Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Sita na Mkutano wa Saba wa Bunge pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa kwenye Mkutano wa Tatu na Mkutano wa Nne wa Bunge

Hon. Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Sita na Mkutano wa Saba wa Bunge pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa kwenye Mkutano wa Tatu na Mkutano wa Nne wa Bunge

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Government Chief Whip ninaomba nichukue fursa hii na mimi kusema maneno machache na hasa nikizungumza pia kwa upande wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ni utamaduni ulio mzuri kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia afya njema na kutuwezesha kuwa hapa na tunaendelea na ajenda katika mkutano huu wa Bunge. Lakini naungana na Waheshimiwa Wabunge pia waliochangia awali bila kusahau kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa kazi nzuri anazozifanya na hasa katika kuhakikisha kwamba ameendelea kuwa mzalendo mwenye maono ya kuliongoza Taifa letu na kuendelea kutoa miongozo mbalimbali kwa viongozi na hata sisi Mawaziri ili kuhakikisha kwamba tunakuwa na ustawi wa taifa letu na maendeleo endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kumpongeza sana Mwenyekiti wa Kamati Dkt. Jasson Samson Rweikiza kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye Kamati yake, lakini pia akisaidiana na ndugu yangu Kilumbe Shabani Ng’enda ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati, lakini vilevile wajumbe wa Kamati hii ya Sheria Ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kazi inayofanywa na Kamati hii ukiangalia juu juu unaweza ukaona ni kazi ndogo, lakini ni kazi kubwa sana na inatija kubwa kweli kwa ustawi wa Taifa letu. Kwa hiyo, nawapongeza sana wajumbe wote wa Kamati kwa kazi kubwa mnayoifanya katika kuhakikisha kunakuwa na utawala bora, haki na usawa katika utendaji wa kazi ndani ya Serikali na katika kusimamia maslahi ya Taifa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninadhani ninawiwa pia kuwapongeza sana watumishi wa Serikali na hasa ambao ni wanafanya kazi kwenye Kitengo cha Sheria wale ambao wamekuwa wakihakikisha kwamba wanatekeleza wajibu wao sawa sawa kwa kufuata sheria, taratibu, Katiba na kanuni zilizowekwa ili kutunga sheria ndogo ambazo zinahakisi mwenendo mzima wa usimamizi wa majukumu ya kila siku katika maeneo yao. Kwa kweli tunawapongeza sana watumishi hao kwa sababu wanasheria wetu katika maeneo mbalimbali kama ilivyosemwa na Kamati hapa kwamba kuna sheria nyingi ambazo zimekuwa zikipelekwa kwenye kamati hii ya sheria ndogo lakini unakuta si sheria zote ambazo zimekuwa na matatizo makubwa.

