Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kaliua
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nianze tu kwa kuunga mkono hoja iliyotolewa na Mheshimiwa Ezra.
Mheshimiwa Spika, naomba tu niwasilishe kwamba, kwa kweli katika huu muda wa wiki mbili kelele zimekuwa ni nyingi sana kwa wanafunzi ambao wamekosa mikopo na kwa wanafunzi ambao wamepata kiwango cha chini kabisa cha mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja yangu nilikuwa najiuliza maswali mepesi tu kwamba, Serikali imefanya vizuri sana kwenye kujenga sekondari, tena nyingi karibu kila kata na pengine kata zingine zina sekondari mpaka tatu. Pia Serikali imefanya vizuri sana kwenye vyuo, kwa maana ya ujenzi na kila kitu, lakini ongezeko la wanafunzi ambao wanasoma limekuwa ni kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa haya yote, nimeona kuna gap ambalo Serikali haijafanya vizuri. Serikali haijafanya vizuri kwenye eneo hili kwamba huku kote wametoka vizuri. Tumekuja vizuri, lakini shida kubwa imekuja kutokea volume ya wanafunzi ambao wanaingia vyuo vikuu ni kubwa sana, ni lazima tuongeze Bajeti. Kwa hiyo la kwanza, naishauri Serikali ije na mkakati hapa Bungeni wa kuhakikisha ina-cover wale wanafunzi wote wanaofaulu vizuri, wasibaki nyumbani.
Mheshimiwa Spika, hapa tunatengeneza bomu. Huwa najiuliza hata vigezo eti wanasema kwamba huyu alisoma shule ya private, labda alikuwa analipiwa milioni mbili, milioni mbili na kadhaa. Sasa nikawa najiuliza wazazi hatuelewi kama kuna wengine wanafilisika, hatuelewi kama kuna wazazi wengine wanastaafu, kama tunaelewa kwamba wapo wazazi ambao uwezo wao unapungua ni kwa nini tunawawekea masharti magumu kiasi hiki? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababau mimi leo inawezekana nina uwezo, kesho kutwa nisiwe na uwezo wa kifedha, kwa hiyo mtoto wangu abaki nyumbani? Kwa mfano, ongezeko tu la takwimu za jana, Tabora tumekwenda kwenye milioni 3.3, kitu ambacho lazima tubadilishe, lazima tu allocate hizi resource vizuri.
Mheshimiwa Spika, nashauri hapa kwenye jambo lingine kubwa tu. Bodi ya Mikopo ni lazima watoke kwenye boksi walilojifungia, lazima wawe na uwezo wa kukaribisha private sectors kwenye uwekezaji wa mikopo kama mabenki. Ni kwa nini tusiwape mabenki angalau ideas na vigezo ili wawe na uwezo wa kutusaidia? Ni kwa nini tujifungie kwamba ni Serikali tu, wakati tunaelewa kabisa nchi zinazoendelea zinakwenda zaidi ya hiki ambacho tunachokifanya.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba wote humu tumepewa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Ndiyo maana kuna mwingine alijaribu kuitoa, tulipopewa ile Ilani ya Chama Cha Mapinduzi hatuwezi kukubali wananchi wetu, wanafunzi ambao wapo kwenye majimbo yetu waendelee kuteseka kwa kukosa mikopo, sasa mwisho wa yote tutaulizwa haya, Ilani ilitekelezwaje hapa utasemaje? Nilijenga tu madarasa halafu nikaacha watoto maelfu wamekaa nyumbani. Wamekaa huku bila kuwasaidia haiwezekani!
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naiomba Serikali itoke kwenye boksi ije na kuhakikisha wanafunzi wote ambao wamefanya vizuri wanakwenda. Vilevile kigezo kingine ni zile taaluma ambazo wanakwenda, yaani mtu ambaye anakwenda Udaktari unampa asilimia ishirini, sio hali ya kawaida jamani tuelewe kabisa kuna mabadiliko ya tabia ya nchi, leo mkulima analima, kesho inawezekana asipate mazao. Sasa kama asipopata mtoto wake ameshayumba ulimpa asimilia ishirini. Tunajenga mazingira gani kwa hawa watoto?
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, kwanza nirejee kusema tu, kama Serikali mkakati tunauhitaji na mkakati huo ujadiliwe kwa kina, lakini kama tulivyofanya kwenye sekta nyingine. Tumefanya vizuri tulipoyumba kidogo kwenye mafuta kukawa na mambo mazuri yakaja, tukafanya na maeneo mangine ambayo wameshauri Waheshimiwa Wabunge wengine. Hivyo, nashauri hili kwetu ni dharura kwa sababu simu tunazopokea hapa nina message ya bwana mmoja anaitwa bwana Bada katoka kutuma message hapa, Mheshimiwa Mbunge unatusaidiaje na kadhalika. Sasa ni maelfu ya watu.
Mheshimiwa Spika, kelele zinakuwa nyingi. Ukikuta Jimbo lina watu karibu laki tano, wazazi na sisi kule ni mafundi wa kuzaa, haya niambieni hizo kelele zinakuwaje? Haiwezekani hivi, ni lazima tuwasaidie watu na ndiyo kutekeleza kwenyewe Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Kwa hiyo suala la ilani tuliyopewa kuinada lazima itekelezwe ili huko baadaye pia mambo yaweze kukaa vizuri sana.
Mheshimiwa Spika, nimalizie tu kwa kusema kwamba ni vizuri hawa watu wa Bodi ya Mikopo wakubali mabadiliko, kuna malalamiko bado yanakuja tu, yaani malalamiko wasijione Miungu watu, wanatakiwa kuwa na changes. Utumishi wa sasa hivi ni utumishi wa service delivery, kauli nzuri na mambo mengine, unapigiwa simu na mtu amekwama badala umfafanulie vizuri unamwambia kamalize huko huko tumeshawapa maelekezo mpaka vijijini, Mtendaji wa Kijiji anajua taratibu za mikopo kwa undani? Wewe kama umepata fursa ya kutumikia watu watumikie. Kwa hiyo nataka wajirekebishe kwenye masuala yao ya maadili, huko nako wanalalamikiwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)