposema kanuni kama hii irekebishwe maana yake inampa mtu huyu utata, aidha, atakuwa lofa zaidi au kiuhalisia atafanya kazi kinyume kwa sababu kanuni haijamueleza kwamba kazi zipi hasa zinazoingiliana na kazi yake ya kupokea matatizo ya kikodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hapo hapo katika kifungu kinachohusu Administration Tax Ombudsman Service Complain Procedure Regulations of 2022 ambazo zimetungwa chini ya kifungu cha 28(g) kwamba huyu mtu akisha collect matatizo anamkabidhi Waziri, Waziri aweze kutoa maelekezo kwenye mamlaka kwa mfano TRA kuchukua hatua juu ya matatizo ya kikodi ambayo ameyapokea kutoka kwa wafanyabiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kanuni haijambana Waziri ndani ya muda gani aweze kutoa hayo maelekezo, kwa hiyo, Waziri anaweza akachukuwa akatia kwenye draw akaendelea na shughuli zake zingine, mwezi, miezi, mwaka wakati tatizo lile la kikodi kwa wale wafanyabiashara linawasumbua, pengine limefanya wengine wanafilisika kwa sababu tayari sheria zile zinaendelea kutumika wakati marekebisho, yanasubiliwa lakini sheria zinaendelea kutumika kwa sababu zimeshaanza kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kifungu hakijambana Waziri kwamba unapaswa sasa umeshapokea haya matatizo toa maelekezo ndani ya miezi mitatu, ndani ya mwaka. Kwa hiyo tunaposema kwamba marekebisho haya yafanyike haraka na ninashukuru kabisa kwamba Kamati imetoa mpaka muda maalum kwamba ndani ya muda fulani marekebisho yawe yamefanyika kwa sababu hivi vitu vinawaumiza watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mtu analalamika labda anatozwa kodi kubwa kutokana na biashara anayofanya Waziri ameshapelekewa, ametia kwenye draw, hakuna kifungu kinambana, mwaka unaisha, mwisho mtu anafilisika. Kwa hiyo, utaona kabisa kwamba ni kifungu kidogo sana, lakini kimesababisha maisha ya watu wengi kuharibika kama hakijafanyiwa marekebisho ndani ya wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo wamesema wenzangu hapa zipo sheria kama hizi kwenye halmashauri, kwa mfano halmashauri inakuambia sasa utafuata kalenda kipindi cha kulima mahindi kimefika utalima mahindi, sasa mtu unakuta ana shamba la umwagiliaji, ana maji anataka kulima nyanya kalenda ya halmashauri inamwambia sasa unatakiwa ulime mahindi. Sasa huyu mtu unamtia umaskini, pengine ndio kipindi ambacho nyanya zinahitajika kwa wingi kalenda haisemi inakuambia tu ni kipindi cha kulima kitu fulani, kwa hiyo unakuta ni sheria ndogo imetungwa kwa lengo zuri, lakini kwa sababu haina uhalisia inasababisha maishi magumu kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunaposema kwamba kanuni hizi zifanyiwe marekebisho haraka ni mambo ambayo yanawagusa wananchi, halmashauri inasema utafuga kwa idadi maalum, sasa unampangia mtu utajiri! Yaani mtu ana uwezo wa kufuga ng’ombe 1,000 wewe unataka unamwambie afuge ng’ombe wanne kwa hiyo sasa ina maana sheria sasa inaanza kubana watu wasitajirike wakati sisi tunataka watu watajirike, nchi ipate kodi na mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo utaona hizi sheria ndogo zisipoangaliwa vizuri zinaweza zikasababisha umaskini ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo, Maazio ya Kamati yanaposema sasa marekebisho yafanyike haraka na inaweka na muda tujue kabisa tunagusa mambo ya wananchi kuweze kuishi maisha bora waweze kupata utajiri na nchi iweze kupata maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nilitaka nisisitize hilo kwa kuunga mkono hoja kwamba hizi sheria ndogo ndio engine ya kufanya sheria mama zifanye kazi, ndio engine ya kufanya kanuni zile za Mawaziri zifanye kazi na niwaombe basi na hawa Mawaziri wanapotunga hizi kanuni wawe wanakumbuka kabisa wanaenda kugusa maisha ya watu na wasitoke nje ya sheria mama ambayo inakuwa imetungwa humu ndani ya Bunge na mara zote sheria zinazotungwa humu haziendi kuwakandamiza wananchi bali kuwaletea maendeleo katika nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba niunge mkono hoja ahsante. (Makofi)