Kwa hiyo, kama kuna sheria ambazo hazina matatizi ina maana kuna timu ya watumishi wa umma wanasheria ambao wanafanya kazi zao kwa ufasaha ni lazima tuwapongeze sana hao kwa kazi hizo na tuwaombe wale ambao wamekuwa wakiwa wakijirudia kuwa na makosa ya uandishi wa sheria na makosa mengine kujirekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inawasilisha nakala ya matoleo ya Magazeti ya Serikali hapa Bungeni na hiyo inapelekea kuwa na mjadala kupitia sheria ndogo na hasa kwa msingi wa Kikatiba wa kukaimu na kukasimisha madaraka haya ya utungaji wa sheria kwa taasisi mbalimbali kupitia ndani ya Serikali na ninaomba nichukue nafasi hii kuungana na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwamba tumepokea maelekezo ya Kamati kama yalivyowasilishwa kwenye taarifa hii ya Kamati na sisi kama Serikali tunakila sababu ya kuyafanyia kazi na kwa maana hiyo basi kwa niaba ya Chief Whip - Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ninaomba nitoe maelekezo yafuatayo kwa watendaji wote wa Serikali ambao wanahusika na maelekezo haya na maazimio haya ambayo yako ndani ya hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ni kuhakikisha wanatii na kutekeleza agizo la Kamati la muda uliowekwa kuhakikisha kwamba sheria ndogo zote zenye dosari zinarudishwa hapa Bungeni mapema ili ziweze kukaguliwa na kuondolewa dosari zilizokuwepo. Kwa hiyo, eneo hilo ni lazima mamlaka zote zilizokasimiwa utungaji wa sheria hizo ninaomba sana wafuatilie mjadala huu na wapokee maelekezo ya Serikali na wahakikishe wanatekeleza jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili ninaomba niendelee kuziagiza na kuzisisitiza mamlaka zote zilizokasimiwa kazi hii ya utungaji wa sheria ndogo kuhakikisha kwamba wanazingatia Masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ilivyopendekezwa na Kamati na kuendelea kuhakikisha kwamba wanapunguza dosari zinazoonekana katika sheria ndogo zikigongana na matakwa ya Kikatiba kwa hiyo jambo hili pia lizingatiwe sana na timu ya wanasheria wetu na mamlaka zilizokasimiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika mjadala tumeona hapa zimesemwa baadhi ya sheria ambazo kwa kweli zinakiuka misingi kwa namna moja ama nyingine ya haki ambazo zingeweza kuwa ni haki za msingi kwa Watanzania na wananchi wanazotumia sheria hizo ndogo. Kwa hiyo tunaendelea kuziagiza hizo mamlaka kuzihakikisha sheria ndogo zinazoenda kurekebishwa zikaandaliwe na kutengenezwa zikiwa na uhalisia wa maisha ya Watanzania katika kuwezesha maisha ya Watanzania kuakisi sheria mama ambazo zimetungwa na siyo kuleta migogoro na migongano ya utendaji wa kazi wa sheria katika maeneo mbalimbali na hapa leo tumeona sheria ndogo za LATRA zimesemwasana hapa ndani na ni kama vile zilienda kuibua sintofahamu katika utekelezaji wake katika jamii. Kwa hiyo, tunaomba marekebisho hayo yatakapofanyika yahakikishe kwamba hayaibui tena migogoro ya namna hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile tunaendelea kuwakumbusha mamlaka zetu kuhakikisha wanapotunga hizo kanuni ama sheria ndogo ziwe na uhalisia wa mambo ambayo yanaendana na hali halisi ya uchumi wa nchi kwa Taifa letu na tumesikia hapa baadhi ya Wabunge wakitukumbusha kwamba sasa hivi tumeamua uchumi wa taifa hili uwe ni uchumi wa kidijitali tunaenda kwenye mitizamo ya ki-TEHAMA, kwa hiyo kila sheria ambayo tunaitunga ni lazima itakuwa na component hiyo ya ki-TEHAMA, kwa hiyo na sheria ndogo ziakisi mwelekeo wa uchumi wa Taifa letu ambao tunao kwa sasa. Lakini tunaendelea kuagiza na kuwakumbusha kuhakikisha wanatunga sheria ndogo zenye usahihi na ufasaha wa uandishi wa majedwali ya sheria ndogo na hasa kurejea kanuni husika na sheria husika katika kuyatengeneza majedwali hayo, jambo hilo pia watakapokuwa wanarekebisha sheria hizo ndogo wahakikishe wanazingatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine tunaendela kuwakumbusha kuzingatia misingi ya uandishi wa sheria ambayo imewekwa katika taratibu mbalimbali ambazo zinatumika katika uandishi wa sheria nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, na jambo lingine tunaendelea kuwakumbusha kuwasiliana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kila eneo ambalo lina matatizo wawasiliane na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kupata miongozo na kuhakikisha kwamba matatizo haya ya uandishi wa sheria ndogo ambazo zimeshindwa kuakisi sheria mama na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jambo hili linaondoka kwa haraka na ikiwezekana tuendelee kupunguza sheria zenye makosa mengi zinapowasilishwa hapa ndani ya Bunge lako tukufu kwa kupitia Kamati ya Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimalizie kwa kusema kwamba Serikali itaendelea kujitahidi kusimamia taasisi zote zinazohusika na mamlaka hii ya uandishi wa sheria ndogo ili kuhakikisha kwamba utawala wa sheria unachukua nafasi yake ndani ya nchi yetu, lakini utawala bora pia unachukua nafasi yake ya kutosha ndani ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunaendelea kulihakikishia Bunge lako tukufu kwamba kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tupo tayari kushirikiana kwa karibu na Kamati ya Sheria Ndogo kuhakikisha kila jambo linakwenda sawasawa kwa ustawi wa nchi na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawapongeza tena Kamati ya Sheria Ndogo na tunawahakikishia kwamba tutaendelea kushirikiana nao. Ahsante sana naomba kuunga mkono hoja ya Kamati hii ya Sheria Ndogo. (Makofi)